Maadhimisho ya siku ya sheria yamefanyika jana katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Karatu. Sherehe hizo zimeenda sambamba na kufungua mwaka mpya wa Mahakama na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa ni Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo
Maadhimisho hayo ya siku ya sheria yalikuwa na kauli mbiu inayosema; UTOAJI HAKI KWA WAKATI NA WAJIBU KWA MAHAKAMA NA WADAU. Mhe. Theresia Mahongo katika hotuba yake amewapongeza wadau sheria kwa kutumia siku hiyo kutoa elimu. Amesema elimu haina mwisho, wananchi wakipata elimu vizuri wanasheria wasio na taaluma (Bush lawyers) hawana nafasi.
Mhe. Theresia amesema kushindwa kutolewa haki kwa wakati limekuwa ni tatizo kubwa, bado kuna watu kwenye Mahakama wanaojihusisha na vitendo vya rushwa. Mhe.Theresia amesema rushwa ni adui wa haki na uongozi wa awamu ya tano umekuwa ukikemea sana rushwa.
Mhe. Theresia amewaelekeza wanasheria kuja na mkakati wa kuwadhibiti Wanasheria wasio na taaluma (Bush lawyers). Wanasheria vihio wamekuwa wakiwaonea sana wananchi, Mhe Theresia amesisitza pia wananchi kupewa elimu ya namna ya kupewa dhamana. Amesema kumekuwa na mkanganyiko kwenye kutoa dhamana kuna wakati mdhaminiwa anatakiwa aje na Mwenyekiti wa kijiji maeneo ya kijijini na wakati mwingine Mwenyekiti wa kijiji anakataliwa na kutaka mtu anayehitaji dhamana kwenda na Mtendaji wa Kata.
Mhe. Theresia amesema kuna mihimili mitatu ambayo ni Serikali, Mahakama, na Bunge. Amesema mihimili hii haingiliani katika kutekeleza majukumu yake, ameomba wananchi wenye kesi mahakamani au baraza la ardhi waendelee na kesi zao mpaka zinapokwisha.
Mhe. Theresia amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwenye vyombo vya sheria ili wapate haki zao. Mahakamani kuna fomu za malalamiko ameomba wananchi wazitumie fomu hizo ili kero zao ziweze kutatuliwa.
Awali Hakimu Mkazi Mfawidhi Mhe. Kuppa amesema hakuna haki bila wajibu, kila mtu anapaswa kutoa haki. Kunyimwa haki ni uonevu mkubwa, nchi yenye misingi ya kikatiba na utawala wa sheria Mahakama ndio chombo kinachotoa haki.
Mhe. Kuppa amesema Mahakama ya Wilaya ya Karatu imejiwekea utaratibu kwa Mahakama za Mwanzo uhai wa kesi uwe ni miezi sita na Mahakama ya Wilaya uhai wa shauri lolote uwe ni miezi kumi na mbili na shauri la madai liwe miezi kumi. Amesema nakala za maamuzi au hukumu hutolewa ndani ya siku ishirini na moja. Usipopata nakala kwa kipindi hicho unanza kufuatilia kwa Hakimu Mfawidhi wa kituo hicho.
Mhe. Kuppa amesema wadau wa Mahakama wanatakiwa kuwa na utamaduni wa kusuluhishana wao wenyewe kupitia katika ngazi ya familia na viongozi mbalimbali kwa mashauri ya kesi ambayo hayana uzito mkubwa kwa mantiki ya adhabu zake kisheria.
Naye O.C. D wa Karatu S.P Musa Gumbo alisema kesi za madawa ya kulevya; nyara za serikali, au kesi za kuhujumu uchumi lazima vielelezo vipelekwe kwa Mkemia mkuu wa serikali. Baada ya hatua hizo lazima majalada yapelekwe kwa Mkurugenzi wa makosa ya jinai ndipo kibali cha kuendesha kesi kinapotolewa. S.P Musa Gumbo amesema ni matakwa ya kisheria kupeleka vielelezo kwa Mkemia mkuu wa serikali na Mkurugenzi wa makosa ya jinai bila kufanya hivyo upelelezi unakuwa haujakamilika na hii inasababisha kesi kuchukua muda mrefu.
S.P Gumbo amesema kutoa haki kwa wakati kwa mashauri kunategemeana na kuita mashahidi kwenye Mahakama kwa ajili ya kutoa ushahidi, amesema huwa wanapata changamoto hasa pale wanapoita mashahidi wa mbali. S.P Gumbo amesema Mahakama huwa ni mkusanyiko wa Mahakama yenyewe, Waendesha Mashitaka na Mawakili. Afisa mmoja anapopata dhararura kati ya hawa Mwendesha mashitaka, Hakimu au Wakili kesi inaahirishwa na kupangiwa tarehe nyingine. Mashahidi hawa wengi wao wanatoka mbali na shahidi hulipwa pesa yake baada ya kutoa ushahidi Mahakamani. Kutokana na changamoto kama hizo mashahidi huwa hawarudi Mahakamani kwa wakati pindi kesi inapoahirishwa na imekuwa ni kikwazo kikubwa kuendesha kesi kwa wakati, kwenye makosa ya jinai
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa