Katibu Muenezi wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, na Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Arusha Ndugu Humphrey Polepole leo amewapokea madiwani watatu waliojiuzulu unachama katika Chama Cha Demokrasia Maendeleo wilayani Karatu.
Hafla ya kuwapokea na kuwaapisha ilifanyika ndani ya ofisi za ccm wilayani Karatu, madiwani waliojiuzulu ni Lazaro Bajuta kutoka kata ya Ganako, Benedicto Modaha kutoka kata ya Daa na Amani Hotay kutoka kata ya Mbulumbulu pamoja na Ndugu John Zakaria.
Ndugu Polepole amewapongeza madiwani hao kwa kuwapa Chama cha Mapinduzi heshima kubwa. Sambamba na kuwapokea wanachama hao wapya Ndugu Polepole ametoa maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi kwa serikali, amesema Karatu kumekuwa na mamlaka mbili za maji KAVIWASU na KARUWASA. KAVIWASU inatoza unit moja ya maji ni Tsh.3000 na KARUWASA inatoza Unit moja Tsh.1750. Si haki kwa watu kutozwa bei tofauti kwa maji yale yale, amesema baada ya mchakato unaoendelea sasa mamlaka zote za maji zitakuwa chini ya serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania. Ndugu Polepole ameelekeza uchaguzi wa KAVIWASU uliokuwa ufanyike tarehe 19 mwezi huu usimame na wasubiri maelekezo ya wizara ya maji. Serikali inapokea maelekezo ya chama cha mapinduzi na hayo aliyoyaelekeza ni maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi.
Ndugu Lazaro Bajuta aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu: amesema kuhama kwao chama ni utashi wao binafsi, amesema ameona mlima aliokuwa akiupanda ambao haupandiki. Amesema juhudi ya serikali ya chama cha mapinduzi katika utekelezaji wa mambo mbalimbali mazuri zimekuwa wazi kwa wananchi lakini baadhi ya watu wamekuwa wakibeza. Amesema amerudi nyumbani na hahitaji ushirika kwenye maamuzi yake binafsi, ametoka kwao kwa sababu hakuwa wakwao. Amesema kituo cha afya Mbulumbulu serikali imetoa milioni 500, kituo cha afya Endabash serikali imetoa milioni 400. Hiyo ni baadhi ya miradi ambayo imegharamiwa na kutekelezwa na serikali ya awamu ya tano kwa kipindi cha miaka mitatu chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Ndugu Benedicto Modaha ambaye alikuwa diwani wa Daa, amesema baada ya uchaguzi mkuu Arusha ilikuwa na mbunge mmoja wa CCM aliyekuwa akitoka wilaya ya Ngorongoro. Leo kuna wabunge wawili tuu wa upinzani mkoa wa Arusha. Baada ya uchaguzi mkuu wilaya ya Karatu ilikuwa madiwani wa Chadema kumi na wanne Ccm, lakini hivi sasa Chadema imebaki na madiwani wanne katika Halmashauri ya Karatu
Ndugu Polepole kushoto akiongoza wanachama wapya wa Chama cha mapinduzi mkono wa kulia kula kiapo cha utii, cha kukitumikia Chama cha Mapinduzi.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa