NA TEGEMEO KASTUS
Kila mtu ambaye ni raia halali wa Tanzania mwenye umri wa miaka kumi na nane na kuendelea mwenye akili timamu kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaruhusiwa kumiliki ardhi. Vigezo vya kugawa ardhi havipaswi kwenda kinyume na katiba ya nchi na haki za binadamu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati akisikiliza na kutatua migogoro ya ardhi katika kijiji cha Chemchem. Ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kutatua migogoro ya ardhi katika eneo husika lenye migogoro ili kujiridhisha kwa kusikiliza pande zote zenye migogoro.
Mh. Kayanda amekemea tabia iliyokuwa imejengeka ya serikali ya kijiji cha Chemchem ya kugawa ardhi kwa wananchi kwa kigezo cha mwenye uhitaji lazima awe ameowa. Kipengele hicho amekifuta na ametoa maelekezo kwa uongozi wa serikali ya kijiji kuhakikisha kila mwenye uhitaji na aliyekidhi vigezo kuhakikisha analipia ada iliyowekwa na Halmashauri ya kijiji, bila kujali kwamba ni mtoto wa kike au mtoto wa kiume. Ametoa rai kwa vijana wa kijiji cha Chemchem kujitokeza na kujiandikisha kuomba ardhi ili wafanye shughuli za uzalishaji katika maeneo watakayokuwa wamegawiwa.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chemchem wakati akisikiliza kero za wananchi.
Mh. Kayanda ameomba watu kuheshimu jitihada zinazofanywa za kutatua migogoro ya ardhi, amesema kama kuna mtu anajambo lake na hajaridhika ananafasi ya kwenda kwenye vyombo vya sheria. Amesema ni wakati sasa wa wananchi wa kijiji cha Chemchem kujikita katika shughuli za maendeleo.
Akizungumza kuhusu upataji wa haki kisheria katika migogoro ya ardhi amesema kwa kawaida migogoro yote ya ardhi inaanza kutatuliwa na mabaraza ya ardhi ngazi ya kijiji, inaenda ngazi ya kata, baadae baraza la ardhi na nyumba ngazi ya wilaya na mahakama kuu kitengo cha ardhi na mwisho ni mahakama ya rufaa. Amesema hizo ni ngazi unaweza kuzifuta kama unaona haki yako hujaipata kwenye upande wa ardhi.
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda amewaambia wananchi wenye malalamiko ya mirathi kuhakikisha wanateuwa msimamizi wa mirathi ili jina lipelekwe mahakama ya mwanzo na liweze kuteuliwa. Amesema hiyo itasaidia msimamizi wa mirathi kuwa na uhalali wa kisheria wa kusimamia malalamiko yake.
Mzee Nicodemus Mwale akizungumza kero yake mbele ya Mkuu wa wilaya ya Karatu
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa