Na Tegemeo Kastus
Ujenzi wa maabara ya chemia katika shule ya sekondari Getamock unandelea kwa kusuasua na kushindwa kukamilika kwa wakati. Ujenzi huo uko katika hatua za awali za uwekaji wa mifumo wa gesi na maji, kinyume na maelekezo ya serikali iliyoelekeza ukamilishwaji wa miundo mbinu hiyo uwe umekamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu fedha hizo kutolewa.
Jengo la maabara ya sekondari Getamock kwa ndani ambalo bado halijamalizika ujenzi
Hayo yamejiri katika ziara ya Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipokuwa akitembelea kujionea ukamilishwaji wa maboma ya maabara kwa fedha zilizotolewa na serikali inayoongozwa na Mh. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukamilisha maboma ya maabara. Mh. Kayanda ameonesha kutoridhishwa na hatua za ujenzi wa shule ya sekondari Getamock, baada ya kukuta stuli 34 za kukalia wanafunzi katika maabara hiyo kugharimu kiasi cha million 2120,000 ukiwa ni wastani wa shilingi 62000 kwa kila stuli.
Stuli thelathini na nne zinazodaiwa kununuliwa kwa gharama ya million mbili.
Mh. Kayanda katika ziara hiyo amebaini baadhi ya walimu wanaofundisha katika shule hiyo kuingia ubia wa shughuli binafsi, kusambaza vifaa vya ujenzi katika maabara hiyo ya Getamock sekondari. Utaratibu huo wa walimu kuingia tenda ya kufanya shughuli binafsi kwenye taasisi wanayoitumikia ni kinyume na taratibu za utumishi wa umma ambazo zimezuia mtumishi kuwa na ubia wa biashara ili kuondoa mgongano wa maslahi (conflict of interest) kati ya taasisi na shughuli zake binafsi. Mh. Kayanda amebaini ununuzi wa kiasi kikubwa cha saruji mifuko 250 kinyume na BOQ ya ujenzi wa jengo hilo unaoonesha uhitaji wa ujenzi wa maabara hiyo ni mifuko 106.
Kaimu Mhandisi wa wilaya Riziki Msite akikagua ujenzi wa darasa Shule ya Msingi Shauriawack.
Mh. Kayanda amebaini licha ya ushauri wa kaimu Mhandisi wa ujenzi wa Halmashauri katika ujenzi maabara hiyo bado kamati ya ujenzi wa shule ya Getamock imeshindwa kusimamia ushauri wa kitaalamu wa mwandisi wa ujenzi. Mh. Kayanda amesema nyaraka za manunuzi ya ujenzi zinatia shaka, hivyo ameelekeza taasisi ya kupambana na rushwa kufanya uchunguzi wa nyaraka za manunuzi za maabara ya shule ya sekondari ya Getamock. Sambasamba na hatua hizo Mh. Kayanda ameelekeza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kufanya uchunguzi ili kujiridhisha na matumizi ya fedha katika mradi wa maabara katika shule ya sekondari ya Domel. Shule hiyo ilikuwa na gofu la maabara ambalo lililikuwa limeshapauliwa bati na limetumia kiasi million 28 kati ya kiasi cha million 30 zilizotolewa na serikali.
Mh. Kayanda amesema kiasi hicho hicho cha fedha kimetolewa kwa shule sekondari Mang’ola na Diego na kila moja kupewa million 30 na wameweza kumalizia maboma na kubakia na fedha ambazo wameziombea kuzitumia kwa ajili ya matumizi mengine, kwa idhini ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Karatu. Amesema serikali ilipoweka utaratibu wa kutumia Force Account ililenga kupunguza gharama za ujenzi na kuwezesha fedha hizo kutumika katika miradi mingine yenye uhitaji wa kuimarisha miundo mbinu.
Muonekano wa jengo la darasa kwa nje shule ya Msingi Shauriawack
Katika ziara hiyo Mh. Kayanda ametembelea ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari Qaru ambayo nayo imepewa kiasi cha million 30 kwa ajili ya ukamilishwaji wa boma la maabara. Mh. Kayanda ameridhishwa na ujenzi wa maabara hiyo na amepongeza usimamizi mzuri wa kamati ya ujenzi wa shule sekondari ya Qaru. Amesema katika ujenzi wa miundo mbinu lazima miradi iendane na thamani ya fedha zilizotolewa na serikali.
Mh, kayanda ametemebelea ujenzi wa darasa katika shule ya msingi Shauriawack iliyopewa kiasi cha million 12 kwa ajili ya ukamilishwaji wa boma la darasa. Mh. Kayanda ameridhishwa ma ujenzi, amepongeza kamati ya ujenzi kwa kushirikiana na wazazi kwa ujenzi darasa hilo. Ameelekeza darasa hilo kuanza kutumika mapema wiki ijayo shule zitakapofunguliwa.
Kazi ya umaliziaji wa boma la maabara katika shule ya sekondari ikiwa inaendelea.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa