Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla ameitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kufanya maamuzi na majadiliano ya haraka na Mkandarasi Tunnel Sadd Ariana kutoka Nchini Iran anayetekeleza ujenzi wa Bwawa la Eyasi Wilayani Karatu, ili kujua hatma ya utekelezaji wa mradi huo unaosuasua kwa kipindi kirefu.
Mhe. Makalla amebainisha hayo Jumanne Septemba 23, 2025 alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo, akionesha kusikitishwa na kusuasua kwake ambapo mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia nne pekee ya utekelezaji wake ilihali ulitakiwa kuwa umefikia asilimia 90 kufikia hivi sasa huku pande zote za Mkandarasi na Tume wakiwa na sababu tofauti kama sehemu ya vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji wake.
“Mimi kama Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa Kamati ya usalama nishauri na kupendekeza kwa Tume kwamba mkae na Mkandarasi kama hana sifa ya kuendelea ni bora mkawa na makubaliano ya pande zote mbili tukaachana na tukatafuta Mkandarasi mwingine. Wananchi wana matarajio na mradi huu hivyo jambo hili lifanyike kwa haraka.” Amesema Mhe. Makalla akisisitiza kuzingatiwa kwa taratibu za kisheria katika majadiliano yao.
Awali katika maelezo yake, Mhe. Mkuu wa Mkoa akizungumza na Maofisa wa Tume ya Umwagiliaji pamoja
na Wakandarasi hao ameeleza kuwa serikali imetenga
Bilioni 21 na Milioni 831 katika kutekeleza mradi wa bwawa hilo ili kuondoa changamoto ya mafuriko kwenye Kata za
Mang’ola na Baray za Wilayani Karatu Mkoani Arusha pamoja na kuzisaidia Kata hizo katika kuimarisha Kilimo cha Umwagiliaji.
Kwa upande wake Bw. Leopard Lunji, Mkurugenzi wa Idara ya miundombinu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
amemueleza Mhe. Makonda kuwa ndani ya wiki mbili zijazo wataketi na Mkandarasi huyo ili kufanya makubaliano ya pamoja katika kutekeleza maagizo na maelekezo ya Mhe.Makalla ili wananchi waweze kunufaika na mradi huo kwa wakati
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa