Uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika tarehe 24 mwezi wa kumi na moja mwaka Elfu mbili na kumi na tisa, umeshuhudia Halmashauri ya wilaya ya Karatu ikipata wenyeviti wote wa vitongoji kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi. Wenyeviti hao walipita bila kupingwa na wengine wakishinda katika maeneo yaliyofanya uchaguzi.
Kitongoji ni eneo la kijiji lilogawanywa kufuatia maagizo ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya au Mji. Hivyo Halmashauri ya kijiji baada ya kupata idhini ya halmashauri ya mji au kijiji itaamua idadi ya vitongoji, kaya katika kila kitongoji na mipaka ya kila kitongoji. Vigezo ambavyo huzingatiwa katika kugawa eneo la kijiji katika vitongoji ni ukubwa wa eneo linalokusudiwa kuwa la kitongoji na idadi ya wakazi waliopo. Hii ni kwa mujibu wa KANUNI TARATIBU ZA SHERIA ZA UENDESHAJI WA KIJIJI NA KITONGOJI NA MTAA zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa mwezi wa kumi mwaka elfu mbili.
Uendeshaji wa Kitongoji, huongozwa na Mwenyekiti wa kitongoji wa eneo husika ambaye huchaguliwa na wakazi wa kitongoji wenye umri wa kuanzia miaka kumi na nane. Uchaguzi wa Mwenyekiti wa kitongoji hufanyika kwa kila baada ya miaka mitano kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi wa viongozi wa vitongoji. Kazi za Mwenyekiti wa kitongoji ni zile zile kama za Mwenyekiti wa kijiji katika ngazi ya kitongoji na hii ni kwa mujibu wa kanuni za taratibu za sheria za uendeshaji wa kijiji na kitongoji na mtaa zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za serikali za Mitaa October (2000)
kanuni za taratibu za sheria za uendeshaji wa kijiji na kitongoji na mtaa zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za serikali za Mitaa zinasema Mwenyekiti anaweza kuondolewa na Mkutano wa wakazi wa kitongoji. Mwenyekiti wa kitongoji anaweza akaondolewa atakapodhihirika kwamba ameshindwa kutekeleza kazi zake au anakiuka maadili ya kazi zake endapo wakazi wa kitongoji watatoa malalamiko.
Hivyo ni vyema wenyeviti wa vitongoji wakafuata matakwa ya kanuni za taratibu za sheria za uendeshaji wa vijiji ili kuepuka kuondolewa kwenye nyadhifa zao hasa ukizingatia serikali imemaliza kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi wa kumi na moja mwaka elfu mbili na kumi na tisa. Wenyeviti wa vitongoji ni viongozi muhimu sana kwa ustawi wa jamiii katika ngazi ya kitongoji. Wao ni viungo muhimu katika kutatua kero za wananchi mahali walipo na ni viongozi wanaowakilisha viongozi wengine wajuu katika nyadhifa tofauti.
Tunahitaji viongozi wa vitongoji kwa kushirikiana na viongozi wengine wa wahamasishe wananchi katika shughuli za maendeleo. Maendeleo yataletwa na sisi wenyewe wananchi tukiwapa ushirikiano wa kutosha viongozi wetu wa vitongoji. Si jambo zuri kwa kiongozi wa kitongoji kuondolewa katika nafasi yako inapodhihirika umeshindwa kutekeleza majukumu ya kiuongozi katika eneo lako. Wananchi waliowachagua katika maeneo wanashauku kuona utendaji mzuri wa shughuli zenu katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.
Wenyeviti wa vitongoji waliochaguliwa wanapaswa kufahamu, Mwenyekiti wa kitongoji anaweza kuondolewa itakaopdhihirika kwamba ameshindwa kutekekeleza kazi zake na anakiuka maadili ya kazi zake. Endapo wakazi wa kitongoji wakitoa malalamiko yaliyosainiwa na wakazi au watu wazima wenye umri wa miaka kumi na nane na kuendelea ambayo yatawasilishwa kwa Afisa mtendaji wa kijiji. Afisa Mtendaji lazima atajiridhisha kwamba tuhuma zilizotolewa zina ushahidi wa kutosha na zimetolewa maelekezo kamili na yenye kueleweka kwa tuhuma hizo.
Afisa mtendaji wa kijiji mara apatapo taarifa hiyo kabla ya kupita siku saba ataandaa mkutano wa dharura wa wakazi wa kitongoji na kupeleka taarifa ya mkutano kwa katibu Tarafa akitaka ahudhurie yeye mwenyewe au Mwakilishi wake. Kanuni za taratibu za sheria za uendeshaji wa kijiji na kitongoji na mtaa zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za serikali za Mitaa zinasema mkutano utaongozwa na Mweneyekiti Mwingine aliyechaguliwa na wanakitongoji kwa ajili ya kuongoza kikao hicho. Baada ya mkutano kuanza Afisa Mtendaji wa kijiji atasoma tuhuma naushahidi wote uliotolewa dhidi ya mwenyekiti wa kijiji.
Mwenyekiti wa kijiji atapewa nafasi ya kujitetea na kutoa maelekezo dhidi ya tuhuma hizo mbele ya mkutano huo. Baada ya kutafakari tuhuma na utetezi uliotolewa, wajumbe wa mkutano watapiga kura ya kuamua kumuondoa madarakani Mwenyekiti wao wa kitongoji au la. Mwenyekiti wa kitongoji ataondolewa madarakani endapo kura za kumkataa zitafika theluthi mbili ya kura zilizopigwa mkutanoni. Upigaji kura za kumuondoa madarakani Mwenyekiti wa kitongoji utakuwa wa siri.
Mwenyekiti aliyeondolewa madarakani ana hiari ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa wanavitongoji wa kumuondoa madarakani, kwa Mkuu wa wilaya ndani ya siku thelethini tangu uamuzi wa kumtoa madarakani ulipopitishwa. Baada ya kupita siku thelathini anazopewa za kukataa rufaa, Afisa Mtendaji wa kijiji ataiarifu Halmashauri ya kijiji kuhusu kuondolewa madarakani Mwenyekiti wa kitongoji ili utaratibu wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa kitongoji ufanyike. Haya yote yatafanyika kwa mujibu wa kanuni za taratibu za sheria za uendeshaji wa kijiji na kitongoji na mtaa zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za serikali za Mitaa October (2000)
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa