Mkuu wa mkoa wa Arusha amefanya ziara katika tarafa ya Eyasi Mang’ola ametembelea miradi na kuzungumza na wanachi pamoja na kusikiliza kero. Katika ziara hiyo mkuu wa mkoa alifanya mkutano wa hadhara na wananchi na kuelekeza azima ya kuongeza maji kwa kuchimba visima.
Mhe. Mrisho Gambo amesema serikali italeta suluhisho la uhakika juu ya tatizo la maji Mang’ola. Amesema alitoa maelekezo kwa Halimashauri kuchimba visima viwili na tayari Halmashauri imeshatenga fedha na kisima kimoja kitachimbwa Dumechang na kisima kingine kitachimbwa Malechang. Amesema amefanya kikao cha ndani na viongozi wanaohusika na maswala ya maji na amezungumza na waziri wa maji Profesaa Mbarawa ni imani kwamba mchoro ule uliofanywiwa kazi na watu wa Bonde la maji la kati ambao umethibitisha Dumechang na Malechang maji yapo. Watu wa DDCA wanaohusika na kuchimba visima ambayo ni taasisi ya serikali watafika na kuchimba visima. Mhe. Gambo amesema watu hao wataangalia kisima cha Jobaj ambacho kinauwezo mkubwa wa kutoa maji wastani wa lita 80000 lakini pampu iliyopale inaonekana ina uwezo mdogo. Amesema katika eneo hilo la Jobaj kuna kisima kingine chenye urefu wa mita 60 na chenyewe hakitumiki, amesema wataalamu wataenda kuangalia kwanini hakitumiki, changamoto zake zitatatuliwa ili kianze kutumika mara moja.
Mhe. Gambo amesema maji yakiongezeka hata ile changamoto ya mgawo wa maji itapungua. Kuna maeneo mengine wanaweza wasitegemee tena maji yale yanayotirika kutoka kwenye chanzo cha maji. Amesema kuna chemchem ipo katika eneo la Mang’ola ambayo ina maji mengi, wataalamu wataenda kuangalia ili nayo iweze kusaidia wananchi katika shughuli za umwagiliaji. Mhe. Gambo amesema wataalamu wa RUWASA watakuja Mang’ola kufanya utafiti kuhusu upatikanaji wa maji na kutoa andiko kwa serikali ili kuweza kubaini na kuondoa changamoto ya maji Mang’ola.
Mhe. Gambo amesema soko la vitunguu Mang’ola linachangamoto, hasa madalali wanaonunua vitunguu kwa bei ya kuwapunja wakulima. Amesema kuna madalali wa ndani na madalali wa nje ambao wanaenda shambani kwa mkulima na kununua vitungu kwa bei ya kumlalia mkulima. Amesema kuna kipindi gunia linauzwa 50000 lakini kuna wakati gunia la vitungu linauzwa 120000 mpaka 150000. Mhe. Gambo amesema serikali imejenga soko pamoja na barabara katika eneo la Mango’la lilogharimu fedha nyingi. Amesema serikali itakuja na mkakati wa kuzuia madalali wa vitunguu Mango’la, amesema kabla ya kutekeleza mkakati huo watawahusisha wananchi ili mkakati huo usiwe na changamoto. Mhe. Gambo amesema wataanza na mpaka wa Namanga kuhakikisha watu hawafungi rumbesa ya magunia ya vitunguu na amesema atahusisha viongozi wa maeneo mengine yanayojihusisha na kilimo cha vitunguu kuzuia kufunga rumbesa katika maeneo yao.
Mhe. Gambo amewaasa wananchi kuheshimu vyanzo vya maji, lakini pia amewaeleza wananchi kuvitunza vyanzo vya maji. Amesema lazima tuje na mkakati wa kupanda miti kuonesha mpaka wa vyanzo vya maji. Amesema wakati serikali ikijipanga kwa zoezi hilo ni wajibu wetu sisi wananchi kuziheshimu mita 60 kutoka chanzo cha maji. Amesema baada ya wiki mbili timu itakuja kukagua vyanzo vya maji na kama kuna mtu atakuwa anajihusisha na shughuli za kibinadamu ndani ya chanzo cha maji hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Naye kaimu afisa maji bonde la kati William Mabula amesema kuna tatizo kupungua kwa maji duniani, na sababu zinazoathiri ni pamoja na mabadiliko ya nchi, kuongezeka kwa joto nchini na ongezeko la watu nchini. Ameomba wananchi kuiheshimu kamati ya jumuiya ya watumia maji Eyasi. Amesema eneo la Eyasi ni eneo lenye utajiri wa maji nchini hivyo njia ya kukabiliana na upungufu wa maji ni pamoja na kutafuta vyanzo mbadala.
Ndugu Williamu amesema kuzuia mafuriko kama ilivyolalamikiwa na wakulima wa Mango’la ni jambo mtambuka linahusisha sekta nyingi. Amesema mambo yanayosababisha mafuriko ni pamoja na kilimo kisicho rafiki kwenye vyanzo vya maji. Amesema ni jambo linahitaji uelewa mpana kwa sababu inawezekana athari za mafuriko zinazopatikana Mang’ola ni athari za wilaya nyingine ambazo matokeo yake yamejitokeza mang’ola. Amesema mabadiliko ya kuondoa hali hiyo ya mafuriko inachukua muda kuanzia miaka 5 na zaidi, ili kuona mabadiliko ya mazingira.
Ndugu William ametoa ufafanuzi juu ya wakulima wakubwa Mang’ola wanaojichukulia maji kienyeji katika vyanzo vya maji na kupeleka mlimani. Amesema sheria inamtaka mtu anayetaka maji kuomba kwa kufuata utaratibu wa kuhusisha jumuiya ya maji ya eneo husika. Wakulima wanaohitaji kutumia maji kiasi kikubwa kwenye mashamba lazima kuangalia kiasi kilichopo kwenye chanzo kabla ya kuruhusu na wanapaswa waombe vibali kwenye jumuia ya kutumia maji ya eneo husika na fomu za kuomba zinapelekwa kwenye bonde. Amesema pamoja na hatua hizo mnufaika wa maji hayo endapo akikubaliwa anapaswa kulipia maji hayo anayoyavuna kwenye chanzo cha maji. Ametoa wito kwa jumuiya ya watumia maji Eyasi kuwatambua watu hao.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa