Na Tegemeo Kastus
Utaratibu wa usambazaji wa maji wa kanda utendelea kama kawaida badala ya wazo la viongozi wa kijiji cha malekchand kutaka utaratibu wa umwagiliaji ufanyike kwa kijiji. Maelekezo hayo yamemaliza mvutano uliokuwepo katika ukanda wa mfereji wa maji (scheme) unaosambaza katika vijiji viwili vya Laghangarer na Malekchand. Maamuzi hayo yanalenga kutoharibu maamuzi yaliyofikiwa awali kati ya jumuiya ya watumia maji bonde la kati singida , viongozi wa skimu kutoka vijiji vyote vinavyozunguka bonde la Eyasi, wataalamu na wadau wanaojihusisha na kilimo cha umwagiliaji tarafa ya Eyasi.
Mh. Kayanda akiwa katika eneo la mfereji wa maji Laghangarer
Hayo yamejiri katika mikutano ya hadhara ambayo Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya Laghangarer na Malekchand. Amesema utaratibu wa umwagiliaji wa kanda lazima ufuatwe, ameongeza kusema wataalamu wa maji kutoka bonde la kati Singida wamepima maji katika mifereji inayosambaza maji katika kijiji cha Laghangarer na Malekchand. Na kwa mujibu wa vipimo hivyo walibaini kasi ya maji katika mifereji inayosambaza maji Laghangarer ni Lita 432 kwa sekunde na kasi ya mifereji inayosambaza maji kwa kijiji cha Malekchand ni lita 414 kwa sekunde.
Mh. Kayanda ameelekeza Juwamaboe pamoja na wataalamu wa maji bonde la kati Singida, kufanya upembuzi yakinifu wa gharama za kuweka mlango katikati ya kiungo cha kusambazia maji kwenye mfereji wa vijiji vya Laghangarer na Malekchand. Amesema baada ya gharama kufahamika Juwamaboe waandike barua kwa viongozi wa vijiji kuwajulisha gharama za ujenzi huo ili maji yaweze kugawanya kwa usawa na kuondoa tofauti wa lita 18 za maji zinazolalamikiwa katika mgao wa maji kwa kanda baina ya vijiji hivyo.
Mh. kayanda akikagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa shule ya sekondari Eyasi
Mh. Kayanda amesema mabadiliko ya tabia ya nchi na kuongeza kwa shughuli za kibinadamu yanaendelea kusababisha maji kupungua. Amesema Halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa visima viwili vilivyochimbwa katika kijiji cha Malekchand. Amesema mwaka wa fedha 2022-2023 Halmashauri ya wilaya itatenga fedha kwa ajili ya kuchimba visima vya maji katika kijiji cha Laghangarer. Amesema kulingana na kasi ya ufunguaji wa mashamba ya kilimo inavyoendelea ni vyema sasa wakulima wakajiunga kwenye vikundi ili kuanza kuchimba visima vyao ili kukabiliana na upungufu wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Eyasi. Kama walivyo fanya wakulima wanaojihusisha na kilimo cha umwagiliaji wa vitunguu na mahindi katika eneo la Midabini na kitongoji cha Kambi ya simba.
Mh. Kayanda akizungumza na wananchi katika kijiji cha Laghangarer
Wakati huo huo Mh. Kayanda amewapongeza wananchi wa vijiji vya Laghangarer na Malekchand kwa jitihada za kuanza ujenzi wa sekondari ya Eyasi ili kupunguza adhaa ya wanafunzi kutembea umbali mrefu. Amehimiza wananchi kuendelea kujitoa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Eyasi. Amesema ili shule ya sekondari ya Eyasi iweze kuanza lazima ujenzi wa maabara, ujenzi wa ofisi ya walimu ujenzi wa madarasa ukamilike. kabla ya wakaguzi wa elimu wa kanda kukagua ili kutoa kibali kwa shule kuanza kupokea wanafunzi. Mh. Kayanda ameelekeza kamati ya ujenzi wa shule hiyo kusimamisha ujenzi wa nyumba ya mwalimu mpaka mwahandisi atakapowapatia ramani ya ujenzi ya serikali. Ameelekeza Mwandisi wa wilaya kufanya ushauri wa kitaalamu ikiwa ni pamoja na kufanya setting ya msingi kabla ujenzi wa nyumba hiyo kuanza. Katika hatua nyingine Mh. Kayanda amewaelekeza viongozi wa serikali za vijiji vya Laghangarer na Malekchand kuweka mipaka ya eneo la shule ya sekondari Eyasi ili eneo hilo lisije likavamiwa.
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda amehimiza viongozi wa Halmashauri ya kijiji kujua mipaka ya kazi zao za uongozi, amesema ni vyema Mwenyekiti akajua majukumu yake kama kiongozi wa kisiasa wa kijiji na Afisa mtendaji wa kijiji akajua majukumu yake kama Mtendaji wa shughuli zote zinazofanyika kwenye kijiji. Amesema wajumbe wa kijiji wanapaswa pia kujua wajibu wao katika kushauri serikali ya kijiji, na kusimamia shughuli za mendeleo katika vitongoji vyao. Amesema viongozi wakifanya kazi kwa ushirikiano hakutakuwa na mvutano au malumbano katika kusimamia miradi ya maendeleo. Amesema mivutano ya uongozi ndio inayosababisha wananchi kukosa ari ya kujitoa kwenye shughuli za maendeleo.
Mh. kayanda akizungumza na wananchi katika kijiji cha Malekchand
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa