NA TEGEMEO KASTUS
Watendaji wa serikali wanapaswa kuacha utaratibu wa kufanya malipo nje ya mfumo, kwenda kinyume na kanuni na sheria za fedha kunaleta hoja na taswira mbaya kwa Halmashauri. Hii itawezesha Halmashauri kuepuka hoja za ukaguzi za kujirudia rudia na kuasaidia wananchi katika kutoa huduma bora.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda aliyekuwa akimuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Arusha katika kikao cha baraza la madiwani maalumu cha kujadili hoja za mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali. Ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Karatu kwa kupata hati safi kwa mwaka uliopita wa fedha. Sambamba na pongezi hizo Mh. Kayanda amesema katika akaunti ya amana kuna fedha zilitolewa, miongoni mwa fedha hizo zilikuwepo fedha za mradi wa maji Ruwasa, ambazo zinapaswa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maji ya Ruwasa. Ameelekeza fedha hizo na nyingine zilizochukuliwa katika akaunti ya amana zirejeshwe kama taarifa ya baraza ilivyosema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu Mh. John Lucian (katikati) akiendesha kikao cha baraza la madiwani maalumu cha kujadili hoja za mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za serikali.
Amesema Halmashauri lazima ijiimarishe katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato, wafanyabiashara ambao leseni zimeisha muda wake, lazima ufuatiliaji ufanywe na watendaji ili walipie leseni za biashara zao. Amesema kila mtumishi asimame kwenye nafasi yake bila kuwepo hali ya kutegeana ili kusaidia Halmashauri kupiga hatua kiutendaji katika kutekeleza matakwa ya kisheria yanayotaka Halmashauri kutenga 40% kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Akizungumzia kuhusu hoja za ukaguzi Mh. Kayanda amekemea tabia iliyojitokeza ya watendaji kutowajibika katika majukumu yao ya kazi. Amesema kuna ufuatiliaji usioridhisha wa fedha zilizokusanywa za mapato katika kuzihifadhi benki, lazima watendaji waongeze ufutiliaji wa ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha fedha zimeenda benki.
Matukio mabalimbali katika picha wakati wa kikao cha baraza la madiwani
Ameongeza kusema Afisa usafirishaji lazima akague vitabu (log book) ili kujiridhisha kama vimejazwa kwa usahihi ili kudhibiti matumizi mabaya ya mafuta. Kuna urejeshwaji wa 10% ya mikopo katika mfuko wa wanawake vijana na walemavu kazi inayoratibiwa na idara ya maendeleo, lazima fedha zirejeshwe kama inavyopaswa. Amesema ni lazima kila mtendaji aliyehusika na kusababisha hoja za ukaguzi kwa uzembe hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake.
Akizungumza katika kikao hicho Kaimu Katibu tawala wa mkoa wa Arusha Bi. Suzani Mnafe amesema lazima udhibiti wa ndani wa Halmashauri uongezeke. Amesema udhibiti wa matumizi ya ndani ya fedha ukiongezeka utasaidia kuondoa hoja za kizembe. Amesema swala la bodi ya uzabuni katika Halmashauri ya Karatu kutokukaa kwa kipindi cha mwaka mzima ndio imechangia hoja nyingi za Mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. John Lucian amesema fedha za serikali zisitumike kwa matakwa ya mtu binafsi. Halmashauri inapaswa kuongozwa kwa taratibu na miongozo iliyowekwa. Amesema maswala ya watendaji wa kijiji au kata wanaojihusha ubadhilifu katika eneo lake la kiutendaji hatua za kinidhamu zichukuliwe hapo hapo. Amesema utaratibu wa kumuhamisha Mtendaji, eneo la utendaji kazi haujengi na badala yake linagharimu Halmashauri hasa katika gharama za uhamisho za kiutumishi za kumuhamisha mtendaji kwenda kituo kingine cha kazi.
Matukio tofauti katika picha wakati wa kikao cha baraza la madiwani
Akizungumza kuhusu watendaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu Ndg. Waziri Mourice amesema maelekezo yote yaliyotolewa kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali yatatekelezwa kama baraza lilivyoelekeza. Amesema Halmashauri kupata hati chafu inaweka doa katika utendaji wa kazi.
Naye diwani wa kata ya Oldean Mh. Peter Mmasi akichangia katika baraza hilo amesema lazima Halmashauri ya Karatu iongezee rasilimali watu watakaosaidia katika ukusanyaji wa kodi katika maeneo ya vijijini. Amesema hiyo itasaidia, kuainisha wafanyabiashara wa vijijini pamoja na aina ya biashara wanazofanya. Amesema wilaya ya Karatu inautajiri wa rasilimali lakini bado kuna vyanzo vingi vya mapato ambavyo havijaingia katika mfumo rasmi wa ulipaji wa kodi.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa