Kikao maalum cha baraza la Madiwani kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri. Kikao hicho maalum kilikuwa na ajenda moja, ambayo ilikuwa inamhusu mwenyekiti wa Halmashauri. Kilihudhuriwa na mwakilishi wa Mkuu wa mkoa ambaye alikuwa ni Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo.
Mwanasheria wa Halmashauri ndugu Prosper Ndomba alitoa ufafanuzi wa kanuni za Halmashauri kwa wajumbe, katika kikao hicho kilichojadili hoja ya kumuondoa Mwenyekiti wa Halmashauri. Amesema kanuni za Halmashauri namba 10 kanuni ndogo ya kwanza c za mwaka 2017, inazungumzia utaratibu wa kufuata. Amesema kanuni inaeleza kama Mwenyekiti wa Halmashauri na Makamu mwenyekiti hawapo au Mwenyekiti wa Halmashauri na Makamu mwenyekiti hawawezi kuongoza mkutano, mjumbe yeyote atachaguliwa kuongoza kikao Maalum cha baraza la madiwani.
Mwanasheria Ndugu Prosper amesema Mwenyekiti wa Halmashauri hawezi kuongoza kikao kinachojadli hoja ya kumuondoa kwenye wadhifa wake wa uongozi. Amesema Mwenyekiti atakuwa na haki ya kujitetea katika Kikao cha Baraza Maalum. Makamu mwenyekiti wa Halmashauri aliyepaswa kuendesha kikao naye alijiuzulu wadhifa wake. Hivyo kulazimu baraza maalum la madiwani kuchagua mjumbe ambaye ataongoza kikao cha baraza la madiwani kwa muda.
Mwanasheria amesema kanuni za Halmashauri namba 4; kanuni ndogo ya 3, kanuni ya kudumu za Halmashauri ndio zinaleza utaratibu wa kupokea hoja za kumuondoa Mwenyekiti, ambazo anazipokea Mkurugenzi kutoka kwa wajumbe. Mwanasheria amesema Mkurugenzi akipokea tuhuma anamuandikia Mwenyekiti Mtuhumiwa ambaye anapaswa kuzijibu ndani ya siku tano. Amesema Mkurugenzi akishapata utetezi wamajibu anamuandikia Mkuu wa Mkoa. Mkuu wa Mkoa anaunda tume ya uchunguzi ambayo inamrudishia Mkuu wa Mkoa majibu ya uchunguzi. Amesema Mkuu wa Mkoa anamrudishia Mkurugenzi, na anaitisha kikao maalumu ili asome matokeo ya uchunguzi. Kanuni za Halmashauri namba 82 Inaeleza utaratibu za kumuondoa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa mujibu wa gazeti la serikali namba 263.
Katika kikao hicho maalum cha baraza la madiwani cha kumuondoa Mwenyekiti hoja zilizotolewa mbele ya kikao dhidi ya Mwenyekiti; ni kufanya biashara na Halmashauri kinyume na maadili na hoja matumizi mabaya ya ofisi. Tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa katika uchunguzi ilibaini hoja ya kwanza ya mradi wa Karatu stationary office supply, mradi unaoendeshwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ulitoa huduma za vitu vya stationary kwa Halmashauri na vienye thamani ya takribani million 18 kwa ajili ya mahitaji ya Halmashauri. Tume ilithibitisha hoja hiyo katika uchunguzi wake baaada ya madiwani 7 kati ya 9 walioulizwa kukubali. Tume ilibaini mgongano wa kimaslahi katika taarifa yake juu ya hoja hiyo iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa mwenyekiti wa Halmashauri.
Hoja ya pili ambayo tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa ilibaini Kampuni ya Mnyenye general supply ambayo ilihusika na uuzaji wa matairi kwa magari ya Halmashauri. Tume ilibaini aliyekuwa Mwenyekiti alitumia madaraka yake vibaya, baada kampuni yake kujihusisha na biashara dhidi ya Halmashauri. Tume ilibaini ukodishwaji wa matairi ambao ulihusisha Kampuni ya Mnyenye general supply dhidi ya Halmashauri. Tume ilibaini katika uchunguzi wake hoja ya kujenga kituo cha mafuta kambi ya simba katika eneo la kijiji. Tume imebaini katika taarifa yake kwamba ujenzi huo haukufuata utaratibu na nikinyume na kanuni za mamlaka ya serikali za mitaa.
Tume katika uchunguzi wake ilishindwa kudhibitisha hoja dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti ya kuendesha vikao vya madiwani kwa misingi ya kiitikadi ya vyama. Tume katika uchunguzi wake ilishindwa kudhibitisha hoja ya aliyekuwa Mwenyekiti kutumia ushawishi wake kumpatia tenda rafiki yake Anatory construction limited aliyepata tenda ya kujenga kituo cha afya Kambi ya Simba na ujenzi wa soko la Karatu.
Tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa ilishindwa kubaini hoja ya aliyekuwa mwenyekiti wa Halimashauri kuhujumu mradi wa ujenzi wa pharmacy. Tume katika uchunguzi wake imeshindwa kuthibitisha hoja kwamba aliyekuwa Mwenyekiti alichimba kisima cha maji eneo la Midabini bila kuhusisha kamati ya maji bonde la kati. Tume katika taarifa yake imeona jambo hilo ni mradi binafsi na hauhusiani na uendeshaji wa Halimashauri.
Tume ya uchunguzi baada ya kupitia vielelezo na kusikiliza pande zote ilipendekeza Mwenyekiti wa Halmashauri kubeba jukumu la kuwajibika dhidi ya hoja zinazomkabili.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Mhe. Jublate Mnyenye amesema katika utetezi wake hoja ya Karatu stationary ilianza tangu 2004. Amesema kweli kampuni hiyo ni miongoni mwa kampuni zilizokuwa zinadai Halmashauri. Mhe. Jublate amesema hakuwa na ushawishi wowote juu ya hoja za Kampuni ya Mnyenye General supply kuuzia matairi Halmashauri. Amesema Halimashauri ilienda kununua matairi katika kampuni hiyo kama watu wengine binafsi wanavyoenda kununua.
Mhe. Jublate amesema hoja ya yeye kukodisha Mahema Alishatoa taarifa kwa mamlaka husika PCCB. Amesema kama kweli alikodisha Mahema kwa kiasi cha Million mbili iweje kwenye akaunti yake iwekwe laki nane bila ridhaa yake. Mhe. Mnyenye amesema ameshinikizwa kujiuzulu ingawa hajajihusisha kibiashara kwa namna yeyote na Halmashauri.
Kikao hicho Maalum cha baraza kilifanya maamuzi yake kwa kupiga kura za siri, na kura hizo ziliwahusisha wajumbe 20 jumla. Jumla ya kura 15 zilitaka Mwenyekiti aondolewe kwenye wadhifa wake na kura 4 zilitaka abaki na moja iliharibika. Maamuzi ya kikao Maalum cha baraza la madiwani baada ya kura kupigwa yalimvua wadhifa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu Mhe.Jublate Mnyenye baada ya theluthi mbili ya wajumbe kupiga kura ya kutokuwa na imani. Mwenyekiti anamuda wa siku 30 kupinga uamuzi wa kikao hicho maalumu cha baraza la madiwani kwa waziri mwenye dhamana.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa