Mkuu wa wilaya ya Karatu ameahidi kupeleka huduma ya maji kwenye kijiji cha Laja na vijiji vya jirani. Mhe. Theresia amesema hayo katika mkutano na wanakijiji wa kijiji cha Laja alipokuwa akisikiliza kero za wananchi. Mkutano huo ulihusisha wataalamu na wajumbe wa kijiji na wananchi wa kijiji cha Laja uliolenga kutatua kero za wananchi.
Mhe. Theresia amesema anafahamu adhaa ya maji wanayopata wananchi wa kijiji cha Laja na vijiji vya jirani. Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa shirika la world vision wataanza kujenga miundo mbinu ya maji mwezi wa kumi mwaka huu. Mhe. Theresia amewahakikishia wananchi wa Laja mradi wa maji utaanza kwa wakati. Amewaomba wananchi kushiriki kwa kujitolea kuchimba mitaro wakati wa ujenzi wa miundo mbinu ya maji.
Wananchi wakiwa katika mkutano kijiji cha Laja
Mhe. Theresia amewahimiza wananchi kupenda kupata matibabu hospitali, amesema amepewa taarifa kijiji cha Laja kwamba wakinamama wajawazito wanaogopa kwa sababu kuna tabibu na wauguzi wa kiume. Mhe. Theresia amesema serikali italeta mhudumu wa kike, lakini bado wanapaswa kwenda hospital ili wapatiwe huduma ya kitabibu. Matabibu na wauguzi wa kiume wamesomea kazi ya kutoa tiba, hivyo amewaasa wakinamama wajawazito kuanza kwenda hospitali mapema. Mhe. Theresia amesema kitanda cha kujifungulia kilikuwa kibovu katika zahanati ya Laja lakini sasa kinafanya kazi vizuri. Mhe Theresia amesema wakinamama waanze kuhudhuria Hospitali kuanzia wiki kumi na mbili, ili kufahamu maendeleo ya ujauzito wake na kuona kama mtoto amekaa sawa.
Mhe. Theresia ametumia mkutano huo kuwakumbusha wananchi juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa, amewaomba wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu. Amewahimiza wananchi kuchagua viongozi bora na siyo bora viongozi. Mhe.Theresia amewaomba wananchi kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo. Mhe. Theresia amewaomba wananchi kutochagua viongozi wanaotoa rushwa. Amesema daftari la kupiga kura litaboreshwa, amesema wananchi waliofikisha umri wa miaka 18, wajitokeze kuandikishwa na wananchi waliobadili makazi, waende na wabadili taarifa zao. Mhe. Theresia amesema taarifa za marekebisho kwa daftari la kupiga kura zitatolewa na mkurugenzi mtendaji wa wilaya.
Awali katika kikao hicho ndugu Emmanuel Mganga na Bi, Julielth Daudi wamesema kijiji cha Laja na vijiji vya jirani vina adha ya maji. Wamesema kijiji cha Laja kuna kisima ambacho kimechimbwa mda mrefu lakini kimeshindwa kutoa maji. Wananchi wamedai kijiji cha Laja kina josho la mifugo lakini nalo limeshindwa kufanya kazi kwa kukosa huduma ya maji ya kuweka katika josho.
Wananchi wakiwa wanasikiliza mKutano
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa