Na Tegemeo Kastus
Maadhimisho ya siku ya wanawake wilaya ya Karatu yamefanyika kwa maandamano ya amani ya kinamama kutoka ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Karatu na kupokewa Uwanja wa Mazingira Bora na Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo.
Mhe. Theresia Mahongo amekabidhi hundi ya Tzs. Million 80 kwa vikundi vya wanawake, ili isaidie wanawake katika vikundi vyao vya uzalishaji. Fedha hizo zimetolewa na Halmashauri ya wilaya ya Karatu, ni fedha ambazo hazina riba wakati wa marejesho ili kuwakomboa kinamama katika shughuli zao za uzalishaji mali.
Mhe. Mahongo katika hotuba yake amepongeza Halmashauri kwa kutenga 4% ya mapato kwa vikundi vya wanawake, amesema Halmashauri inafanya vizuri sana katika kipengele hicho. Amesema ushiriki mdogo wa wanawake katika shughuli za uchumi unatokana na mitaji midogo lakini ukosefu wa ujuzi na uzoefu katika biashara pamoja na mila na desturi kandamizi ambazo zimekuwa kikwazo kikubwa. Ameomba wanawake kuendelea kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kukopesheka, ametoa rai kwa mabenki kupunguza riba kwenye mikopo wanayotoa kwa wanawake ili waweze kujenga uchumi wa familia na uchumi wa taifa. Amesema wanawake wanakopa fedha kidogo sana, kwa sababu hawana mitaji mikubwa.
Wanafunzi wakike wakiwa wamebeba bango lenye kauli mbiu ya siku ya wanawake katika maandamano kuelekea uwanja wa mazingira bora.
Ameomba vikundi vya wanawake kulipa mikopo kwa wakati amesema kumekuwa na kasumba kwa baadhi ya vikundi vya wanawake kutolipa fedha za mikopo kwa wakati. Amesema jambo hilo linarudisha nyuma sana utoaji wa mikopo kwa vikundi vingine vya wanawake. Amesema serikali tunatoa mikopo isiyo ya riba lakini wengine wanadanganyana kwamba fedha za serikali hazirudishwi, amesema serikali tumeshachukua hatua ya kuandikishiana mikataba kila baada ya mwaka mkopaji anarudisha. Halmashauri imejipanga kufanya ufutiliaji wa mara kwa mara kwa vikundi vya wanawake, mpaka sasa kuna Tzs. million 685 ziko tayari kwenye mzunguko.
Mhe. Theresia Mahongo amesema katika siku ya maadhimisho ya wanawake, mama ni mtu pekee sana katika malezi ya watoto na familia; mwanake ni mlezi , mwanamke ni daktari, mwanamke ni mchumi na mwanake ni kiongozi, mwanamke ni mshauri, mwanamke ni mfariji, na mwanamke ni hakimu.
Mhe. Mahongo ameomba wananchi kutumia fursa ya (WEI) Bantwana ambayo wametoa nafasi ya kuwasomesha wasichana 20 waliokatishwa masomo kutokana na ujauzito. Amesema wazazi ambao wasichana wao wamepata ujauzito katika umri mdogo na kukatisha ndoto zao za kuendelea na elimu kupeleka watoto wao (WEI) Bantwana ili waweze kuendelezwa kielimu, amesema kwamba kumekuwa na wazazi wenye mabinti waliopata ujauzito lakini bado wanawanyima vijana wao kujiunga na shirika hilo kupata elimu. Ametoa rai kwa wasichana waliopata mimba katika umri mdogo kujitokeza ili waweze kuitumia fursa.
Wanawake wakiwa wamebeba bango, katika maadhimisho ya siku ya mwanamke
Mhe.Mahongo amesema kauli mbiu ya “kizazi cha usawa kwa maendeleo Tanzania ya sasa na baadae” inasaidia kuenda katika maendeleo ya uchumi wa kati. maadhimisho ya siku ya wanawake yamekuwa na midahalo ili kutoa elimu kwa wanawake kwasababu hatupati muda wa kukutana mara kwa mara. Amesihi wanawake wenye uwezo kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo baadae mwezi wa kumi mwaka huu. Amewaasa wanawake kuwa na umoja, amesema amani tuliyonayo; wanawake wamechangia kwa kiasi kikubwa sana, ameomba kuwakataa wote watakaoleta vurugu kwenye uchaguzi, ameomba wanawake kujitokeza kusikiliza sera za wagombea ili kutambua mgombea sahihi.
Mhe. Mahongo ametumia hadhara hiyo kutoa tahadhari juu ya ugonjwa wa corona kwa wananchi wa Karatu, amesema ugonjwa huu ni hatari sana na unaambukizwa . Amesema ugonjwa wa corona bado haujafika Tanzania, ameomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kubwa kama wizara ya afya inavyoelekeza na tuombe mwenyezi mungu ugonjwa huu usitufikie.
Awali Mtendaji wa jinsi na jinsia kutoka Shirika la (WEI) Bantwana Bi, Grace Muro amesema kuna tofauti na jinsia na jinsi. Anasema jinsi ni kitu kinachotofautisha mwanamke na mwanaume kibailojia kutokana na uumbaji wa mungu. Amesema jnsia ni mtizamo wa jamii husika juu ya utendaji na utekelezaji wa shughuli za kijamii, amesema lakini mtizamo huo unaweza kubadilika.
Bi. Muro amesema kwa muda mrefu aliofanya kazi katika Halmashauri ya wilaya ya Karatu amegundua jamii ya Kiiraq inamuona mwanamke ni pambo. Amesema kwa mila desturi za kiiraq inamuona mwanamke hastahili kupewa elimu, kwa sababu akiolewa anaenda kunufaisha ukoo mwingine. Amesema Mhe. Mahongo ni mkuu wa wilaya ya Karatu lakini amefanya mambo mengi ya maendeleo katika wilaya ya Karatu. Bi. Muro amesema swala la kumnyima elimu mwanamke linafifisha maendeleo katika jamii ya kabila la wairaq. Bi, Muro amesema kuna tabia kwamba familia ikimuozesha mtoto wa kike inatupa kaa la moto nyuma kwa sababu eti si mleta maendeleo. Jambo hili linafifisha maendeleo ndio maana tunasema kauli mbiu ya siku ya wanawake ni “kizazi cha usawa kwa maendeleo Tanzania ya sasa na baadae” sio maendeleo ya familia siyo maendeleo ya ukoo ni Maendeleo ya Tanzania. Amesema hii ni mila ukuta, mila potofu inayoendelea kwa jamii ya wairaq ni lazima ivunjwe.
Naye binti aliyeathirika na mimba za utotoni alijitambulisha kwa jina moja Agnes anasema alikatisha masomo kutokana na mimba za utotoni alipokuwa sekondari. Ameomba wanaume kuacha kukatiza ndoto za watoto wa kike, Anasema anashukuru shirika la (WEI) Bantwana limemsaidia kujifunza kushona vikapu, kutengeneza maua, mafuta ya kujipaka kutengeneza make up, amesema shirika limemsaidia kuendeleza kipaji chake kabla ya kukatishwa masomo. Bi Agnes alikuwa anataka kuwa mwandishi wa habari kama angefanikiwa kuendelea na masomo yake. Baaada ya kupata ujauzito alitengwa na marafiki zake, ametoa wito kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao ili waweze kufutilia mienendo ya watoto wao vizuri.
Wakinamama walimu wakiimba kwaya katika maadhimisho ya siku ya wanawake
Wakinamama wakiwa katika picha ya pamoja katika uwanja wa mazingira bora.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa