NA TEGEMEO KASTUS
Maamuzi ya ujenzi wa zahanati katika kitongoji cha Endamarariek yamefikiwa, baada ya sintofahamu ya muda mrefu kwa wananchi na uongozi wa Halmashauri ya kijiji. Mvutano huo ulivihusu vitongoji viwili vya Ayarat na Endamarariek ambavyo vyote viko katika kata ya Endamarariek vilivyokuwa vinalumbana juu ya usahihi wa eneo la ujenzi wa zahanati ya afya.
Maamuzi hayo yamefanywa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas kayanda katika mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika kata ya Endamarariek. Mh. Kayanda ameahidi kutoa kiasi cha 500,000 kama sehemu ya mchango wake katika ujenzi wa zahanati hiyo. Ameueleza uongozi wa serikali ya kijiji kwamba atashikiriki kwenye ujenzi wa uchimbaji wa msingi wa zahanati hiyo.
Mh. Kayanda ametoa maelekezo kwa uongozi wa Halmashauri ya kijiji katika mkutano wa serikali ya kijiji unaotarajiwa kufanyika Jumamosi kuainisha eneo ambalo zahanati itajengwa katika kitongoji cha Endamarariek. Amesema pamoja na kuanisha eneo la ujenzi wakubaliane kiasi cha mchango wa fedha utakaochangiwa na wananchi kwa ajili ya ujenzi wa zahanati. Mh. Kayanda amesema baaada ya kikao cha uongozi wa serikali kijiji atatoa kibali kwa ajili ya mchango wa ujenzi wa zahanati.
Mh. Abbas kayanda akikagua uimara wa daraja kwenye ujenzi wa babaraba ya Endabash Mnadani kuelekekea Endamarariek.
Mh. Kayanda ameelekeza Afisa ushirika wa wilaya Ndg. Kastuli pamoja na Mrajisi Msaidizi wa Mkoa kutoa elimu ya namna ushirika unavyotakiwa kuendeshwa kwa mjibu wa sheria. Amemuelelekeza Mrajisi Msaidizi wa mkoa kuja kutambua ushirika wa Duma Amcos umekusanya kiasi gan cha fedha na hizo fedha ziko wapi ?? Amesema lazima chama cha ushirika kiendeshwe kwa uwazi, na kwa maslahi ya wanachama wa ushirika. Amesema lazima ushirika uwanufaishe wakulima na wafugaji na sio kunufaisha mtu binafsi. Sambamba na hilo Mkuu wa wilaya ametoa maelekezo kwa Afisa kilimo Endamarariek kutoa taarifa ya mapato na matumizi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia 2017-2019 juu ya mradi wa shamba darasa katika kijiji hicho na kueleza mapato na matumizi ya mwaka fedha mwaka 2020. Afisa kilimo anapaswa kutoa taarifa hiyo tarehe 8 mwezi huu katika mkutano wa Halmashauri ya kijiji.
Mh. Abbas Kayanda pamoja na wananchi wametembea umbali zaidi km 1 wakikagua ujenzi wa barabara ya Endamarariek Kuelekea shule ya Msingi Duma
Mh. Kayanda ametoa maelekezo kwa wakala wa barabara vijijini kuhakikisha wakandarasi wanaotengeneza barabara vijijini wajenge utamaduni wa kuripoti kwenye uongozi wa serikali ya kijiji kabla ya kuanza kazi. Amesema kujitambulisha kwenye uongozi kunasaidia kazi kufanyika kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuepuka vikwazo vya kuweka mifereji (matoleo) ya kusaidia kutoa maji kwenye barabara. Utekekezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi ni pamoja na utengenezaji na ukarabati wa miundo mbinu. Amesema shule ya sekondari Florian imepewa million 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu, serikali imetoa million 637,400,000 wilayani Karatu kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha miundo mbinu katika shule za sekondari na msingi. Mh. Kayanda ameomba wananchi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Awali katika ziara hiyo mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Kayanda alitembelea eneo ambalo ujenzi wa machinjio kata ya Endabash mnadani ulikuwa umesimama kutokana na mvutano uliokuwepo katika ujenzi wa mradi huo. Ujenzi wa machinjio unakadiriwa kugharimu kiasi cha million 5, Ujenzi ulikuwa umebakia upauzi pamoja na umaliziaji wa (slab) sakafu ya chini. Mh. Kayanda ametatua mvutano huo na ametoa maelekezo mpaka kufikia taraehe 20 mwezi wa nane mwaka huu ujenzi uwe umekamilika na ameahidi kwenda kuzindua mradi huo wa machinjio.
Mh. Abbas kayanda akiangalia ujenzi wa drift unaoendelea kwenye barabara Endabash Mnadani kuelekea Endamarariek
Mh. Kayanda ametembelea barabara ya mnadani mpaka Endamarariek inayosimamiwa na Tasaf na inayogharimu kiasi cha million 75. Ametoa maelekezo kwa Mratibu wa Tasaf wilaya kuhakikisha barabara ya mnadani Endamarariek inakamilika ujenzi wake ifikapo tarehe 20 mwezi wa nane mwaka huu ikiwa ni pamoja na umaliziaji wa ujenzi wa madaraja pamoja na drift za barabara hiyo.
Mh. Kayanda ametembelea na kukagua ujenzi wa barabara ya Endamarariek kuelekea shule ya msingi Duma ambayo nayo inagharimu kiasi cha million 75. Barabara hiyo kwa mujibu wa mkataba inatarajiwa kukamilika 30 mwezi wa nane mwaka huu. Ametoa maelekezo kwa Mratibu wa Tasafa na msimamizi wa ujenzi wa barabara hiyo kuhakikisha ndani ya muda huo vivuko vinajengwa na madaraja yanajengwa kwa kuzingatia thamani ya fedha katika mradi. Mh. Kayanda amesema hakuna muda utakaongezwa kwenye ujenzi wa mradi huo, amesema tarehe 1 mwezi wa tisa ataenda kuupokea ujenzi wa mradi huo.
Mh. Kayanda ametembelea shule ya msingi Endabash kujionea ukarabati wa madarasa matatu yanayoendelea kukarabatiwa katika shule hiyo na shirika la world vision na ujenzi wa vyumba vipya nane vya madarasa katika shule ya msingi Endabash ambavyo vitajengwa kwa muda wa miezi mitatu. Mh. Kayanda amesema ukarabati huo unaofanyika ukikamilika utasaidia kumarisha miundo mbinu ya madarasa katika shule hiyo kongwe ya Endabash. Amesema ni imani kwamba wanafunzi watakuwa wanasoma katika mazingira mazuri zaidi.
Mh. Abbas Kayanda kushoto akitoa Maelekezo kwenye ujenzi wa jengo la Machinjio Endabash.
Awali Ndg. Godluck Innko Programme Manager wa world vision amesema mbali na ukarabati wa madarasa kuna ujenzi wa matundu 18 ya vyoo, ujenzi wa sehemu tatu za kunawia mikono pamoja na jiko la kupikia chakula. Kituo cha kunawia mikono kitajengwa upande wa vyoo vya wasichana na kituo kingine kitajengwa upande wa vyoo vya wavulana na kingine kitajengwa katika eneo la jiko. Amesema kuna jengo la utawala la walimu pamoja na chumba kimoja maalumu kwa ajili ya mwalimu mkuu amesema mdarasa mapya yatakayojengwa katika shule hiyo yatawekwa madawati. Ndg. Innko amesema wanaangalia na shule ndogo ya msingi ya Salamay yenye mdarasa mawili na choo, amesema wataongeza madarasa mengine mawili katika shule hiyo na choo cha wasichana chenye matundu sita.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa