Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu ndugu Waziri Mourice, amefanya mkutano na wafanyabiashara wa soko kuu la Karatu. Mkutano huo wa kawaida ulilenga kutoa taarifa za ujenzi wa soko pamoja na kuzungumza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara ambao wamehama kupisha ujenzi wa soko unaoendelea.
Ndugu Waziri Mourice amewaahidi wafanyabiashara hao kufuatilia kwa karibu ujenzi wa soko hilo. Katika makubaliano ya awali soko lilitakiwa kumalizika kupauliwa tarehe 8 mwezi wa 7 mwaka huu. Mkurugenzi amesema mpaka kufika muda huo upauzi utakuwa bado haujamalizika lakini ameahidi kusimamia kidete swala la upauzi wa soko. Mwaka mpya wa fedha unaoanza Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi million 100 katika ujenzi wa soko. Ndugu Waziri amesema haridhishwi wafanyabishara hao kukaa nje ya soko kwa sababu hata halmashauri inakosa mapato kutokana na ujenzi kutokamilika.
Ndugu Waziri Mourice ametumia nafasi hiyo kuwaomba wafanyabiashara ambao hawajachukua vitambulisho vya ujasiriamali kuchukua bila shuruti. Amesema hakuna mtu anayepaswa kutoa ushuru wa shilingi 300 tena na badala yake wachukue vitambulisho vya ujasiriamali. Ndugu Waziri Mourice ameahidi kuwalipa walinzi madai yao ya mshahara wa miezi mitatu. Walinzi hao mkataba wao wa kufanya kazi unaisha mwaka huu wa fedha, amesema walinzi hao wawili watalipwa madai yao na Halmashauri pamoja na mlinzi mwingine wa buchani ambaye naye anadai malimbikizo ya miezi saba ya mshahara. Katika kikao hicho wananchi walikubaliana kutafuta namna ya kutafuta walinzi wa kulinda vibanda vyao na kuwalipa kupitia viongozi wao.
Wafanyabishara wenyewe watapanga kiasi cha kuwalipa walinzi hao bila kuhusisha Halmashauri. Ndugu Waziri Mourice amewatoa hofu wafanyabishara amesema pindi soko litakapokamilika watarudi kwenye soko hilo kwa sabababu Halmashauri ina majina ya wafanyabishara waliokuwepo awali. Lakini pia hata viongozi wa wafanyabiashara wa soko hilo wanayo orodha ya majina ya wafanyabishara wenye uhalali wa kurudi kupata sehemu za biashara katika soko hilo. Ndugu waziri Mourice amesema katika ujenzi wa meza hizo za ndani watachukua maoni kutoka kwa wafanyabiashara ili sehemu za biashara zikae kwa namna iliyobora.
Awali katika mkutano huo wafanyabiashara kutoka soko la chini walimuelezea Mkurugenzi adhaa ya maji wanayopata. Bi, Flora Mgaza amesema soko la chini liko katika mkondo wa maji hivyo mvua zinaponyesha, eneo linakuwa siyo rafiki kwao na kwa wateja kufanya biashara. Ameomba soko likamilike kabla ya masika nyingine haijafika ili waweze kuepuka adha wanayopata wakati wa masika. Pia amesema soko la chini lina magofu ambayo watu hawafanyi biashara jambo linaloleta ugumu hasa wakati ulinzi muda wa usiku. Mfanyabiashara huyo amesema zipo fununu watu kutaka kutumia mwanya wa magofu ya vibanda hivyo kuja kupata nafasi ya vibanda vyao pindi soko jipya litakapokamilika.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa