Na Tegemeo Kastus
Serikali inafanya utaratibu wa kurasimisha maeneo kwa wananchi ili waweze kupata uwezo kutumia hati zao za kumiliki ardhi kupata mikopo. Watu wanaongezeka lakini eneo la ardhi linabaki kuwa lile lile hivyo ni vyema kuhifadhi na kuendeleza maeneo yetu badala ya kukimbilia kuyauza.Kadhia ya migogoro mingi ya ardhi kwa wananchi inachochewa na kukosekana uwazi kwa uongozi wa Halmashauri ya kijiji cha Marera katika uuzaji wa maeneo ya kijiji.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipokuwa akitatua kero za wananchi katika kata ya Rhotia na baadae kufanya mkutano wa hadhara aliozungumza na wananchi. Ameelekeza taasisi ya kuzuia na kupambana na rusha (Takukuru) kufanya uchunguzi kwa uongozi wa Halmashauri ya kijiji cha Marera. Baada ya malalamiko mengi kuelekezwa kwa Mwenyekiti wa kijiji cha Marera na mabalozi wanaotuhumiwa kufanya udalali wa kuuza viwanja kwa njia za udanganyifu jambo linaloibua migogoro mingi ya ardhi katika kijiji cha Marera.
Mwanachi akiwa amesimama na bango wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Rhotia Kati
Mh. Kayanda amesema asilimia 99 ya malalamiko ya wananchi ni mgogoro ya ardhi, amessema changamoto za migogoro ya ardhi zisipotatuliwa haraka zitasababisha uvunjifu wa amani. Amesema kila kiongozi Marera atakayebainika baada ya uchunguzi kufanyika kula fedha za wananchi au kujinufaisha atazirejesha fedha hizo. Amesema Takukuru watachunguza taarifa za mapato na matumizi za kijiji cha Marera pamoja na kiasi cha shilingi million tano ambazo zimekosa mchanganuo na vielelezo vyote vya malalamiko hayo vilivyotolewa na wananchi vimewasilishwa Takukuru tayari kwa kufanyiwa uchunguzi.
Akizungumzia malalamiko ya mabango yaliooneshwa na wanachi kuonesha kutokuwa na imani na Mwenyekiti wa kijiji cha Marera. Mh. Kayanda amesema wananchi wanapaswa kuandika orodha ya majina pamoja na saini zao zitakazoonesha nia ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti kisha mkutano Mkuu wa Halmashauri ya kijiji utaitishwa. Amesema utaratibu kumuondoa madarakani lazima ufuatwe kama ulivyofutwa wakati wa kumuweka madarakani.
Mh.Kayanda amewaasa viongozi wa serikali waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi ni vyema wakakubali kutoa ufafanuzi wa kina juu ya mambo wanayoulizwa na wananchi. Amesema huwezi kuwa kiongozi; wananchi wasikuhoji, uongozi ni pamoja na kutoa taarifa zinazowahusu wananchi kwa kina na kwa wakati, ili kuonesha dhana ya utawala bora. Viongozi wapo kwa niaba ya wananchi, katika kuongoza huwezi kukwepa maswali kutoka kwa wananchi.
Mh. Abbas Kayanda (kulia) Katika ofisi ya kijiji cha Rhotia akitatua kero za wananchi
Akizungumzia kuhusu swala gharama za maji kuwa juu katika kata ya Rhotia Mh. Abbas Kayanda amesema ametoa maelekezo kwa Mwenyekiti wa bodi ya maji Rhotia kupanga bei upya ya maji ili kutimiza dhana ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani. Amesema bei elekezi iliyowekwaa na serikali ni shilingi 1700 kwa unit moja ya maji. Amesema haipendezi wananchi kulalamika bei ya juu ya maji, ameongeza kusema Ruwasa katika bajeti ya maji ya mwaka ujao wa fedha 2021-2022 imepanga kurekebisha miundo mbinu ya maji Rhotia. Hivyo ukarabati huo utasaidia kuondoa miundo mbinu chakavu na kuimarisha upatikanaji wa maji kwa wananchi. Amesema lazima sasa bodi ifikirie namna ya kuongeza usambazaji wa maji kwa watu badala na kuweka bei ya juu katika kila unity moja ya maji inayotumiwa.
Wananchi wakizungumzia kuhusu kero ya maji ndg. Ramadhani Iddi amesema walikuwa wanalipa kiasi cha shilingi 2000 kwa unit moja ya maji ili kuwezesha maji kupatikana muda wote lakini matokeo yake uhaba wa maji ndio umeongezeka. Amesema swala la bei ya maji limekuwa likipigwa danadana jambo ambalo limekuwa likitoa picha mbaya kwa wananchi.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa