NA TEGEMEO KASTUS
Wananchi wa kijiji cha Marera wamepata tumaini jipya baada ya ujenzi wa zahanati ya Marera ulioanza mwaka 2011 kukamilika. Zahanati hiyo inatarajia kutoa huduma za afya kwa kaya 462 zenye wakazi 2635, wazo la kujenga zahanati limetokana na umbali mrefu kutoka kijiji cha Marera mpaka kituo cha afya Karatu na gharama za juu za huduma afya katika kituo cha afya cha Rhotia kinachosimamiwa na kanisa katoliki.
Hayo yamesemwa Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati wa uzinduzi wa zahanati ya Marera. Ujenzi wa zahanati hiyo, wananchi wamechangia nguvu kazi million 14,775,700 Wadau wa maendeleo wamechangia Million 1 Halmashauri Million 45,876,000. Mh. Kayanda kipekee amempongeza Afisa mtendaji wa kijiji pamoja na Mwenyekiti wa kijiji cha Marera kwa kazi nzuri ya kusimamia na kumalizia ujenzi wa zahanati ya Marera. Ujenzi huo wa zahanati umeenda sambamba na ujenzi wa nyumba ya watumishi, amesema zahanati ya Marera imepata watumishi watatu, afisa tabibu mmoja, mhudumu wa afya na nesi. Ameomba wananchi wa kijiji cha Marera kuwapa ushirikiano mzuri wafanyakazi hao wa afya walioletwa katika zahanati hiyo, katika utendaji wa majukumu yao ya kazi.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda akifungua zahanati ya Marera
Mh. Kayanda amesema ujenzi wa zahanati ya Marera, umeonesha wazi kwamba wananchi wakiamua wanaweza kuleta maendeleo wenyewe. Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati na kila kata inakuwa na kituo cha afya na kila wilaya inakuwa na hospitali ya wilaya. Zahanati ya Marera imesajiliwa na itaanza kupata mgao wa dawa kutoka Msd.
Mh. Kayanda amesema Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli ameweka vipaombele katika kuboresha sekta ya afya, kuboresha sekta elimu, kuboresha sekta ya maji na miundo mbinu. Amesema vituo vya afya vya serikali vinatoa matibabu kwa wazee wa zaidi ya miaka 60 bure, kwa mtoto wa chini ya miaka 5 na mama mjamzito bure. Lakini pia kwa wilaya ya Karatu serikali imetoa kiasi cha billion 1 kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo ya hospitali ya wilaya ambayo ujenzi ulishaanza awali na ujenzi wa majengo mapya mengine manne.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda akikagua kichomea taka katika zahanati ya Marera
Mh. Kayanda amesema serikali imekuja na mfumo wa bima ya afya iliyoboreshwa ambao ukitoa shilling 30,000 kwa watu sita wa kaya moja wanapata huduma za afya kwa kipindi cha mwaka mzima. Ameomba wananchi kujiunga na mfuko huo, amesema kuumwa mtu hupangi ila kuumwa kuna kuja wakati wowote na unaweza kuumwa kipindi ambacho huna fedha. Amesema ni vyema wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa kwa sababu inasadia mwananchi kupata huduma wakati wowote.
Mh. Kayanda amesema kwa upande wa elimu serikali inatoa million 53 kila mwezi kwa uendeshaji wa shule ya msingi na million 73 zinatolewa kwa ajili ya uendeshaji wa shule za sekondari wilayani Karatu. Amesema jukumu la mzazi limebaki kununua sare za shule daftari la mtoto na kalamu, amesema hayo ndio mabadiliko yanayofanywa na serikali kwa wananchi.
Muonekano wa jengo la zahanati kwa nje
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa