Mkuu wa mkoa wa arusha Mhe. Mrisho Gambo ameendelea na ziara yake ya kikazi wilayani Karatu. Mkuu wa mkoa ametembelea na kukagua eneo la madini ya dhahabu katika kijiji cha Endagem lilopo katika kitongoji cha Murus tarafa ya Endabash. Pamoja na kutembelea soko la madini liliopo kata ya Endabash ambalo uuzaji wa madini unafanyika siku ya alhamisi.
Mhe. Gambo amejionea shughuli za madini namna zinavyofanyika katika eneo hilo na akazungumza na wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu. Mhe. Mrisho Gambo amesema eneo hilo licha ya kuwa na watu waliokata leseni zaidi 500 lakini kwa ukubwa wa shughuli za uchimbaji wa madini haioneshi kama kuna idadi hiyo ya watu. Mkuu wa mkoa amesema hata mazingira ya uchimbaji siyo rafiki sana, amesema bado uchimbaji unafanyika kwa njia ambazo siyo za kisasa. Mhe. ametoa maelekezo eneo hilo kutengenezwa eneo la maliwato, lakini pia ametoa maelekezo kwa meneja wa Tanesco kufanya upembuzi yakinifu kuona namna ya kuleta umeme katika eneo hilo. Jambo litakalosaidia shughuli za uchimbaji wa madini, hasa katika mitambo inayotumia nishati ya umeme katika uchambuaji madini. (uchenjuaji wa madini)
Mhe. Theresia Mahongo Mkuu wa wilaya ya karatu amesema barabara ya kuelekea kijiji cha Endagem itaendelea kuboreshwa ili iweze kuwa nzuri na kupitika kwa urahisi. Amesema ukarabati tayari umeshaanza hasa katika maeneo korofi ya barabara. Barabara hiyo inahitaji fedha nyingi hasa kutokana na kuwepo kwa makorongo makubwa. Mhe. Mahongo amesema wakati wa mvua kwenye migodi huwa kunatokea majanga mengi, amewaomba wachimbaji kutoa taarifa haraka pindi matatizo yanapojitokeza.
Mkuu wa Mkoa wa arusha akipata maelekezo kutoka kwa mchimbaji juu hatua za usafishaji mpaka kupata madini.
Naye Muwakilishi wa afisa madini Mkazi ndugu Gabriel Senge amesema kuna maeneo takribani matano ya uchimbaji wa madini. Tangu mwaka 2002 kulikuwa na uchimbaji mkubwa wa shughuli za madini Endagem. Hivyo kuvutia wachimbaji wengi kuja na kujishughulisha na kazi za uchimbaji wa madini. Hiyo ilivutia watu wengi kukata leseni lakini katikati kukatokea mdororo wa shughuli za uchimbaji na mashimo ya migodi kuanguka. Ndugu Gabriel amesema hata bei ya dhahabu ilishuka na kuchangia pia shughuli za uchimbaji kupungua.
Ndugu Gabriel amesema kwa sasa bei ya madini ya dhahabu imeimarika na hata kiasi kinachopatikana cha madini kinanufaisha wachimbaji wadogo. Amesema kuna hati 302 za madai ya leseni na asilimia kubwa ya hati hizo za madai zinatoka katika eneo la Endabash. Hati hizo nyingi zinaisha muda wake mwaka huu na kuna ambazo zimeshaisha muda wake tangu mwezi wa kwanza. Amesema wameandika ombi la kufuta leseni 100 kwenda kwa Mtendaji mkuu wa tume ya madini. Ombi lao likiridhiwa hati hizo zitafutwa, muwakilishi wa afisa madini ameomba wananchi hasa wachimbaji wadogo kuomba leseni kupitia maafisa madini wakazi na wataalamu wengine walio katika wilaya ambao wanaweza kuwasaidia. Ndugu Gabriel amesema upo mfumo wa njia za mtandao (online) kwa kutumia GPS unaoweza kuonesha kama eneo limekatiwa leseni au halina leseni.
Mwenyekiti wa wachimbaji ndugu Afred Mwaswenya amesema kitaalamu kutoka shimo moja hadi jingine kunatakiwa kuachwe mita 10. Amesema zamani watu walikuwa hawafuati utaratibu huo ndio maana 2002 mashimo mengi yalianguka katika eneo hilo. Amesema kuna miamba 0.1, 0.2. 0.3 ya madini ya dhahabu yanayopatikana Endagem. Ndugu Mwaswenya amesema kwa sasa wanaweza kupata gramu100 mpaka 150 kwa mwezi. Ndugu afred ameshukuru kwa ujio wa mkuu wa mkoa kwenye machimbo ya Murus amesema kwenye machimbo hayo wanachangamoto ya upatikanaji wa maji. Amesema nyenzo wanazotumia kwenye uchimbaji si nzuri, amemuomba mkuu wa mkoa kupitia wizara ya madini kuwapa fedha hata kama ni kwa mkopo ili isaidie katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya uchimbaji wa madini.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa