Na Tegemeo Kastus
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Karatu lakusudia kukaa na wawekezaji wa mashamba makubwa ili kusaidia kuondoa vichaka na mapori ambayo yamekuwa hifadhi ya wanyamapori katika maeneo ya makazi ya watu. Kikao hicho kitalenga kujenga na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya wananchi na wawekezaji na kuhimiza wawekezaji kuendeleza maeneo ambayo hawajaendeleza.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya karatu, Mh. John Lucian katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya tatu ya mwaka. Kikao ambacho katika siku yake ya kwanza taarifa za maendeleo ya kata zimewasilishwa, Mh. Lucian amesema ameshawaalika wawekezaji wa mashamba makubwa kata ya Oldean, Ofisini kwake ili kufanya nao mazungumzo. Amesema lengo kubwa ni kuimairisha mawasiliano na ukarabati wa barabara zinazoingia na kutoka katika kata hiyo, amesema muwekezaji wa shamba la Tembotembo na Agacia wamekubali kutoa fedha kwa ajili kutengeneza barabara itakayopita nje ya mashamba na ofisi zao.
Watendaji wakiwa katika kikao cha cha robo ya tatu ya mwaka ya baraza la madiwani
Mh. Lucian amesema katika kujenga mazingira ya usalama barabara itayopita nje ya mashamba ya wawekezaji hao itasaidia kuwapa wananchi uhuru wa kuitumia, amesema ni lazima kulinda na kuimarisha mazingira mazuri ya uwekezaji. Wawekezaji hawa lazima walindwe kwa sababu wanaipatia serikali kodi ambayo inaenda kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo. Ameongeza kusema katika kikao hicho watawaomba wawekezaji ili kupata sehemu ya maeneo kwa ajili ya wananchi kufanya shughuli zao za uzalishaji. Amesema wananchi wengi wanaoishi katika kata ya Oldean hawana kipato kutokana na kuwa na maeneo machache ya kilimo.
Naye Mh. Maria Patrice diwani wa viti maalumu amesema katika kusaidia kutatua changamoto katika eneo la Oldean amesema kumekuwa na mkwamo kwa sababu mara nyingi wakifanya vikao wanakutana na mameneja wa mashamba. Amesema vikao vingekuwa na tija zaidi kama vingefanywa na wamiliki wenyewe wa maeneo husika ambao wanakauli juu ya maeneo yao ya uwekezaji.
Amesema miaka ya nyuma wananchi walikuwa wanaruhusiwa kulima maharage na mahindi hivyo kuzuia hatare ya wanyama pori kujificha katika vichaka vilivyoachwa katika maeneo ya uwekezaji. Amesema sasa hivi wananchi wamezuiwa kujihusisha na kufanya shughuli za kilimo hivyo kufanya kuwa eneo lenye vichaka na kusababisha wanyama pori kuishi katika vichaka hivyo. Mh. Patrice diwani wa viti maalumu amesema kuna jitihada za dhati zilizofanywa na serikali ikiwa ni pamoja na kulichukua eneo la (Rivacu) Rift Valley Cooperative union ambalo Halmashauri ililitenga eneo kwa ajili ya wananchi kupata eneo la makazi. Lakini bado wananchi wanahitaji maeneo zaidi kwa ajili ya kujihusisha na shughuli za kilimo na makazi.
uwasilishaji wa taarifa za maendeleo za kata ukifanyika katika siku ya kwanza ya baraza la madiwani
Akizungumza katika baraza hilo mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu Ndg. Waziri Mourice amesema swala la kuzungumza na wawekezaji wa mashamba ili waridhie kutoa sehemu ya maeneo kwa wananchi liangaliwe kwa tafsiri ya sheria. Amesema kama muwekezaji anaridhia kutoa sehemu ya ardhi kadri atakavyowiwa ni vyema akatoa nyaraka za umiliki wa eneo ili ziweze kurekebishwa. Ili kuja kuondoa migongano ya kisheria baadae kati ya muwekezaji na wananchi kuliko kutoa ahadi za maneno peke yake.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa