NA TEGEMEO KASTUS
Wataalamu wa afya watakiwa kufanya ufuatiliaji wakina wa vifo vyote vinavyohusiana na uzazi pamoja na watoto wachanga katika vituo vya kutolea huduma za afya na vile vinavyotokea kwenye jamii. Ili kupata takwimu sahihi za changamoto hizo zitakazosaidia kujua ukubwa wa tatizo. kinachoongoza serikali kuja na mipango ni takwimu ambazo zinasaidia kujua hali ikoje na tunaelekea wapi katika kutatua.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati akizindua kikao cha kujadili vifo vitakanavyo na uzazi na watoto wadogo, kilichohusisha wataalamu wa afya na wadau wa afya katika wilaya zote za mkoa wa Arusha katika ukumbi wa Karatu sekondari. Mh. Kayanda amesema katika kuhamasisha tuwashirikishe viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na viongozi wa kimila ili kukabiliana na kutokomeza tatizo la vifo vya uzazi na watoto wadogo. Amesema jitihada za kukabiliana na kutokomeza changamoto ya vifo vya uzazi na watoto wadogo si swala la wataalamu wa afya pekee.
Mh. Abbas Kayanda akiwa katika ufunguzi wa kikao kazi cha watendaji wa afya.
Mh. Kayanda amesema wataalamu wa afya lazima wawe na mahusiano mazuri na viongozi wanaowazunguka katika maeneo ya kiutendaji. Mahusiano mazuri yatasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi. Mganga wa kituo anapaswa kuwa na ushirikiano mkubwa na uongozi wa serikali ya kijiji ili kushirikiana katika kutatua changamoto za kiutendaji wanazokabiliana nazo katika utendaji wa kazi.
Akizungumzia kuhusu mazingira ya utoaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya, amesema lazima watendaji wa afya wawe na lugha zenye staha kwa wagonjwa. Amesema lugha nzuri ndizo zinamfanya mgonjwa kupata faraja wakati wa kupata huduma za afya. Amesema lazima sekta ya afya izidi kuwaangalia kwa ukaribu watumishi walio maeneo ya pembezoni kwa kuwapa motisha ya kazi.
Mh. Abbas Kayanda katika matukio tofauti wakati wa ufunguzi
Mh. Kayanda amesisitiza sekta ya afya kusimamia mfumo wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya. Amesema kuna baadhi ya vituo vya afya havina mfumo wa mapato jambo ambalo linasababisha serikali kukosa mapato. Ameongea kusema lazima kusimamia mfumo wa upatikanajia wa madawa pamoja na vifaa na vifaa tiba viwe vinapatikana muda wote katika vituo vya afya.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa damu salama amesema kila Halmashauri inapaswa kufanya uhamasishaji wa kuchangia kupata damu salama. Ameweka msisitizo wa kuendelea kuisimamia kampeni ya, “nisaidie niweze kuishi mimi na mama yangu” ameelekeza Halmashauri ambazo hazijazindua kampeni hiyo kwenda kuzindua. Lakini pia Mh. Kayanda ameelekeza kuendelea kuhudumisha huduma ya kliniki mkoba ili kuendelea kusaidia wale wananchi ambao hawapo kwenye maeneo yenye vituo vya afya ili waweze kunufaika na kliniki mkoba.
Ameongeza kusema sekta ya afya inahitaji kuendelea kuweka mkazo na kuhimiza wakinama wajawazito waanze kwenda kiliniki na wajifungulie kiliniki ili mama na mtoto waweze kuwa salama.Amesema mahudhurio ya kinamama kliniki ni madogo, lazima tutumie timu zetu za uhamasishaji ili kuwahamasisha kinamama kujifungulia katika vituo vya afya.
Amehimiza watendaji wa afya walioshiriki kutumia maarifa waliopata kwenye kikao wasaidie kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma. Amesema mambo mnayoyapata kwenye kikao mjitahidi kushirikisha watendaji wenzenu katika sekta ya afya katika kusambaza maarifa mapya mliopata kwenye kikao kazi. Utamaduni wa kusambaza maarifa ya ujuzi kwa watendaji wenu wa chini ni muhimu katika kuleta mabadiliko chanya ya kiutendaji.
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda ameonesha kutoridhishwa na tabia za boharai ya dawa MSD yakusambaza dawa katika vituo vya afya bila kushirikisha wajumbe wa kamati ya afya ya kituo cha afya. Amesema wajumbe wa kamati ya afya ni watu muhimu kuthibitisha dawa zinazoletwa kwenye kituo. Amesema kumekuwa na changamoto za vituo vya afya kuletewa dawa ambazo hazijaagizwa na kituo. Hivyo kupunguza ufanisi wa utendaji kazi katika vituo vya afya, ni vizuri utaratibu wa kukabidhi dawa uwe unazingatia taratibu zilizowekwa.
Matukio tofauti katika picha wakati wa uzinduzi
Ameongeza kusema wataalamu wa afya wanapaswa kuhakikisha dawa zinazopokelewa kutoka bohari ya dawa MSD ziwe zinahifadhiwa vizuri. Waganga wasimamizi wa vituo vya afya wahakikishe wakishapokea dawa wanaziingiza kwenye reja, lakini kuna kitabu cha dispense register ambacho kinaonesha dawa ambazo unaenda kutoa, na bill-card inayokuwa stoo. Ukifanya ukaguzi wa dawa zilizoingia na dawa zilizotoka bado mahesabu hayaleti uhalisia wa dawa zilizopo na dawa zilizotoka. Watendaji hawafuati utaratibu wa kujaza wakati wakiingiza dawa na wakati wa kuzitoa kwa wagonjwa. kutofuata utaratibu wa kuweka kumbukumbu sawa ya dawa zinazoingia na dawa zinazotoka ndio zinachangia upotevu wa dawa. Amesema katika kujenga mazingira ya uwazi katika utoaji wa huduma ni vyema wasimamizi wa vituo wakabandika aina ya dawa zinazopatikana kwenye zahanati, dawa zinazopatikana kwenye kituo cha afya ili kujengwa uelewa wa pamoja kwa wananchi.
matukio katika picha,watendaji wa afya wakisikiliza hotuba ya ufunguzi.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa