Na Tegemeo Kastus
Serikali kupitia wadau wa maendeleo shirika la world vision imefanikiwa kufanya ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa nane, kukarabati vyumba vitatu, kujenga ofisi ya walimu, kujenga jiko, matundu kumi na nane ya vyoo na vituo vya kunawia mikono wanafunzi.
Ujenzi na ukarabati huo umefanyika katika shule ya msingi Endabash iliyotembelewa na mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipokagua miradi inayotekelezwa na world vision katika Tarafa ya Endabash. Ujenzi wa miundo mbinu hiyo ikiwemo uwekaji wa madawati katika madarasa, samani za viti na meza kwa ofisi ya walimu umegaharimu kiasi cha shiling 400,500,000 kwa shuke ya Endabash na shule shikizi ya Endabash Saramay ujenzi wa madarasa mawili pamoja na ujenzi wa vyoo vya wasichana umegharimu kiasi cha shilingi 85,500,000.
Muonekano wa shule ya msingi Endabash baada ya ujenzi na ukarabati mkubwa uliofanywa na wadau wa elimu
Mh. Kayanda amewapongeza shirika la world vision kwa usimamizi mzuri wa miradi, amesema ujenzi wa miundo mbinu hiyo ya elimu umebadilisha mazingira ya kujifunzia mwanafunzi. Ujenzi huo wa madarasa umesaidia shule ya Msingi Endabash kupata vyumba vya ziada vya madarasa. Amesema wanafunzi watavutika kusoma zaidi lakini pia amehimiza walimu kuongeza kiwango cha ufaulu kwa kuwaongezea wanafunzi majaribio ya mitihani mingi na kufanya mitihani ya pamoja na shule nyingine za jirani. Amesema kufanya majaribio mengi kutawapa wanafunzi uwezo wa kujibu maswali kwa ufasaha.
Wakati huo huo Mkuu wa wilaya ametembelea na kujionea mradi wa maji wa Endagemu mbao shirika la world vision limeshaujenga. Mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi 192 636,790 kwa kuchimba kisima na kukarabati tanki la maji lenye uwezo wakubeba lita 50, 000,000 ikiwa ni pamoja na kuweka mfumo wa umeme wa jua. Sambamba na kujenga mtandao wa maji ukiwa na vituo 9 vya kuchotea maji.
Mh. Kayanda katika kikao cha ndani na wananchi wa kijiji cha Endagemu amesema ujenzi wa miradi huo ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2020 -2025. Amesema Mradi huo unasaidia familia 450 za kijiji cha Endagemu kupata huduma ya maji safi na salama, amesema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kumtua mama ndoo kichwani. Amesema wananchi wa Endagemu wanatakiwa waone umuhimu wa kuchangia huduma ya maji ili mradi huo uweze kujiendesha wenyewe.
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya Mh. Kayanda amemuagiza Mwenyekiti wa jumuia ya watumia maji Endagemu kurudisha fedha za mfuko wa maji ambazo amezitumia vibaya kabla ya mwezi wa tatu. Mh. Kayanda amesema lazima viongozi wa jumuiya ya watumia maji wawe waaminifu na wajenge tabia ya kusoma mapato na matumizi katika mfuko wa maji inayochangiwa na wananchi.
Mh. Kayanda amesema kwa wale wananchi wenye uwezo, wanaweza kuomba kuunganishiwa maji katika nyumba zao. Amewaelekeza wataalamu wa Ruwasa kuenda kuwajengea uwezo jumuiya ya watumia maji Endagemu na Endawasu ili wasambaze maji kwa wananchi kwa gharama zilizotolewa kwenye muongozo na serikali. Amesema serikali imelenga kuwasogezea wananchi huduma za kijamii karibu.
Amesema ukosefu wa huduma za maji umesababisha adhaa kubwa kwa wakinamama kuchota maji mbali na maeneo wanapoishi. Upatikanaji wa maji safi na salama umesaidia kupunguza magonjwa ya tumbo na kuwapa wananchi muda wa kujikita katika shughuli za maendeleo.
Mh. Kayanda alipotembelea chanzo cha maji Endagemu
Msimamizi wa miradi wa world vision Endabash Ndg. Goodluck Nnko amesema shirika la world vision litaendelea kushirikiana na serikali katika ujenzi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kuboresha huduma kwa jamii. ndg Nnko amewashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaopata wakati wa utekelazaji wa miradi mbalimbali inayofanyika katika tarafa ya Endabash.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa