NA TEGEMEO KASTUS
Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanywa kila juni 16 tangu ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 na jumuiya ya umoja wa Afrika.
Afisa ustawi wa jamii wilaya ya Karatu Bi ElIzabeth Savini anasema ofisi ya ustawi wa jamii huwa inashughulika na mashauri ya ndoa na madai ya matunzo ya watoto. Anasema huanza kusikiliza katika ngazi ya mtendaji wa kata na ikishindikana malalamiko hupelekwa ngazi ya wilaya kwa hatua zaidi.
Anasema hali kadhalika kwa upande wa madai ya matunzo ya watoto barua huwa inaletwa wilayani kutoka Afisa Mtendaji wa kata wa eneo husika, kama shauri limeshidikana katika ngazi ya kata. Anasema kwa ngazi ya wilaya shauri linachukuliwa hatua mbalimbali kutokana na sheria zilizopo na kama mvutano ni mkubwa basi shauri lianaenda mahakamani. Wilaya ya Karatu ni moja ya wilaya iliyobahatika kuwa na mahakama za watoto kwa ajili ya kushughulikia mashauri ya watoto.
Bi. Savini anasema kwenye madai ya matunzo ya mtoto huwa yanalenga kuwataka wazazi washirikiane kutunza mtoto, badala ya kuacha majukumu kwa mama tuu. Bi. Savini anasema kwa upande wa Mashauri ya familia huwa tunasuluhisha kwa kutoa ushauri kwa kusisitiza wahusika kufahamu na kuvifuata viapo vyao vya ndoa.
Bi. Angle Mwegoha Mwanafunzi (UDOM) wa shahada ya kwanza mwaka wa pili katika fani ya ualimu wa saikolojia na ushauri anaeleza misingi ya familia bora, na inavyosaidia watu kuishi kwa upendo na furaha na inayoweza kupigania maslahi ya watoto ukilinganisha na familia zinazoingia kwenye migogoro.
Familia ni watu wakaribu wanaokuzunguka, watu hao wanaweza wakawa ndugu wa damu au watu wasio ndugu wa damu ila kwakuwa wanahusika na maisha yako wanakuwa sehemu ya familia yako.
Bi, Mwegoha anasema familia inaanza kujengwa na watu wawili ambao wanapaswa kufahamu majukumu yao ya ujenzi wa familia. Anasema kabla ya kujenga familia ni lazima pia kufahamu kwamba katika mapito ya ujenzi wa familia kuna nyakati za raha na nayakati za huzuni. Licha kufahamu lazima wakabiliane na changamoto kwa mazingira waliyonayo na wawe na uhakika wa kile wanachaofanya bila kuiga watu wengine wanafanya nini, kama njia ya kufikia malengo.
Familia lazima ijengwe katika misingi ya kuvumiliana, tukianza katika msingi wa familia ambao ni baba na mama. Bi, Mwegoha anasema baba na mama wakivumiliana familia itakuwa imara hata kama hawana uchumi imara. Hiyo inasaidia kukabiliana na jambo lolote gumu litakalo kuwa mbele yao kwa sababu wameshakubali maisha yao, hivyo kuishi kwa amani na furaha.
Bi. Mwegoha anasema ili kuyatekeleza hayo tunahitaji kufanya uchaguzi sahihi wa mtu utayeingia naye kwenye familia. Anasema mambo ya utandawazi yamekuja kuturahisishia maisha kwa kiasi flani. Lazima tuweze kutawala hali ya usasa wa maisha ili isiwe kichocheo cha kuvunjika kwa familia na kuathiri watoto.
Bi. Mwegoha amesema ni kweli utandawazi umechangia familia kutengana, anasema hasa kwenye matumizi ya simu ambayo mtu hawezi kukaa zaidi ya masaa mawili bila kutumia. Zaidi kwenye ulimwengu wa utandawazi kuna mambo yanayopotosha kabisa maadili na kusababisha ugomvi mkubwa kwenye familia. Bi Mwegoha anasema hii inasababishwa na watu kushindwa kutumia utashi walionao na kuruhusu utandawazi utawale mawazo na akili zao.
Bi. Mwegoha amesema jambo jingine linalosabisha familia kuvunjika ni watu kuishi kwa mazoea. Kila mmoja kusashau jukumu la mwezake. Hii maranyingi inatokana na watu hao awali katika jitihada za kuanza kujenga misingi ya familia kama wapenzi kuishi maisha ya kuigiza. Hivyo kushindwa kuendelea na maisha kuigiza na kuanza kuishi kwa mazoea hivyo kusababisha heshima na upendo kupotea. Bi. Mwegoha anasema inapotokea, mmoja wa wanafamilia kukumbuka maisha ya mwanzo, na kujiuliza mbona hakuna (mashamsham) uchangamfu, ndipo maswali yanaibuka mbona amebadilika ? anasema kama awali muda wa kumjali ulikuwepo iweje kwenye ndoa uwe umetingwa na kazi kuliko ilivyokuwa awali. Hapo ndipo migogoro inapoanza ambayo inawaathiri watoto katika upatikanaji wa mahitaji na malezi bora na kupelekea familia kuvunjjika.
Bi. Mwegoha anasema nyumba inajengwa na mwanamke ni vyema mwanamke kubeba jukumu la kusimamia usalama katika familia na kusimama kwenye nafasi yake kama mama. Baba kama msingi Mkuu wa familia lazima aelewe na kuyatekeleza majukumu aliyonayo kwa familia. Bi, Mwegoha anasema lazima wanafamilia kukumbushana na kuelezana mienendo mema ya familia kwa vitendo.
Bi. Mwegoha anasema hata mtu anayekengeuka na kuamua kuwa na mchepuko bado hakuna uhalisia. Anasema mchepuko unaweza kufanya jambo kwa ajili yako kwa kuigiza ilimradi uone anakujali na anakuthamini na uone mwenza uliyenaye hatoshi. Bi Mwegoha anasema kwa hali ya kawaida unaanzaje kuacha mtu anayebeba aibu zako na kukulelea familia ikiwa pamoja na kuendeleza ukoo wako.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa