Rc Makalla ataja Mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa wananchi akiagiza mradi ukamilike haraka_
Wananchi wa Vijiji saba vya Kata za Mang’ola na Baray Wilayani Karatu Mkoani Arusha wamemshukuru Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa ujenzi wa mradi mkubwa wa skimu za Umwagiliaji za bonde la Eyasi, Mradi wenye kugharimu Shilingi Bilioni 38, 434, 137, 621. 18, wakisema mradi huo umekuwa na manufaa makubwa katika kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara katika eneo hilo.
Wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla leo Jumanne Septemba 23, 2025, wakati wa ukaguzi wa mradi huo, wananchi hao wameeleza pia namna ambavyo wamenufaika na ruzuku za mbolea na pembejeo za kilimo, wakisema maendeleo ya Kata zao kwasasa na ukuaji wa uchumi unaoshuhudiwa umetokana na tija kubwa wanayoipata kwenye kilimo cha Vitunguu, Mpunga na mahindi.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa, Bw. Joseph Hitla, Mkazi na Mkulima wa Kijiji cha Maleckchand amemshukuru pia Mhe. Makalla kwa kusimamia vyema utekelezaji wa shughuli za serikali katika eneo hilo pamoja na kuwatembelea kwenye mashamba yao, akisema Mhe. Makalla amekuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza kutembelea mashamba hayo na kukagua shughuli za kilimo zinazoendelea katika eneo hilo.
Kulingana na CPA Makalla, kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wananchi wa Vijiji vya Mang’ola Barazani, Maleckchand, Laghangarer pamoja na Vijiji vya Qang’dend, Mbuga nyekundu, Jobaj na Dumbechand, akiagiza Mkandarasi na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuongeza kasi kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa Kimkataba.
Mradi wa skimu za umwagiliaji Bonde la Eyasi unatekelezwa na Mkandarasi M/S CRJE (EA) Ltd wakiingia makubaliano na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji mnamo Machi 30, 2023 kwa Mkataba wa miezi 18 ya kiutekelezaji, mradi ukitarajiwa kukamilika na kukabidhiwa rasmi serikalini kufikia Machi Mosi mwaka 2026.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa