NA TEGEMEO KASTUS
Uongozi wa kijiji cha chemchem wahimizwa kuanza kutenga maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo . Kutengwa maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo kutasaidia ufugaji wenye tija na unaolenga kupata mifugo yenye afya bora.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati akizindua maonesho ya tatu ya uogeshaji wa mifugo yenye kauli mbiu ‘kuogesha kwa afya na ufugaji wenye tija”. Uzinduzi huo umefanyika kiwilaya katika kijiji cha Chemchem kata ya Rhotia. Amesema lazima wafugaji waanze kutenga maeneo kwa ajili ya malisho ili kusaidia mifugo kupata chakula wakati wote. Nasikutenga tu bali kufuata maelekezo ya kitaalamu kujua ni aina gani za nyasi zina
zofaa kupandwa kwa ajili ya kulisha mifugo katika maeneo ambayo yatakuwa yametengwa ili kuwa na ufugaji wenye tija.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda akiwa katika zoezi ka uogeshaji wa mifugo kijiji cha Chemchem
Mh. Kayanda ametoa wito kwa wafugaji kuacha ufugaji huria na badala yake kufanya ufugaji wa kisasa. Wafugaji tunapaswa kuongeza ubora wa bidhaa zetu ili tuweze kupata soko zuri na kuinua hali ya maisha yetu. Amesema serikali kwa kulitambua hilo ndio maana imeanzisha uogeshaji wa mifugo. Kuogesha mifugo inasaidia kukinga mifugo na maradhi lakini pia inasaidia mfugo kuwa na afya bora. Serikali imeenda mbali ndio maana imetaka kuwe na kamati za usimamizi wa majosho.
Mh. Kayanda amesema kuogesha mifugo haimaanishi kuogesha ng’ombe peke yake tunatakiwa tuogeshe ng’ombe mbuzi kondoo na hata punda. Amesema ukiogesha baadhi ya mifugo na kuacha mifugo mingine tatizo la magonjwa litaendelea kuwepo. Mifugo ambayo haijaogeshwa ni rahisi kuaambukiza mifugo iliyoogeshwa. Wafugaji lazima wazingatie usafi wa zizi la ngombe, zizi linatakiwa kufanyiwa usafi na kupigwa dawa ili kuuwa mazalia ya kupe, amesema kama mifugo itaoshwa na kurudishwa kwenye zizi ambalo halikufanyiwa usafi na kupigwa dawa bado tatizo linakuwa halijatatuliwa.
Mh. Kayanda ameelekeza Maafisa Mifugo kukaa karibu na wafugaji na kuwapa elimu juu ya ufugaji wa kisasa. Lakini pia kutoa elimu ya namna wafugaji wanaweza kutenga sehemu ya maeneo yao ya kilimo kwa ajili ya malisho. Amesema Elimu ya ufugaji wa kisasa itawasaidia wafugaji kunufaika na mifugo yao na kuboresha hali ya maisha kuanzia kipato cha mtu mmoja mmoja na familia kwa ujumla.
Mh Kayanda amewaambia wafugaji wa kijiji cha Chemchem ikifika wakati wa kuchangia fedha kwa ajili kununua dawa za majosho wawe tayari kuchangia. Kila mfugaji atakayechangia ahakikishe anapewa risiti. Amesema risiti itaondoa changamoto za ubadhilifu wa fedha kwenye uendeshaji wa Majosho.
Awali Afisa mifugo wa wilaya ya Karatu ndg. Denis Buberwa amesema kuna lita 162 zilizogawiwa na serikali kwa ajili ya zoezi la kuogesha wa mifugo wilayani Karatu. Amesema Madawa ya kuogesha mifugo yanakuja kwa mwaka mara mbili. Wilaya ya karatu mpaka sasa ina jumla ya majosho 15.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa