Na Tegemeo Kastus
Kuna baadhi ya maeneo ambayo wananchi wamejenga makazi ya kuishi ambayo awali yalikuwa ni mapitio ya wanyama. Halmashauri kwa kunashirikiana na Mamlaka ya hifadhi ya bonde la Ngorongoro tunaendelea kuhakikisha tunawarudisha wanyamapori katika eneo la hifadhi.
Hayo yamesemwa na Mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu Ndg. Waziri Mourice katika kilele cha siku ya wanyamapori kilichofanyika katika eneo linalojengwa Hospitali ya wilaya katika kijiji cha Changarawe. Ndg. Mourice ameomba mamlaka kuendelea kushirikiana na Halmashauri ili kuendelea kukabiliana na wanyama wanaoingia katika makazi ya watu. Kuwaondoa wanyama kwa wakati kunasaidia kutoleta madhara katika makazi ya watu lakini kunaondoa wanyamapori katika hatari ya ujangili.
Kaimu Mhifadhi wa Mamlaka ya Ngorongoro Dkt. Christopher Timbuka akipanda mti katika eneo linalojengwa Hospitali ya wilaya ya Karatu.
Ndg. Mourice ameomba mamlaka ya bonde la Ngorongoro kuweka wenye mpango wa bajaeti swala la matumizi bora ya ardhi katika kata zinazopakana na hifadhi. Amesema tukiwaelimisha wananchi, wakaingia katika mpango wa matumizi bora ya ardhi itasaidia kuondoa mivutano kati ya wananchi na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro. Amesema tukiwatunza hawa wanyama vizuri inasaidia shughuli za utalii kuongezeka na tunazidi kupata fedha za utalii.
Ndg. Waziri Mourice ameshukuru kwa fedha takribani million 800 zilizotolewa na mamlaka ya hifadhi ya bonde la ngorongo katika kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo. Amesema kati ya fedha hizo mamlaka imetoa kiasi cha million 600 kwa kujenga majengo matatu ya hospitali ya wilaya ambayo yako katika hatua mabalimbali za ujenzi, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la utawala na jengo la Maabara.
Ndg. Mourice amesema mamlaka imetoa miche ya miti zaidi ya 14000 katika Halmashauri ya Karatu bure katika miche hiyo miche 3000 imetolewa kwa ajili ya kupanda eneo linalojengwa Hospitali ya wilaya ya Karatu. Zoezi la upandaji wa miti limefanyika likiongozwa na kauli mbiu ya misitu na maisha endelevu ya watu na maliasili.
Makamu Mwenyekiti wa Halamshauri ya Karatu Mh. John Bayo akipanda mti katika eneo linalojengwa hospitali ya wilaya.
Ndg. Mourice amesema kupanda miti kunasaidia kuendeleza jitihada za kutunza mazingira kwenye eneo linalojengwa hospitali ya wilaya. katika kuendeleza ujirani mwema Mamlaka ya bonde la Ngorongoro inatoa mikopo kupitia Geopark. Mambo haya yasingewezekana kama tusingekuwa tumepakana na mamlaka ya bonde la ngorongo katika Halmashauri ya wilaya ya Karatu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. John Bayo ameomba Mamlaka ya hifadhi ya bonde la Ngorongoro kuwapa mafunzo vijana 50 ili wasaidie kufukuza wanyama pori wanaojitokeza sana katika Maeneo la kambi ya nyoka, Tloma maeneo ya Kata oldean Kata Daa kata ya Rhotia. Amesema wanyama wanaoingia kwenye makazi ya watu husababisha wanafunzi wa maeneo hayo kuwa na maendeleo mabaya kitaaluma. Hali inayosababishwa na kukosa kuhudhuria shule mara kwa mara kutokana na muingiliano wa wanyama katika maeneo ya makazi ya watu.
Akizungumza juu ya zoezi la upandaji wa miti kaimu mhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi ya Bonde la Ngorongo Dkt. Christopher Timbuka amesema faida za kupanda miti zimesaidia sana kupunguza utegemezi wa bidhaa za misitu. Amesema kesi za wananchi kuingia ndani ya hifadhi zimepungua akitolea mfano kata ya Mbulumbulu amesema wananchi wamepanda miti inayosaidia kuwapatia mbao na kuni.
Dkt. Timbuka amesema Mamlaka ya Hifadhi ya bonde la Ngorongoro katika jitihada za kuzuia athari zinazoweza kuletwa mabadiliko ya tabia ya nchi, Mamlaka imejikita katika kuongezea uwezo msitu wa kufyoza na kuhifadhi hewa ya ukaa kwa kurudishia msitu uoto wa asili ulioathirika kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu zisizorafiki kwa mazingira.
Ameongeza kusema Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro imeweza kuzuia uchomaji ovyo wa misitu kuzuia uchomaji wa mikaa, kuzuia mifugo wasio ruhusiwa ndani ya hifadhi, na kuzuia ukataji ovyo wa misitu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma na kujikita katika kulinda vyanzo vya maji.
Wananchi wa vijiji vya Changarawe na Dofa wakishiriki kupanda miti kwenye eneo linalojengwa hospitali ya wilaya.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa