Na Tegemeo Kastus
Shirika la World Education Initiative (WEI) Bantwana; waache wasome ambalo lipo chini ya ufadhili wa watu wa marekani USAID, limefanya mdahalo juu ya kupinga ukatili wa kijinsia katika uwanja wa Mnadani wilayani Karatu.
Mkuu wa wilaya ya Karatu, Mhe. Theresia Mahongo katika hotuba yake ya ufunguzi amepongeza shirika la (WEI) bantwana kwa kuandaa mdahalo huo. Mhe. Mahongo amepongeza wananchi wanaojihusisha na shughuli za bodaboda kwa kazi ya kubeba vijana na kupeleka shuleni. Amesema wanawake wote wanatambuliwa duniani, ndio maana Tanzania Mhe. Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuliona hilo alimchagua msaidizi wake ambaye ni makamu wa Rais kuwa mwanamke. Amesema Makamu wa Raisi Mhe. Samia Suluhu ndiye atakayekuwa Mgeni rasmi wa kilele cha siku ya wanawake huko mkoani Simiyu. Mhe. Mahongo amesema mwaka jana wilaya ya Karatu ilikuwa na mimba 25 za watoto wa sekondari na mimba 5 kwa watoto wa shule ya msingi amesema hicho ni kitendo kinachoumiza sana kwa mzazi.
Mhe. Mahongo amesema mzazi anamuandaa binti yake kuwa mfanyakazi au kiongozi ili baadae aje kusaida familia; anapokumbwa na watu wanao mlaghai, binti zile ndoto zake zinayeyuka. Amesema binti anakuwa bado ni mtoto na anapata mtoto katika umri mdogo na anakuwa ni mzigo kwa mzazi. Ametoa wito kwa madereva bodaboda kujali mabinti, kwa kuwaacha wasome ili watimize ndoto zao. Amesihi madereva bodaboda kuwa mfano katika wilaya ya Karatu kwa kuwatoa watoto sehemu husika kuwapeleka shuleni kama wakienda kuwachukuwa shuleni basi wawarudishe nyumbani wakiwa kwenye mikono salama.
Mhe. Mahongo amewaomba wananchi wa Karatu kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa korona, kwa kuepuka kupeana mikono. Amesema ugonjwa huu umesambaa kwa nchi takribani 84 duniani kwa sasa, ameomba wananchi kuwa makini na kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa idara ya afya. Amesema wilaya ya Karatu imeshajiandaa kukabiliana na ugonjwa huo lakini bado amehimiza wananchi kuchukua tahadhari kubwa juu ya ugonjwa huo.
wananchi wakifuatilia Mjadala kwa umakini katika uwanja wa mnadani wilayani Karatu.
Mtaalamu wa jenda na jinsi na jinsia katika shirika la (WEI) ambalo liko chini ya udhamini wa watu wa marekani Bi, Grace Muro amesema wamejikita katika kufanya kazi katika shule za sekondari za kutwa mbazo zimekuwa na tatizo kubwa la watoto wa kike kukatishwa masomo yao kwa sababu ya mimba. Amesema wao kama (WEI) wamekuja kufanya kampeni ili jamii iweze kuwa na uelewa juu ya athari za mimba za utotoni, amesema hawa watoto wa kike ni wakinamama tunaotarajia kuleta maendeleo siku za usoni. Lazima tuhamasishe jamii kuacha mila potofu zinazofanya mtoto kike kuwa duni, amesema tumelenga kampeni yetu kwa hawa madereva wa bodaboda ambao kidole kinalenga kwao waweze kuchangia maendeleo ya mtoto wa kike. Ameomba madereva bodaboda kuwaona watoto wa kike kama dada zao, na wajikite katika shughuli za kujipatia kipato.
Ndugu John Lucian Katibu wa madereva bodaboda wa zamani amesema lazima watoto wa kike nao wawe na maadili lakini amesisitiza kuongeza elimu ya madili kwa wazazi. Amesema lazima wazazi wajenge mabweni ili wanafunzi wa kike wawe shuleni au wajenge shule za sekondari karibu na maeneo ambayo ni rafiki kwa wanafunzi kike ili wanaweza kufika kwa urahisi shuleni. Amesema kuna tatizo la mimba kwa watoto wa kike ambalo linamalizwa kinyumbani jambo ambalo linafanya kesi za mimba kuendelea kuongezeka. Ameomba wanaohusika na utetezi wa haki za kisheria za watoto wa kike kupata mimba mashuleni, kuongeza umakini.
Wananchi wa wilaya ya Karatu katika matukio tofauti kwenye picha wakati wa uchangiaji wa mjadala wa unyanyasaji wa kijinsia katika uwanja wa mnadani wilayani Karatu.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa