Na Tegemeo Kastus
Halmashauri lazima ikusanye mapato vizuri ili iweze kutekeleza shughuli zake za miradi maendeleo, ni jukumu letu kusimamia ukusanyaji wa mapato katika kata zetu. Halmashauri imekisia kukusanya kiasi cha billion nne na million mia tano kwa mwaka huu wa fedha.
Mh. Abbas Kayanda amesema hayo wakati akihutubia katika kikao cha kwanza cha baraza la madiwani. Vyanzo vya mapato vilivyoainishwa kwenye bajeti visimamiwe vizuri, ili vitoe mapato yaliyokusudiwa. Tunahitaji madawa, tunahitaji kujenga zahanati, tunahitaji kujenga madarassa tunahitaji kujenga nyumba za walimu, tunahitaji kujenga lami Karatu, vyote hivyo vinategemea namna tutakavyokusanya mapato.
Mh. Kayanda amesema kuna umuhimu wa kudai risiti za za EFD pindi tunaponunua bidhaa madukani ili kuongezea ukusanyaji mapato serikalini. Tuendelee kufikiria vyanzo vingine vya mapato ambavyo hatujavigusa katika maeneo yetu. Lazima tushirikiane ili tuweze kufikia malengo tuliojiwekea.
Mkuu wa wilaya ya karatu Mh. Abbas Kayanda akizungumza katika kikao cha kwanza cha baraza la madiwani
Akizungumzia kuhusu elimu Mh. Kayanda amesema kuna fedha nyingi zinazokusanywa kwa miradi mbalimbali ya elimu. Amesema wazo la kuunda mfuko wa elimu litamsaidia kumpunguzia mwanachi, mzigo wa kuchangia mara kwa mara ujenzi wa miundo mbinu ya elimu. Amesema kuna kazi kubwa ya kufanya kuinua kiwango cha ufaulu kwa elimu ya msingi, tukiimarisha mfuko wa elimu itatusaidia kuwapa motisha walimu wanaofanya vizuri.
Mh. Kayanda amesema katika shule za sekondari bado ufaulu hauko vizuri, lazima tutafakari kwa umoja wetu namna ya kuondoa ufaulu wa daraja sifuri na daraja la nne. Tuna kazi kubwa ya kufanya ili tuweze kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa sekondari.
Mh. Kayanda amesema katika sekta ya afya kumekuwa na mwitikio wa chini kwa wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya ya jamii. Tuwaelimishe wananchi juu ya umuhimu wa kujiunga katika mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa. Amesema wananchi wakijitokeza kujiunga na bima ya afya vituo vyetu vya afya na zahanati vitaongeza upatikanaji wa madawa na vifaa tiba.
Amesema bado kuna changamoto ya wakinamama kwenda kujifungua katika vituo vya kutoa huduma za afya, lazima wakinamama wahamasishwe kwenda kujifungua katika vituo vya huduma za afya. Vituo vya afya visivyo katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato kieletronic vinatakiwa viwe na mfumo wa ukusanyaji wa mapato ili kuondoa upotevu wa ukusaanyaji wa mapato.
picha katika matukio tofauti wakati Mh. Abbas Kayanda akizungmza katika kikao cha baraza la madiwani
Akizungumzia kuhusu ustawi wa jamii Mh. Kayanda amesema Halmashauri ya Karatu ilitambua wazee 7776 kati ya wazee hao waliobahatika kupata vitambulisho vya matibabu bure ni 3037. Amesema lazima tujipime katika kipindi cha miaka mitano, tutaifanyia nini jamii yetu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. John Lucian Mahu amesema baada ya baraza kujigeuza kamati imepitisha wazo la kuanzisha mfuko wa elimu wa wilaya ya Karatu. Amesema wazo limekuja kwa sababu tumekuwa tukisuasua sana katika kuinua kiwango cha ufaulu. Amesema wazo hilo limeafikiwa lipelekwe kwenye kamati maalumu itakayoundwa na Mkurugenzi ambayo itasaidia kuchakata na kupeleka maoni katika kamati tendaji ya Halmashauri (CMT) ili ije na mapendekezo ya namna ya kutekeleza wazo la mfuko wa elimu wa jimbo. Mh. Mahu amesema baaada ya kujadiliwa mawazo hayo yatapelekwa katika kamati ya fedha na baada ya hapo itapelekwa kwenye baraza na tutaanzisha mfuko wa elimu wa wilaya ya Karatu.
Mh. Mahu amesema wazo jingine lilojadiliwa na baraza lilojigeuza kama kamati imeridhia kuhamisha mnada wa Karatu kwenda nje ya mji wa Karatu. Amesema sasa upande wa juu wa eneo la mnaada itajengwa stand ya kisasa ya mabasi makubwa na eneo la upande wa chini utajengwa uwanja wa mpira wa kisasa na viwanja vingine vya michezo na upande mwingine wa eneo hilo watajenga ukumbi wa kisasa wa mikutano wa Halmashauri. Amesema kamati pia imeridhia kujengwa kwa hosteli za wasichana na hosteli za wavulana kama sehemu mojawapo ya kubuni vyanzo vipya vya mapato katika eneo hilo la uwanja wa mnadani.
Mh. Mahu amesema zoezi la kuhamisha eneo la mnada litafanyika taratibu na mnaada utapelekwa katika eneo jingine nje ya mji. Stand ya sasa ya mabasi itatafutiwa kazi nyingine kadri itakavyoonekana inafaa. Mh. Mahu amesema lazima tushirikiane kwa pamoja wataalamu na watendaji ili tuwafute machozi wananchi. Amesema kusimamia mapato sio kazi ya mkurugenzi ni kazi yetu sote ili tuweze kupunguza madeni tunayodaiwa kama Halmashauri.
wataalamu katika matukio tofauti wakifuatilia kikao cha Baraza
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ndugu Waziri Mourice amesema utaratibu mzuri utawekwa kwa ajili ya kuunda mfuko wa elimu wa jimbo. Amesema mfuko wajimbo hautagusa wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea. Amesema mfuko utakusanya michango kwa wananchi wenye umri wa miaka 18 -59. Amesema elimu imeboreshwa na hivyo tuanatarajia ongezeko kubwa la wanafunzi.
Akizungumzia kuhusu afya amesema kila kata inatakiwa iwe na kituo cha afya na kila kijiji kinatakiwa kiwe na zahanati lakini hatuna zahanati kila kijiji. Amesema tuna kata 14 ambazo kila kata ianatakiwa kuwa na kituo cha afya lakini kwa sasa serikali inavituo 5 vya afya. Amesema hali hiyo inasababisha vituo vya afya kuzidiwa kutokana na wingi wa watu kutokana na ubora wa huduma na bei nafuu zinazotolewa katika vituo vya afya vya serikali.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa