NA TEGEMEO KASTUS
Viongozi waswaa kuacha kujikweza na kutumia nyadhifa za uongozi walizo nazo vibaya na badala yake waheshimu kila mtumishi kwa nafasi yake. Kila mfanyakazi ni muhimu kwa nafasi aliyonayo ndio maana yupo kwenye utumishi wa umma. Watumishi lazima tujaliane wenyewe kwa wenyewe na tuwe kitu kimoja.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipokutana kusikiliza changamoto za watumishi wa tarafa ya Karatu uliowajumuisha walimu wakuu, walimu wa kawaida, watumishi wa afya, watumishi wa kilimo na mifugo, na maafisa watendaji kata na vijiji. Amesema lazima watumishi wawe na ushirikiano katika utendaji kazi, wakifanya hivyo watakuwa na mafanikio makubwa sana. Watumishi wanapaswa kupewa moyo na viongozi na kutembelewa mara kwa mara katika mazingira wanayofanya kazi. Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na watumishi katika ujenzi wa taifa letu.
Mh. Abbas Kayanda akizungumza na watumishi wa Tarafa ya Karatu
Mh. Kayanda amegusia kuhusu elimu amesema swala la chakula kwa wanafunzi lina umuhimu wa kipekee na limekuwa likitoa matokea chanya hasa katika shule ambazo wanafunzi wanapata chakula cha mchana. lakini pia kuna kuchangia walimu wa ziada wanaosaidia kufundisha watoto, Mh. Kayanda amesema ataendelea kuzungumza na wananchi ili waone umuhimu wa kuchangia hususani pale wazazi wanapokubaliana. Katika swala la utoro wa wanafunzi amesema watendaji wa kijiji na kata wanapaswa kusimamia na kudhibiti utoro wa wanafunzi, hata katika sheria ya elimu ya mwaka 1967 imeeleza bayana mamlaka za watendaji wa kijiji na kata moja ya jukumu lao ni kuhakikisha wanafunzi watoro wanarejea shuleni.
Mh. Kayanda amesema swala la kunyanyua kiwango cha ufaulu ni jambo linategemea mafiga matatu. Amesema ufaulu unamhusu Mwalimu, ufaulu unamhusu Mwanafunzi na unamhusu mzazi au Mlezi. Amesema mmoja kati yao akikosekana hakuna muujiza unaweza kuongeza kiwango cha ufaulu. Mwalimu anaweza akajitahidi lakini mwanafunzi asijitahidi, mwanafunzi na mwalimu wanaweza wakajitahidi lakini mzazi asitoe ushirikiano. Lazima wote watatu wawe kitu kimoja ndipo waweze kuleta matokeo mazuri katika sekta ya elimu. Mh. Kayanda amesema kuna tabia imejengeka ya swala la walimu walewale kusimamia mitihani kila mwaka amesema swala hilo litafanyiwa kazi na kila mwalimu mwenye sifa ya kufundisha zaidi ya kipindi cha miaka mitatu na kuendelea kama inavyohitajika, atapewa nafasi ya kusimamia mitihani ya kidato cha pili na kidato cha nne.
watumishi wakimskiliza Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda
Mh . Kayanda amesema swala la kufanya mdahalo juu maendeleo ya hali ya taaluma ya wilaya ya Karatu litafanyika mwanzoni mwa mwaka ujao. Swala hilo litakusanya wadau wa elimu na walimu wenyewe, amesema kuna mambo ambayo wadau wa elimu wanapaswa kusaidia na kuna mambo ambayo waalimu wanapaswa kuyafanya.
Naye Afisa elimu taaluma wa sekondari wa wilaya Mwl. Robert Sijaona akizungumzia uboreshaji wa ufaulu ili kupata wanafunzi wenye ubora zaidi, amesema serikali inafanya mabadiliko ya mfumo wa elimu hatua kwa hatua kuendana na mahitaji. Amesema swala la kubadili mfumo wa haliwezi kufanyika ghafula. Mwl. Sijaona amesema kwa sasa serikali imeanza kuwapa semina za kujengea uwezo walimu wa KKK. Ili kuongeza ujuzi wa kuwasaidia wanafunzi kujua kusoma kuandika na kuhesabu. Amewapongeza walimu wa shule ya msingi kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kujenga wasomi wa baadae. Ametoa raia kwa walimu wa sekondari kufanya jitihada za hali na mali kusaidia wanafunzi wanaoingia shule za sekondari kupata hamasa za kufahamu masomo wanayo jifunza kwa ufasaha. Amesema ipo changamoto ya kutumia lugha ambayo mwalimu akimsaidia mwanafunzi kwa karibu anaipokea vizuri. Amesema wanafunzi wanapishana uwezo wa uelewa kuna mwanafunzi anaelewa taratibu na kuna mwanafunzi wanaelewa haraka. Wote hawa sisi tunapaswa kuhakikisha wanafikia matarajio ya ndoto zao.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa