NA TEGEMEO KASTUS
Mkuu wa wilaya Mh. Abbas Kayanda ameelekeza kwa wenyeviti wa vitongoji kuwa na daftari la wakazi, ili kujua wananchi wanaoingia katika kijiji cha Matala.amesema lazima wageni wanaoingia katika vitongoji kutambuliwa na kufahamika na viongozi wa vitongoji.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya wakati akihutubia mkutano wa hadhara kwa wananchi wa Matala. Amesema kijiji cha Matala kimekuwa na matukio ya uhalifu mengi ambayo hayaripotiwi kwa viongozi wa ulinzi na usalama.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Matala
Mh. Kayanda amesema kutakuwa na mafunzo ya jeshi la akiba (mgambo) kuanzia mwezi wa tisa ili kudhibiti vitendo vya uhalifu katika kijiji cha Matala. Mafunzo hayo yatahusisha vijana wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, amesema mafunzo hayo ni lazima kufanyika baada ya awali kushindwa kufanyika. Mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika kijiji cha Matala, lakini pia yatasaidia kujengwa ari ya uzalendo kwa vijana dhidi ya nchi yao. Mh. Kayanda amesema wananchi wa Matala wakiwa na amani itasaidia kufanya shughuli zao za kimaendeleo vizuri.
Mh. Kayanda amesema lazima wananchi wajitolee kujenga kituo cha polisi katika kijiji cha Matala. Amesema wakishaanza kujenga Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu ameahidi kutoa Mabati kwa ajili ya kuezeka jengo la kituo cha polisi Matala.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda katika Matukio tofauti akikagua eneo la Pampu ya maji Matala kabla ya mkutano wa Hadhara.
Mh. Kayanda amesema kuna mradi wa maji Matala ambao serikali imetoa kiasi cha million 300 kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya Maji lakini kuna baadhi ya watu wamefanya hujuma na kuharibu miundo mbinu ya maji. Amesema lazima kuimarisha ulinzi wa miundo mbinu ya maji ili iweze kuwa imara na kusaidia wananchi.
Mh. Kayanda ametembelea eneo lilojengwa tanki la maji Matala na kukuta kipande cha chuma cha kupitisha maji kutoka kwenye tanki kwenda kwenye kisima kimekatwa,lakini amejionea namna vioo vya jengo hilo vilivyopasuka na uzio wa pampu za kusukuma maji umeharibika na eneo liko katika hali ya uchafu. Ametoa maelekezo kwa uongozi wa Halmashauri ya kijiji kuhakikisha ndani ya siku mbili chanzo cha maji kiwe katika hali ya usafi na eneo hilo liwe linalindwa. Amesema tathimini ya uchunguzi wa uharibifu itakayofanyika juu ya miundo mbinu ya vyanzo vya maji Matala, itolewe na ikibainika mtu yeyote amehusika katika uharibifu wa miundo mbinu ya maji, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Matala Ndg. Majoda Kidosa amesema kumekuwa na matukio ya watu kupigwa na wengine kutishiwa usalama wa maisha yao. Wananchi wengi wanahofia kutoa taarifa za uhalifu kwa sababu wanaogopa vitisho wanavyopata kutoka kwa wahalifu hao. Ndg. Kidosa amesema watu wanaofanya uhalifu wengi wao wanaishi nao lakini kuna watu wachache wanaotoka maeneo ya jirani.
Amesema kuna wahalifu watatu ambao waliwakamata na kuwafungia katika ofisi ya kijiji lakini kwa uzembe uliofanya na Mlinzi wa zamu wa eneo hilo wahalifu walitoroka asubuhi ya saa mbili baada ya mlinzi kuacha lindo na kwenda kunywa chai. Amesema kutokuwa na vijana wenye nidhamu na mafunzo ya jeshi la akiba imekuwa changamoto kubwa katika kukabiliana na matendo ya uhalifu katika kijiji cha matala.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa