Na Tegemeo Kastus
Usimamizi na utoaji wa huduma za afya katika kituo cha afya Kambi ya simba umezidi kuimarika, hasa katika upatikanaji wa dawa na huduma za kitabibu zinazotolewa katika kituo hicho. Wananchi waliokuwa wakipokea huduma katika kituo hicho wamesema malalamiko ya ukosekanaji wa dawa kwa sasa hakuna.
Hayo yamebainika katika ziara ya Mkuu wa wilaya Mh.Abbas Kayanda alipotembelea kata ya Mbulumbulu kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja upatikanaji wa dawa. Mh. Kayanda ameoneshwa kuridhishwa na utendaji mzuri wa watendaji wa afya katika kituo hicho na ameelekeza magari ya dharura (ambulance) yaliyowekwa katika vituo vya afya kwa ajili ya kusaidia wagonjwa yabaki katika vituo vya afya husika badala ya kufanya shughuli nyingine.
Dkt. Jackline Nlula (kushoto) akimuonesha Mkuu wa wilaya Mh. Abbas Kayanda (kulia) vifaa tiba vinavyopatikana kituo cha afya Kambi ya simba.
Mh. Kayanda amesema gari linatakiwa kuwa (stand by) wakati wowote kwa ajili ya kusaidia wagonjwa, amesema kituo cha afya Kambi ya simba ni muhimu sana kwa wananchi wa Mbulumbulu kwa sababu kinapunguza umbali mrefu wa kwenda Karatu mjini kupata huduma za afya. Amehimiza watendaji wa afya kuweka utaratibu mzuri wa kuagiza dawa kabla hazijaisha ili wananchi waendelee kupata huduma. Sambamba na hilo Mh. Kayanda amehimiza wananchi kulipia bima za afya ili kujengea uwezo wa upatikanaji wa dawa katika zahanati na vituo vya afya. Serikali inatoa huduma za afya kwa watoto wa chini ya miaka mitano bure kinamama wajawazito na wazee wasiojiweza bure ni sera ambayo serikali inaitekeleza katika kusaidia wananchi wake. Lazima wananchi tuoneshe uzalendo kwa kuisaidia serikali katika kuboresha miundo mbinu ya utoaji wa huduma za afya kwa kuchangia katika Ichf iliyoboreshwa inayowezesha watu 6 katika familia kulipia 30000 kwa mwaka.
Picha katika matukio mbalimbali wakati Mh. Abbas Kayanda akifanya ukaguzi kituo cha afya Kambi ya Simba
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda amesikiliza kero katika ofisi ya kijiji cha Kambi ya simba ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika ngazi ya kata. Amewaelekeza watendaji kuhakikisha mashauri ya migogoro ya ardhi wanayaelekeza katika vyombo vilivyokasimiwa madaraka hayo, ili shauri likimalizika kusikilizwa katika vyombo liwe limeisha kwa mujibu wa sheria. Amesema kufanya hivyo kunasaidia watendaji wa serikali kusimamia maamuzi yaliyofanywa kulingana na hukumu ilivyoandikwa kisheria.
Mh. Kayanda amesema kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kero za mashauri ya ardhi, amesema ni makosa kwa mtendaji kujadili hukumu iliyotolewa na mahakama au baraza la ardhi. Watendaji wanapaswa kushughulikia mashauri ya maswala ya ardhi kwa kuzingatia miongozo ya sheria badala ya kutumia utashi binafsi.
Naye Afisa Ardhi Mteule ndg. Faraji Rushagama amesema waziri wa ardhi ametoa fomu maalumu kwa ajili ya wananchi kuzijaza katika ngazi ya kata ili Mashauri ya ardhi yawe katika mpango taarifa (database) ili kujua mwenendo wa mashauri yote ya ardhi. Watendaji wa ardhi wapate nafasi ya kuyafanyia kazi mashauri yaliyondani ya uwezo wao au kuyapeleka katika vyombo vya maamuzi ili yapate nafasi ya kuanza kuchambuliwa na kutolewa maamuzi ya kisheria.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa