Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh.Theresia Mahongo na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, wamefanya ziara kwenye shamba la Muwekezaji na kukagua Makazi ya wafanyakazi Kiran huko Oldean.
Ziara hiyo ililenga kukagua uimara wa nyumba za wananchi katika shamba la muwekezaji Sunial Aggarwal.Wakazi wanaoishi katka shamba hilo la Kiran wanaishi katika mazingira hatarishi baada ya nyumba zao kuwa na uchakavu wa muda mrefu. Mhe. Mahongo amesema eneo hilo lina wakazi wenye mkataba na Muwekezaji wa kufanya kazi na wakazi ambao hawana mkataba na Muwekezaji wa kufanya kazi. Mhe. Mahongo amemuelekeza Muwekezaji kuwapa makazi ya muda wananchi wote walio katika nyumba hizo 28 za muwekezaji.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo akiwa mbele ya nyumba ya mkazi wa kiran iliyokuwa katika hali ya uchakavu.
Amemuelekeza Muwekezaji kuwapa notisi ya kuhama kwa wakazi wasio na mkataba wa kufanya kazi baada ya zoezi la kuhamisha kwenye makazi ya muda salama. Ameongeza kusema kama kutakuwa na wakazi watakaoendelea kung’ang’ania kukaa kwenye makazi ya muajiri basi ni vyema Muwekezaji akaenda mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Mhe. Theresia Mahongo ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa shamba hilo la Kiran Kuhakikisha wananchi wanaoishi katika nyumba hizo kuwa wameshaondoka. Amesema mwezi watatu kutakuwa na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha na ni vyema muwekezaji wa shamba hilo akatafuta nyumba za kuhifadhi wananchi hao mapema ili nyumba hizo mbovu ziweze kubomolewa na kujengwa upya.
Mhe. Mahongo amewahakikishia wananchi hao kwamba watachukua orodha ya majina ya watoto wanaosoma na kuweka utaratibu ambao utasaidia watoto hao kuendelea na elimu katika maeneo watakayo hamia. Mhe. Mahongo amemuelekeza Afisa Tarafa wa Karatu kusimamia zoezi hilo la kuhamisha wakazi hao wa shamba la Kiran Estate Oldean.
Meneja Mkuu wa shambala Kiran Ndugu Davinder Singh amesema shamba hilo awali lilikuwa na kesi iliyokaa miaka 20 mahakamani na baada ya kesi kuisha mwaka 2011 shamba lilikuwa na hali mbaya. Amesema baada ya kesi walijikita katika kufanya ukarabati mkubwa wa shamba, na ilipofika wakati wa kuomba wananchi wasio na mkataba wa kazi na muwekezaji huyo walikataa kuondoka.
Ndugu Omari Hamza ambaye naye ni Meneja ameomba ushirikiano kwa wananchi hao ili zoezi la kuwaondoa liweze kuenda vizuri, amesema kuna kipindi walileta trekta kuhamisha wafanyakazi saba lakini walikosa ushirikiano.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo (kulia) akizungumza na mkazi wa Kiran katika ziara yake ya kukagua makazi katika eneo hilo.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa