Mkutano wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya Karatu umeendelea kwa siku ya pili, ambayo baraza limetumia kuchagua Mwenyekiti mpya wa Halmashauri. Nafasi ambayo ilibaki wazi baada ya aliyekuwa Mwenyekiti kuondolewa kwenye nafasi katika kikao maalum cha baraza la madiwani.
Kikao cha uchaguzi kiliongozwa na ndugu Abbas Kayanda kwa mujibu wa kanuni za Halmashauri namba 6 kifungu cha pili inayoelekeza utaratibu wa kufuata kuijaza nafasi ya mwenyekiti kwa muda, pindi baraza linapokuwa halina Mwenyekiti Halmashauri wala Makamu mwenyekiti. Ndugu Waziri Mourice katibu wa baraza alitangaza majina ya wagombea ambayo ni Mhe. Lazaro Bajuta kutoka kata ya Ganako na Mhe. Lazaro Geje Kutoka kata ya Mang’ola na wagombea wote walitoka chama cha mapinduzi ambacho ndio chama pekee kilichotoa majina ya wagombea wa nafasi hizo mbili.
Mwenyekiti wa muda wa kikao ndugu Abbas Kayanda alitangaza mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti mpya wa Halmashauri kuwa ni Mhe.Lazaro Geje. Mhe. Geje alipata ushindi wa kura 15 kati ya kura 3 zilizomkataa. Mwenyekiti ndugu Abbas alisema kwa mamlaka aliyopewa kwa ya kanuni ya 6 kifungu cha pili namtangaza Mhe. Geje kuwa Mwenyekiti mpya wa Halmashauri. Baraza hilo lilimchagua Mhe. Lazaro Bajuta kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo amewahusia viongozi wateule kuwa makini katika utendaji wa kazi zao ili wasiwaumize wananchi. Amesema kutenda kazi vizuri ni kutekeleza yale mliowaahidi wananchi, ambao wamewaamini na kuwateuwa. Mhe. Theresia amewaelekeza viongozi walioteuliwa kusimamia vizuri mapato ya ndani ya Halmashauri na kuepuka hoja za ukaguzi za mara kwa mara zinazokwamisha maendeleo ya wilaya.
Naye Katibu Tawala wa wilaya ndugu Abbas Kayanda amempongeza Mwenyekiti Mpya wa Halmashauri na Makamu mwenyekiti kwa kuteuliwa kushika nafasi hizo. Amesema wananchi wanataka mabadiliko, kutoka sehemu waliyopo na kwenda mbele zaidi kimaendeleo. Ndugu Abbas amewaahidi Mwenyekiti wa Halmashauri na Makamu mwenyekiti, kwamba watapata ushirikiano mzuri kutoka kwa watendaji wa Halmashauri.
Kikao hicho cha baraza la madiwani kilitumika kujaza nafasi za wenyeviti wa kamati za Halmashauri, baada ya wenyeviti wa awali kuhama vyama vyao na kuacha nafasi hizo wazi. Mhe, Yotham Manda ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya elimu maji na afya. Mhe. Josephat Margwe ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya uchumi.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa