Na Tegemeo Kastus
Katibu Tawala wa wilaya ya Karatu Ndg. Abbas Kayanda amehimiza Maafisa waandikishaji na BVR KIT OPERATORS kuchukua tahadhari inayotolewa na wizara ya afya, wakati huu wa ugonjwa wa virusi vya corona kwenye zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura.
Ndg. Kayanda amesema ni vizuri tahadhari zote zikachukuliwa vizuri ili zoezi la uandikishaji lisiwe chanzo cha kueneza ugonjwa. Amesema hayo wakati akihitimisha semina ya siku moja ya maafisa wandikshaji na BVR operators katika ukumbi wa Afisa tarafa Karatu. Zoezi la maboresho ya daftari la wapiga kura linatarajiwa kuanza 17/4/2020 na kufanyika kwa muda wa siku tatu.
Ndg. Kayanda amesema zoezi linahitaji uvumilivu na umakini mkubwa katika ujazaji wa taarifa, ametoa wito asingependa kuona wilaya ya Karatu inakuwa na dosari yeyote katika zoezi la maboresho ya daftari la wapiga kura. Amesema waandikishaji na Bvr Operators wamepewa dhamana kufanya kazi kwa niaba ya watu wengine, isingekuwa rahisi wote sisi katika wilaya ya Karatu tushiriki katika zoezi kama hilo. Hivyo waandikishaji wamechaguliwa kwa sababu wanaaminika na wataitendea haki kazi walioyopewa.
Kwenye vikao vya tathimini juu ya kazi ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura, wilaya ya Karatu iwe kinara kwa kufanya vizuri katika zoezi hilo. Ameomba wataalamu kutoa maelekezo mazuri ya ufasaha kwa watendaji wa chini ili kazi iweze kwenda vizuri. Ndg, Kayanda ametoa wito kwa watendaji watakao kabidhiwa vifaa kuvitunza vizuri. Amesema zile mashine za BVR KIT ni mashine za gharama kubwa na madhumuni ni kufanya uchaguzi kwa njia za kisasa. Ameomba wandikishaji kutunza mashine kwa kuhifadhi vizuri lakini pia kuzitunza kwa kuzitumia vizuri. Ndg. Kayanda amewataka watendaji vijiji na kata kuhamasisha wananchi kujitokeza na kuboresha taarifa katika dafatari la wapiga kura.
Awali Ndg. Waziri Mourice Afisa Mwandikishaji wa wilaya ya Karatu, amesema kuna uwezekano watu wengi wakajitokeza katika uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa sababu vyuo na shule zimefungwa. Ameomba Maafisa waandikishaji kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kuweza kutimiza malengo.
Ndg. Waziri amesema mawakala wa vyama vya siasa ni watazamaji lakini siyo watoa maelekezo katika zoezi hilo. Amesema jambo lolote la dharura litakalojitokeza, waandikishaji watoe taarifa kwa watendaji wa kata ili waweze kutatua changamoto zitakazojitokeza katika zoezi.
Ndg. Waziri amesema katika zoezi hilo, wananchi watakuja vituoni na watataka kuelimishwa namna ya kuboresha taarifa zao katika daftari la wapiga kura. Ameombwa waandikishaji kutumia busara kuwaelekeza wananchi kwa upole ili zoezi liende vizuri. Amesema ndio maana tume ya taifa ya uchaguzi inafanya mafunzo mara kwa mara kwa wataalamu ili kukumbusha watendaji na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi kwa sababu binadamu tumeumbiwa kusahau.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa