NA TEGEMEO KASTUS
Mvutano wa viongozi kati ya kijiji cha Gidibaso na kijiji cha Endamarariek uliosimamisha kwa muda Mradi wa maji unaojengwa na wadau wa maendeleo umetatuliwa kwa njia ya amani na Mkuu wa wilaya ya karatu amba po viongozi wa vijiji hivyo wameridhia na kuzika tofauti zao. Viongozi hao sasa wamehimizwa kuweka nguvu katika kusimamia shughuli za miradi ya maendeleo ambayo itasaidia kuboredha huduma za jamii na kuleta ustawi mzuri wa uchumi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh, Abbas Kayanda katika kikao cha ndani kilichohusisha wajumbe wa Halmashauri ya kijiji cha Gidibaso na wajumbe wa Halmashauri ya kijiji cha Endamarariek uliolenga kuja na mstakabali wa pamoja juu ya kutatua mgogoro ulijitokeza kati yao. Mh. Kayanda amesema kwa ujumla mgogoro umeisha na mradi wa maji unaendelea baada ya kikao cha mkuu wa wilaya ya Karatu. Ameongeza kusema sifa ya kiongozi hupimwa kutokana na maendeleo anayoyaleta kwa kushirikiana na wananchi. Amesema mpango wa ujenzi wa miundo mbinu ya maji unaotekelezwa na wadau wa maendeleo shirika la world vision unadhamiria kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kila mahali katika tarafa ya Endabash.
Mh. Kayanda akizungumza na wajumbe wa vijiji vilivyokuwa vikivutana.
Amesema wadau wa maendeleo shirika la world vision wanalenga kuhakikisha 90% ya tarafa ya Endabash inapata maji safi na salama. Akizungumzia kuhusu msuguwano wa viongozi katika kikao hicho Mh. Kayanda amesema wafadhili hawapendi kufanya kazi sehemu zenye migogoro. Kitendo cha kuzuia chanzo cha maji kutumika ni kinyume cha sheria ya maji no 5 ya mwaka 2019. Amesema serikali haifurahii vitendo vya ugomvi, vinavyofanywa na viongozi wa kijiji na amewataka viongozi maslahi binafsi katika kushughulikia maswala ya umma . Amesema vyema viongozi wakaongoza kwa hekima na busara na pale dosari inapojitokeza ni vizuri kukaa na kuitatua kwa pamoja.
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda amesimamisha utoaji wa hati za kimila katika vijiji vya Gidibaso na Endamarariek kwa sababu vijiji hivyo havina hati ya umiliki wa adhi ya kijiji. Amesema ni wakati sasa wa vijiji vya Gidibaso na Endamarariek wakajikita katika kuhakikisha vijiji vyao vinapata hati ya umiliki wa ardhi ya kijiji ili viweze kupata sifa ya kutoa haki miliki za kimila kwa wananchi wenye uhitaji. Amesema viongozi wanapaswa kuhimiza ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa ofisi na zahanati katika vijiji ambavyo havina miradi hiyo. Ujenzi wa zahanati katika ngazi ya kijiji ili kusogeza huduma za afya karibu na maeneo wanayoishi wananchi.
Matukio katika picha wakati wa kikao
Mh. Kayanda amehimiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa corona, amesema wananchi wanapaswa kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuendelea kuvaa barakoa, kunawa mikono na maji tiririka na kutumia vitakasa mikono. Amewajulisha wananchi juu ya upatikanaji wa chanjo, ambayo inapatikana katika kituo cha afya Endabash, Kituo cha afya Askofu Hhando na kituo cha afya Karatu. Ameomba wananchi kwa hiari yao kwenda kupata chanjo ambayo Mkuu wa wilaya ya Karatu aliizindua tarehe 3mwezi wa 8. Amesema kuna upotoshwaji mkubwa unafanywa na watu kwa njia ya mitandao juu ya chanjo ya corona ni vyema watu wakaacha upotoshaji huo unaojenga hofu kwa wananchi.
Wajumbe wakizungumza katika kikao
Awali mwenyekiti wa kijiji cha Gidibaso Ndg. Thomas Irafay akizungumzia tofauti iliyokuwepo katika mvutano na kijiji cha Endamarariek, amesema kulikuwa na kikao cha kujadili kuhusu swala la mradi wa maji unaojengwa na shirika la world vision. Amesema kijiji cha Endamarariek ambacho ni kijiji mama cha Gidibaso ndipo kisima cha maji kilipojengwa wakati huo wakiwa ni kijiji kimoja. Amesema mvutano ulianza kipindi ambacho kulikuwa na ombi la kufanya pump test kwa ajili ya kuanza kujenga na kusambaza maji kwa kijiji cha Gidibaso. Amesema hapo ndio mvutano ulipoanza kati ya uongozi wa kijiji cha Endamarariek na uongozi wa kijiji cha Gidbaso. Amesema licha ya vikao vya pamoja kukaa baina ya vijiji husika bado mvutano uliendelea kuwepo kwa sababu ya uelimishaji mdogo kwa wananchi juu ya namna mradi huo wa maji utakavyoweza kunufaisha kwa pamoja vijiji hivyo.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha Endamarariek Ndg. Thomas wilbroad Bayo amesema mvutano waliokuwa nao mkubwa na kijiji cha Gidbaso ni kukosekana kwa taratibu za vikao rasmi wa kuomba mradi ulio katika Halmashauri ya kijiji cha Endamarariek. Amesema maswala ya utekelezaji wa mradi huo yalikuwa yanazungumza nje ya vikao rasmi, hivyo kuleta hali ya wasiwasi juu namna ya mradi wa kisima kilichopo katika kijiji Endamarariek utakavyowanufaisha kwa pamoja kijiji cha Endamarariek na kijiji cha Gidibaso.
Matukio katika picha wakati wa kikao
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa