NA TEGEMEO KASTUS
Serikali imetoa takribani million 210 kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika shule za sekondari wilayani Karatu. Fedha hizo zimetoka katika mfuko wa EP4R, Maabara hizo zitajengwa shule ya sekondari Domel, Mang’ola, Qurus, Getamock, Baray Khusumay, Diego na Kansay sekondari.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipokuwa anazungumza na walimu wakuu, Maafisa watendaji wa vijiji, Kata na watumishi wa afya katika tarafa ya Mbulumbulu katika mkutano uliofanyika shule ya sekondari Diego. Mkuu wa wilaya alitumia kikao hicho kusikiliza changamoto mbalimbali wanazokabiliana watumishi hao katika maeneo ya kazi. Aidha serikali itaendelea kuimarisha miundo mbinu ya afya na elimu hatua kwa hatua.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda akiwa katika kikao na watumishi
Mh. Kayanda amesema katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu, bado serikali inaendelea kuajiri walimu, na pia Halmashauri itagawa walimu waliopo katika shule ambazo hazina walimu kabisa, mathalani kama shule ina walimu wa hesabu au phyisics wawili basi mmoja aende shule isiyo na mwalimu hata mmoja wa masomo hayo. Mh. Kayanda amesema upo umuhimu wa kuwapongeza walimu wanaofanya vizuri katika ufundishaji na ufaulishaji. Amesema jambo hilo litawaongezea ari walimu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Mh. Kayanda ametoa maelekezo kwa Maafisa watendaji wa kijiji; kata, na tarafa kujenga tabia kutembelea taasisi zinazowazunguka katika maeneo yao ya kiutendaji, ili kubaini changamoto na kuzitatua ikiwa ni pamoja na kuzitolea taarifa wilayani changamoto ambazo ziko nje ya uwezo wao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi. Amesema watendaji wanapaswa kufuatilia na kuchukua hatua za kisheria kwa wanafunzi waliopewa mimba. Maafisa hao watendaji wanapaswa kufuatilia na kuchukua hatua kwa wanafunzi watoro kwa kuhakikisha wanarejea shuleni.
Mh. Kayanda amesema serikali imefanya ukarabati na ujenzi wa miundo mbinu katika kituo cha afya Kambi ya simba kwa gharama ya zaidi ya million 500. Amesema serikali imepeleka vifaa na vifaa tiba katika kituo cha afya kambi ya simba vienye thamani ya zaidi ya million 200 na sasa upo mkakati wa kuchimba kisima cha maji ili kusaidia kituo cha afya kambi ya simba kuwa na maji ya uhakika muda wote. Mh.Kayanda amesema serikali imetoa fedha million 400 Kituo cha afya Endabash kwa ajili ya ujenzi na ukarabati na ujenzi, kituo hicho cha afya pia kimepokea vifaa na vifaa tiba . Mh. Kayanda ameomba watumishi kuthamini na kutunza miundo mbinu inayojengwa katika sekta ya afya na elimu.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa