Na Tegemeo Kastus
Mtendaji yeyote wa serikali haruhusiwi kutumia fedha za makusanyo yeyote alizokusanya bila kupeleka fedha hizo bank kwenye akaunti ya serikali. Hiyo inasaidia watendaji wa serikali kuepuka matumizi mabaya ya fedha za serikali kwenye shughuli za miradi ya maendeleo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipofanya ziara katika shule ya msingi Gidbaso kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu vinavyojengwa na serikali ya kijiji na wananchi katika kata ya Endamarariek. Amesema lazima watendaji wafuate sheria na taratibu za kutumia fedha baada ya kuziweka fedha hizo kwenye akaunti maalumu ya kuhifadhi fedha. Kutumia fedha bila kuzipeleka benki ni makosa kwa sababu si utaratibu wa matumizi ya fedha za serikali.
Mh. Abbas Kayanda akizungumza na kamati ya ujenzi na wananchi katika shule ya Msingi Gidbaso
Mh. Kayanda amesema kitendo cha mtendaji wa kijiji cha Gidbaso kutumia fedha kwa ajili ujenzi wa madarasa bila kuzipeleka benki kunasababisha kukosekane kwa uwazi wa mapato na matumizi. Ameagiza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa mapato na matumizi ya fedha zilizokusanywa na kijiji kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda amewapongeza wananchi wa kijiji cha Gidbaso kwa mwamuko wa kuchangia miradi ya maendeleo katika kijiji chao. Amehimiza wananchi kuendelea kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuweza kufikia kiwango cha million 9 walizojiwekea, ambazo mpaka sasa wameshachangia kiasi cha million 5.5 na ujenzi wa madarasa upo katika hatua ya ujenzi wa msingi. Amesema hakuna fedha itakayochangwa na wananchi ambayo itapotea, maendeleo ya wananchi wa Gidibaso yataletwa na wana-Gidibaso wenyewe.
Sambamba na hilo Mh. Kayanda amemuelekeza Afisa Mtendaji kata wa kata ya Endamarariek kufuatilia mapato na matumizi ya fedha zilizochangwa na wazazi kwa ajili ya walimu wa muda waliokuwa wanafundisha shuleni hapo ili kujiridhisha kama kweli walimu hao walilipwa au hawakulipwa. Amesema katika taarifa hiyo iainishe walimu hawakulipwa mwezi gani na fedha zilizokusanywa ni kiasi gani ?
Awali Ndg. Izrael Tluway mkazi wa Gidbaso ameeleza kufurahishwa na ziara iliyofanywa na mkuu wa wilaya amesema ziara hiyo imewapa ari ya kuongeza kasi ya ujenzi wa madarasa. Ndg Tluway amemuomba mkuu wa wilaya kufuatilia madai ya malipo ya walimu wa muda kwa sababu ya kukosekana kwa uwazi wa taarifa za walimu hao wa muda katika shule ya msingi Gidbaso hivyo kushindwa kulipwa kwa wakati stahiki zao. Amesema walimu hao wamekuwa wakilalamika kutolipwa fedha zao kwa wakati na hivyo kushindwa kuendelea kufundisha.
Mh. Abbas Kayanda akizungumza na wananchi
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa