Na Tegemeo Kastus
Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Karatu limetenga million 100 kwa ajili ya kukabiliana na janga la corona. Fedha hizo zimetengwa ili kununua vifaa tiba madawa pamoja na na kuandaa miundo mbinu salama kwa ajili ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19.
Mwenyekiti wa Halmashuri Mhe. Lazaro Gege amesema kama kutakuwa kuna uhitaji wa baraza kukaa basi litakaa ili kujadili namna zaidi ya kukabiliana na janga la corona. Ameomba kamati ya kupambana na corona ya wilaya kuweka mkakati wa kutoa elimu zaidi kwa wananchi. Amesema zile fedha kwa ajili ya mgao wa maadhimisho na shughuli mbalimbali ambazo zilikuwa zifanyike, mchanganuo wake upelekwe kamati ya fedha kwa ajili ya kuidhinishwa. Ameomba kamati ya kupamabana na virusi vya corona iweke kipaombele katika kuwapatia wananchi elimu zaidi juu ya maambukizi ya virusi vya corona.
Diwani wa kata ya Daa Mhe. Benedicto Modaha akiwa katika kikao cha baraza la madiwani
Mhe. Theresia Mahongo amepongeza hatua ya baraza hilo la madiwani kwa kutenga kiasi hicho cha Million 100 kwa ajili ya Kupambana na Corona. Mhe. Mahongo amesema awali kanisa la sabato, kanisa la KKT na watu binafsi wamechangia fedha kwa ajili ya kukabiliana na janga la corona. Kiasi cha michango hiyo kimetumika kununua dawa pamoja na mahitaji mengine, ambayo yanasaidia kukabiliana na janga la virusi vya corona. Mhe. Mahongo amewapongeza sana watu wa afya kwa jitihada wanazofanya, amesema kwenye karantini lazima kuwepo askari Mgambo ili washukiwa wasitoke. Amesema kuna utaratibu maalumu kwa watu walio karantini wakiwa wanamahitaji wanawapa fedha wahudumu wa afya ambao wanawanunulia mahitaji na kuwaletea watu hao walio katika karantini.
Mhe. Mahongo ametoa wito kwa wananchi kufanya shughuli za mazishi kwa idadi isiyozidi watu 30 ili kupunguza misongamano. Amesema kuna watu wamekaa usiku wanacheza Pooltable wanacheza karata, watu wanakunywa pombe za kienyeji bila utaratibu. Ameomba maafisa Tarafa kuchukua hatua za kulinda usalama kwa wananchi kwa kuzuia vitendo vinavyoweza kuongeza maambukizi kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya Corona. Mhe. Mahongo Amemjumuisha Mwenyekiti wa kamati ya elimu afya na maji Mhe. Yotham Manda kuwa mjumbe katika kamati ya wilaya inayokabiliana na Virusi vya corona.
Mkurugenzi Mtendaji ndg. Waziri Mourice amesema janga tulilonalo ni kubwa tunahitaji kufanya maamuzi. Amesema kiwango cha 60% kinachotengwa kwa ajili ya uendeshaji wa Halmashauri ukiangalia namna bajeti inavyopangwa na utekelezaji wake si kweli matumizi yote ya uendeshaji ni 60%. Ndg. Mourice amesema kununua gari la Mkurugenzi si kipaumbele sana, kuna watumishi wanakaa geti la Manyara ambao wanapima joto kila mwanachi anayeingia Karatu na gharama za ufutiliaji zinabebwa na Halmashauri. Amesema kuna watumishi wanatoa tiba bado ni hiyo hiyo 60% inatumika ameomba madiwani kutotizama swala la kutenga fedha kwa kuangalia bajeti ya uendeshaji wa Halmashauri na badala yake litizamwe pande zote.
Mganga mkuu wa wilaya Dkt. Musatafa Waziri amesema mpaka sasa elimu imetolewa kwa watumishi wote na elimu hiyo ni endelevu. Amesema elimu imetolewa kata zote kwa njia ya kutangaza kwa kutumia gari la matangazo. Kuandika barua kwa Mafisa watendaji kata wote kutoa elimu na kuchukua tahadhari ya virusi vya corona. Kutoa elimu nyumba za ibada, mahotel, mamantilie pamoja na nyumba za kulala wageni, juu ya namna ya kujikinga na virusi vya corona. Dkt waziri amesema wamehamasisha jamii juu ya kuweka na kunawa na maji tiririka na sabuni kwenye sehemu zote za biashara nyumbani na maeneo yote yenye mikusanyiko. Dkt waziri amesema wametoa elimu kwenye minada pamoja na masoko lakini pia kutambua kwa kutenga maeneo ambayo wagonjwa wanaweza kukaa pindi ikitokea kisa cha mgonjwa wa corona. Waganga wafawidhi wamepewa maelekezo kwenye vituo vyote vya afya kuweka chumba maalum cha kumhifadhi mshukiwa wa ugonjwa wa corona kwa muda, wakati hatua nyingine za kitabibu zikiendelea kwa mujibu wa miongozo.
Madiwani wakiwa katika kikao cha robo ya tatu wakifuatilia kwa makini mjadala
Dkt. waziri amesema watenga shule ambazo zitatumika kuweka wagonjwa, endapo itatokea wagonjwa wengi wa virusi vya corona, shule hizo ni Karatu sekondari na Ganako. Amesema vikao mbalimbali vya afya vinakaa kwa ajili kubaini changamoto na kuzitatua na kutoa elimu kwa wahudumu wa afya.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa