Na Tegemeo Kastus
Viongozi wa serikali za Halmashauri za vijiji waaswa kujenga uadilifu katika utendaji wa majukumu ya kazi. Lengo la kuundwa kwa serikali za mitaa ni kuwezesha viongozi kuwa karibu na umma na kusaidia kuunganisha wananchi na serikali kuu. Ukiwa kiongozi unakuwa mfano kwa watu wengine katika kufuata taratibu na sheria katika uendeshaji wa serikali ya kijiji. Moja ya sifa ya utawala bora ni pamoja na kulinda siri ya mambo yanayozungumzwa katika vikao vya ndani vya Ofisi.
Mh. Kayanda akiwa na wananchi wa kijiji cha Endala kwenye mkutano wa hadhara.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipofanya Mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Endala. Amesema swala la kusoma mapato na matumizi ya Halmashauri ya serikali ya kijiji si swala la hiari bali ni wajibu wa viongozi kutekeleza takwa hilo la kisheria katika kuendesha serikali ya kijiji. Amesema athari viongozi wa kijiji kuvutana katika uongozi zinachangia kwa kiasi kikubwa kudorora kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Matukio katika picha wakati wa kikao cha hadhara katika ofisi ya kijiji cha Endala
Mh. Kayanda amesema wananchi ndio waajiri wa viongozi, lazima hekima na busara itumike wakati wa kusikiliza kero zao. Kimbilio la wananchi ni viongozi wa serikali za kijiji, ameongeza kusema viongozi wanapozungumza na wananchi lazima watumie lugha za staha bila kuwa na kiburi cha madaraka. Amesema hakuna jambo viongozi wa serikali ya kijiji watafanya bila kushirikisha wananchi. Ametoa rai kwa wananchi vilevile kutumia lugha ya staha kwa viongozi wanapoawasilisha kero na malalamiko yao kwa viongozi ili kuepusha kutunishiana misuli. Amesema wananchi mtoe ushauri kwa viongozi katika kujenga misingi ya maendeleo ya Halmashauri ya kijiji. Katika mkutano huo viongozi wa Halmashauri ya kijiji cha Endala na wajumbe wake wamemaliza tofauti zao zilizokuwa zimejitokeza awali na kufungua ukurasa mpya. Katika hatua nyingine viongozi hao wamekubaliana kufanya kikao cha Halmashauri kuu ya kijiji cha Endala mwishoni mwa wiki ijayo kwa ajili ya kusoma taarifa ya mapato na Matumizi.
Mh. Kayanda akiwa katika eneo la ujenzi wa choo kwenye shule ya sekondari ya Marang
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda ametembelea na kujionea ujenzi wa choo cha wanafunzi katika shule ya sekondari Marang, mradi unaojengwa kwa nguvu za wananchi. Ujenzi wa choo hicho umegharimu takribani million 7 na upo katika hatua za umaliziaji. Mh. Kayanda amepongeza viongozi wa vijiji vya Ayalalio na Endonyawet kwa kusimamia ujenzi huo na ameelekeza viongozi wa vijiji husika kuhakikisha ifikapo tarehe 20/09/2021 ujenzi huo wa choo uwe umekamilika. Mh. Kayanda pamoja na kutembelea mradi huo ametembelea pia eneo linalotarajiwa kujengwa kituo cha afya Buger lilopo katika kijiji cha Ayalalio. Ujenzi huo umetengewa kiasi cha million 400 katika bajeti ya fedha ya mwaka huu.
Mh. Kayanda akiwa katika eneo la ujenzi wa miundo mbinu ya umeme wa Rea Kijiji cha Ayalalio
Wakati huo huo Mh. Kayanda ametembelea kujionea miradi ya Rea mzunguko wa 3 awamu ya 1 iliyokuwa imeachwa kiporo na mkandarasi NIPO aliyevunjiwa mkataba. Miradi hiyo kwa sasa inatekelezwa na kampuni Tanzu iliyo ndani ya Tanesco, amesema maeneo yote ambayo yamesimikwa nguzo za umeme, huduma hiyo ya umeme itaenda. Ameelekeza meneja wa Tanesco kuhakikisha kwamba kila genge linalohusika na kazi ya usambazaji wa umeme, linakuwepo eneo lake la mradi na kufanya kazi kikamilifu. Ameongeza kusema changamoto ya nguzo za umeme kuachwa chini ni hatari, ameelekeza meneja wa Tanesco wa wilaya kuhakikisha nguzo zote za umeme zinasimikwa.
Naye meneja wa Tanesco wa wilaya ya Karatu Mhandisi Henry Chahe amesema wamepokea maelekezo ya serikali na wataanza kuyafanyia kazi. Amesema umeme wa Rea utaenda kwenye vijiji makao makuu ya vijiji na kuhakikisha taasisi za umma zinapata huduma ya umeme. Amesema kwa sasa wamejikita katika kusimika nguzo ndogo na baadae watajikita katika kusimika nguzo kubwa. Mhandisi Chahe ametoa rai kwa wananchi kuepuka kufanya usanifu wa umeme kwenye nyumba kwa kutumia vishoka na badala yake watumie mafundi wanaotambulika na Tanesco. Ameomba wananchi kutumia contol number iliyowekwa na shirika la umeme ili kufanya malipo ya kupata huduma ya umeme lengo likiwa ni kukwepa vitendo vya ulaghai wa fedha vinavyofanywa na watu wenye nia ovu.
Mh.Kayanda akizungumza na viongozi wa serikali ya kijiji cha Endonyawet, katika ofisi za kijiji hicho cha Endonyawet.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa