Na Tegemeo Kastus
Matokeo ya kitaifa ya mtihani wa darasa la saba yaliyotangazwa hivi karibuni na katibu wa baraza la mitihani Dkt. Charles Msonde yameiletea Halmashauri ya wilaya ya Karatu heshima ya pekee kwa kutoa mwanafunzi aliyefaulu vizuri kwa kushika nafasi ya tatu kwa ngazi ya kitaifa. Mwanafunzi huyo Given Cosmas Malyango ndiye mwanafunzi anayeongoza kwa ufaulu vizuri kwa upande wa wanafunzi wa kike.
Given Cosmass Malyango ni mtoto pekee kwa baba na mama yake, ana umri wa miaka 13. Mama yake ni mwalimu wa shule ya msingi Sumawe Karatu na baba yake ni mwalimu shule msingi katika moja ya shule Mkoani Dar-es salaam. Alianza elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Dudiye mkoani Manyara ambayo ilikuwa shule ya serikali na alisoma kwa kipindi cha miezi sita mwaka 2010. Mama yake Goodness Kirway alipopata uhamisho kwenda karatu, akafanya mtihani wa awali wa kujiunga na shule binafsi ya Tumaini Junior japo ufaulu wake haukuwa mzuri.
Given alipokuwa darasa la kwanza, katika shule ya Tumaini junior English medium school mtihani wa mwisho wa mwaka wa darasa la kwanza alishika nafasi ya pili kati ya wanafunzi arobaini. Darasa la pili katika matokeo yake akawa miongoni mwa wanafunzi wa tano waliofanya vizuri. Kuanzia darasa la tatu mpaka la saba akawa mtu wa kwanza; licha ya uwezo wa darasani Given ni kiongozi bora, amewahi kuwa dada mkuu msaidizi na baadae kuwa dada mkuu, wadhifa ambao amemaliza nao Tumani Junior English medium school.
Given anasema yeye ni mtu anayependa kutunza mda, alipokuwa shule alikuwa anatumia mda vizuri anafanya kazi mda wa kazi na mda wa kusoma anautumia vizuri kusoma. Given anasema ya shule iliwapangia mda mzuri wa kusali kwa pamoja jioni na asubuhi. Lakini siri ya mafanikio yake ni kusali na kusoma kwa bidii, huwa anasali pia peke yake kabla kulala na wakati wa kuamka licha ya kusali na wenzake. Shule iliwapa mazoezi ya mtihani ya wiki na mitihani ya mwezi ambayo walikuwa wanashindana na shule nyingine kimikoa. Lakini pia anawanafunzi ambao ni marafiki zake alioshirikiana nao kimasomo na kwenye changamoto mbalimbali ambao ni Caster Sizza ambaye ni mwenyeji wa Musoma na Emmaculate Alex ambaye ni mwenyeji wa Moshi.
Tabia ya kusali amefundishwa na mama yake mzazi Bi, Goodness Kirway, Given anasema mama yake ni mfariji wake mkubwa na amekuwa akimpa moyo pindi anapopata changamoto katika maisha yake ya shule. Given anasema baba yake Cosmass Malyango pia ni mtu anayependa maendeleo, kupitia kusoma. Mzee Cosmass Malyango hapendi familia yake ipate shida. Given anakumbuka alishawahi kupoteza kiasi cha shilling 30,000 akiwa kwenye ziara ya kutembelea Hifadhi ya ziwa Manyara akafadhaika sana, lakini alipoomba mwalimu awasiliane na mama yake alipewa kiasi hicho cha fedha alichopoteza.
Changamoto alizozipata akiwa shuleni ni swala la kuamka asubuhi na mapema ili kujiandaa na vipindi vya masomo. Kadhia nyingine aliyokuwa akikabiliana nayo ni jinsi ya kuhamisha jibu kupeleka katika karatasi ya maswali. Given anasema kuna wakati alikuwa anakosea majibu siyo kwa kutofahamu swali bali ni ile hali kujichanganya wakati wa kuandika majibu.Given anasema yote tisa kumi ni swala la kushindwa na mwanafunzi wa Costigan kwenye mtihani wa PESNO uliofanyika mwezi wa tatu mwaka huu na kuzidiwa kwa alama mbili. Anasema ni bora hata angezidiwa kwa alama tano kumi siyo mbaya kuliko kuzidiwa kwa alama mbili.
Given anasema kuwa mwanafunzi wa tatu kitaifa haikutokea kwa bahati mbaya, alijipanga vyema katika masomo yake. Amesema jitihada hizi hazitaishia hapo anajipanga kwa miaka minne ijayo aweze kufanya vizuri zaidi. Given anasema yeye anapenda masomo ya sayansi ingawa masomo yote anafaulu kwa uwiano sawa. Lengo lake ni kuja kuwa Mnajimu kwa sababu watu wengi wanaiogopa taaluma hiyo kwa sababu ya gharama za kusoma. Lakini wanaogopa kwa sababu wanaona kwenda angani kufanya utafiti wa kisayansi ni kwenda kinyume na mipango ya mungu. Given anasema mtu anayemhamasisha ni Mnajimu mwenye asili ya marekani anayeitwa Neil Armstrong. Given anasema atafurahi sana kama atatimiza ndoto zake hizo. Given anapenda kusoma Chuo kikuu cha Dar es salamu; madhari yake alivyoona kwenye picha ni mazuri, lakini kwa namna ambavyo Dkt Chris Mauki Mhadhiri wa chuo hicho alivyoelezea kuhusu chuo hicho, alipowatembelea wanafunzi hao shuleni kwao Tumaini Junior Karatu
Given pia anapenda michezo anacheza mpira wa pete nafasi ya kiungo wa katikati na anacheza mpira huo kama kiungo mshambuliaji upande wa pembeni. Given anasema anaweza kucheza mpira wa miguu wa wanawake, yeye hucheza kama beki wa katikati. Given anasema yeye ni shabiki wa klabu ya Barcelona na Yanga kwa Tanzania. Anapenda unyumbulifu wa Lionel Messi katika mpira wa miguu na jinsi anavyotoa ushirikiano kwa wachezaji wenzake. Given amesema licha ya kupenda michezo yeye atajikita zaidi kwenye maswala ya taaluma.
Given anasema yeye akiwa nyumbani anapenda kumsaidia mama yake shughuli za nyumbani kupika kufanya usafi na mda wa ziada hutumia kuangalia katuni. Anaamini siku moja naye atakuwa jasiri, mama yake humuambia ukitaka maisha yawe magumu yatakuwa magumu na ukitaka maisha yawe rahisi yanakuwa rahisi. Pamoja na mafanikio ya Given, msingi mkubwa umebakia katika imani yake ya kusali na kufanya kazi kwa bidii. Given anawahusia wadogo zake aliowaacha shule ya msingi, ili wafanikiwe hawana budi wafanye kazi kwa bidii.
Bi, Goodness Kirway mama mzazi wa Given nasema mwane amempa heshima kubwa, anamini msingi mkubwa wa mafanikio upo katika elimu. Anakumbuka kitu kilichompa changamoto, ni wakati Given anaanza shule hakuwa na ufaulu mzuri kama mzazi akawa anamuombea ili afaulu vizuri na mungu anamemsaidia matokeo yanaonekana. Bi, Goodness, anasema anapenda mwanae awe Daktari wa binadamu, kwa sababu tangu alipokuwa mdogo alionesha nia ya kuwa daktari kwa michezo ile ya kitoto aliyokuwa anacheza nyumbani. Anakumbuka mwanae aliopokuwa mdogo alishamuambia babu yake anataka kuwa daktari ili afanye utafiti kwanini mtu akizeeka nywele zake zinabadilika nakuwa nyeupe. Bi, Goodness amesema licha ya kuwa anapenda mwanae kuwa Daktari anamruhusu kuendelea na ndoto zake kuwa Mnajimu.
Mwalimu mkuu Bi, Grace Benedict Saguma anasema, Given amempa amani sana, na amemjengea jina. Bi, Grace anasema Given ananidhamu ya hali ya juu sana na alikuwa anasoma kwa bidii hayo yaliyotokea waliyatarajia .Bi, Grace anasema Tumaini Junior ni shule inayofanya vizuri sana Wilaya ya Karatu kwa sababu ya mshikamano wao na hili lilitokea limezidi kuwatangaza zaidi.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa