NA TEGEMEO KASTUS
Dhamana tuliyopewa kama watumishi ni kutumikia wananchi wanyonge, ambao wengi wanakuja kwenye ofisi zetu. Lakini wengine tunawafuata vijijni kwa ajili ya kwenda kuwahudumia, lazima tutoe kauli zenye dhamira ya kuwasaidia. Lazima watumishi tuwe mfano kwa kuheshimu mipaka ya kazi.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbasi Kayanda wakati akiwa anazungumza na wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Karatu. Mh. Kayanda amesema lazima watumishi walinde rasilimali za serikali, amesema rasilimali ni pamoja na afya ya mtumishi mwenyewe, lakini pia kutunza samani za serikali.
Mh. Kayanda amesisitiza kwa wakuu hao wa idara na vitengo juu ya kujenga mahusiano katika utendaji wa kazi. Jambo ambalo litasaidia watumishi kufanya kazi kama timu moja badala ya kufanya kazi kwa makundi. Ameonya juu mahusiano yasiyokuwa na tija katika shughuli za serikali, amesema katika utekelezaji wa majukumu ya serikali undugu na urafiki unauwekwa pembeni.
Wakuu wa idara wa Halmashauri wakiwa wanasikiliza kwa makini Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbasi Kayanda katika kikao kwenye ukumbi wa Halmashauri Karatu
Mh. Kayanda amesema lazima kuwe na uwazi wa fedha zinazoletwa kwenye Halmashauri, lazima wakuu wa idara wafahamu ili waweze kusaidiana katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Mh. Kayanda amesema bado kuna udhaifu katika kushirikiana, amesema mathalani swala la wanafunzi kurudi shuleni kuna maelekezo mahususi yaliyotolewa na wizara ya afya katika kukabiliana na janga la corona. Amesema je wakuu wa idara wamefuatilia juu ya utekelezaji wa maelekezo hayo mahususi ya wizara ya afya ?? amesema lazima tuwe na taarifa za wanafunzi waliokuja shule, na wanafunzi ambao hawajahudhuria tangu shule kufunguliwa. Amesema lazima tujitahidi sana kutekeleza majukumu yetu ndio maana serikali inasema tusikae ofisini.
Mh. Kayanda amesema kuna fedha za miradi ambazo serikali imezileta mwisho wa mwaka wa fedha, amesema fedha hizo zimeingia kwenye utekelezaji wa miundo ya afya na elimu. Hizo fedha zinapaswa kukamilisha ujenzi wa miundo mbinu ya miradi hiyo ndani ya kipindi za miezi mitatu na miradi iendane na thamani ya fedha iliyotolewa. Mh. Kayanda amesema kuna kasumba fedha inatolewa halafu inakaa muda mrefu kwenye akaunti ya shule amesema aina hiyo ya urasimu hapana na haiwezekani kwa sababu fedha imekuja kwa kazi ya utekelezaji wa miradi.
Mkuu wa wilaya ya Karatu akizungumza na wakuu wa idara
Mh . Kayanda ameweka mkazo kwenye swala la vitambulisho vya wajasiriamali amesema kuna vitambulisho 12500 ambavyo imepewa wilaya ya Karatu. Amesema mpaka kufikia tarehe 31 mwezi huu lazima tuwe tumeuza vitambulisho zaidi ya nusu tulivyopewa. Amesema kila mkuu wa idara ahakikishe anasimamia kata yake kwenye zoezi la kuuza vitambulisho vya wajasiriamali, amesema Jumamosi ijayo atakutana na wakuu wa idara wote wamueleze wameuza vitambulisho vingapi na wanampango gani madhubuti wa kuviuza vitambulisho vya wajasiriamali.
Mh. Kayanda amegusia juu ya hali ya usafi amesema mji wa Karatu ni mchafu, sheria za usafi zipo. Ametoa maelekezo kwa mkuu wa idara ya afya pamoja na Afisa mamlaka ya mji mdogo kuja na mkakati wa kufanya mji uwe msafi. Amesema wananchi wapewe elimu kila mtu afanye usafi kwenye eneo lake. Amesema kuna kasumba ya watu kuchukua mifuko ya takataka na kuitupa kwenye mitaro ya barabara na watu kutitririsha maji machafu, amesema hilo haliwezekani. Karatu ni mji wa utalii lazima tubadili madhari ya mji wetu.
Mh. Kayanda amegusia juu ya migogoro mbalimbali amesema kuna migogoro iliyondani ya uwezo wa wakuu wa idara lazima iishe, amemuelekeza Afisa radhi kushughulikia mgogoro wa adhi juu ya mipaka wa kijiji cha Masabeda na Endala. Amesema hataki migogoro inayokaa muda mrefu kama umri wa mtu, amesema maelekezo yanayotolewa na viongozi wa kitaifa au baraza nyie watumishi ni wajibu wenu kutekeleza.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa