Nyoka ni viumbe hai ambao wako kwenye kundi la reptilia ambao kundi hili la viumbe hai lina damu baridi na magamba. Kundi hili hujumuisha wanyama wa aina mbalimbali lakini tutajikita katika kumzungumzia nyoka. Nyoka wanatambaa kwa sababu hawana miguu na hutumia sumu kuwinda lakini wakati mwingine wanashika mawindo ya vyakula vyao kwa miili au midomo. Nyoka huwa wana ukubwa wa sentimita 10 hadi mita saba 7.6 kwa mujibu wa Afisa wanyamapori Cornel Lengai.
Nyoka hawa wamegawanyika katika makundi mawili, nyoka wenye sumu na nyoka wasio na sumu.Inakadiriwa kwamba kuna aina za nyoka takribani 3,000 duniani na Inaaminika kati ya aina hizo za nyoka ni aina 375 ndio wenye sumu. Nyoka huwa anaogopa sana binadamu kuliko binadamu anavyoogopa nyoka. Nyoka anapenda kujificha sana na hapendi kukaa mazingira anayokutana na binadamu.
Afisa wanyamapori ndugu Lengai anasema nyoka hutafuta namna ya kutoroka au kujihami anapokabiliana binadamu na ili aweze kumkimbia. Nyoka mwenye sumu hapendi kutumia sumu yake vibaya kwa sababu anatumia nguvu nyingi kuitoa. Hutumia sumu wakati wa makabiliano, ndio maana hata nyoka wanao rusha mate, hufanya makadirio ya hali ya juu kuhakikisha yameingia machoni kwa mtu anayekabiliana naye.
Afisa wanyamapori ndugu Lengai anasema sumu za nyoka zinatofautiana kutoka aina moja ya nyoka kwenda aina nyingine ya nyoka. Kuna nyoka kama koboko anaweza kukabiliana na idadi kubwa ya maadui kwa kugonga na kuacha sumu kwa kila anayeingia kwenye makabiliano. Lakini kuna aina ya nyoka wenye sumu ambao hawana uwezo huo wa kukabiliana na idadi kubwa ya maadui kwa wakati mmoja.
Afisa wanyamapori ndugu Lengai anasema nyoka hujilinda kwa kuuma bila kuacha meno yenye sumu (dry bite) ili kukabiliana na mazingira husika. Hufanya hivyo ili kuhifadhi sumu yake ili inapotokea matumizi sahihi aweze kutumia. Humsaidia kuhifadhi nguvu yake mwilini kwa sababu kitendo cha kutoa sumu humfanya atumie nguvu nyingi.
Nyoka wenye sumu kali wanaopatikana afrika ni pamoja na (black mamba) koboko (puff adder) kifutu (spitting cobras) swira. Nyoka hawa wanatofautiana sumu, afisa wanyamapori ndugu Lengai anasema sumu aina cytotoxin hushambulia seli za juu za mwili wa mgonjwa na kuziharibu au kuleta kidonda. Sumu hiyo hupatikana kwa nyoka kama kifutu (puff adder) na spitting cobra.
Sumu aina ya haemotoxin ni sumu ambayo humsababisha Mgonjwa Muathirika damu yake kuwa nyepesi sana na kuanza kuvuja ndani kwa ndani au kushindwa kuganda kama inamwagika kutoka kwenye kidonda. Nyoka aina ya bomsling kitaalamu ndio mwenye sumu ya haemoxin ambayo akigonga husabisha mgonjwa kutoa damu sehemu zote za wazi za mwili, kitendo ambacho husababisha mgonjwa kufariki.
Sumu aina ya neurotoxin hushambulia mishipa ya fahamu ya mgonjwa. Mgonjwa akipata sumu hii hawezi kufanya chochote hata kutikisa kidole, na mgonjwa hufariki baada ya muda mfupi. Nyoka aina ya black mamba na true cobra ndio wanaotoa sumu ya aina hii wanapomgonga mgonjwa. Nyoka hawa aina ya cobra wanauwezo wa kurusha mate usawa wa macho ya binadamu wakati wa makabiliano na sumu ya mate yake inapoingia kwenye macho ya binadamu inaweza kusabaisha upofu.
Sumu aina ya cardiotoxin husababishia mgonjwa alijeruhiwa na nyoka mwenye sumu ya aina hiyo mapigo yake ya moyo kusimama na kufa.
Sumu aina ya Myotoxin husababisha mgonjwa aliyejeruhiwa kushambuliwa misuli yote na kusababisha kifo kwa mgonjwa.
Afisa wanyamapori Ndugu Lengai anasema mgonjwa aliyejeruhiwa na nyoka dalili ya kwanza inayojitokeza ni maumivu makali katka sehemu aliyoshambuliwa. Mgonjwa anapata ganzi, kuvimba sehemu husika ya jeraha, kuanza kuvuja kwa damu ambayo isipozuiliwa huweza kuua mishipa ya fahamu. Nyoka huweza kutoa sumu kali kwenye mishipa ya fahamu ambayo husimamisha shughuli ya upumuaji na kuua mgonjwa aliyejeruhiwa kabla ya matibabu. Dalili nyingine ni pamoja na mgonjwa alijeruhiwa kushindwa kupuma vizuri, kushindwa kuona na kushindwa kusema.
Afisa wanyamapori ndugu Lengai anasema ili kufanikisha huduma ya kwanza kwa kiwango stahiki na kwa uhakika ni vyema kuwa na ufahamu kwamba mtu aliyejeruhiwa, ameng'atwa na nyoka wa aina gani, kwa rangi, umbo la kichwa ama aina ya magamba kwani kila aina ya nyoka ina huduma yake ya kwanza
Afisa wanyamapori anasema Mathalani kama mtu aliyeng'atwa na kifutu (Puff adder), hushauriwi kutoa hudumu ya kumfunga kiungo kwa sababu inaweza kusababisha kiungo kuoza au kuharibika kwa haraka zaidi, japokuwa kwa mtu aliyeng'atwa na mamba, forest, (Egyptian cobras) swira unaweza kumfunga kwani itasaidia sumu kutosambaa kwa uwepesi kupitia mzunguko wa damu.
Huduma za kwanza unazopaswa kumpa mgonjwa aliyejeruhiwa na nyoka ni kumuondoa muathirika katika eneo la hatari na kumpeleka eneo lenye usalama. Lakini pia unapaswa kumpa matumaini majeruhi kwa sababu inawezekana majeruhi ameumwa na nyoka asiye na sumu au nyoka aliye mgonga amefanya (dry bite) ameuma bila kumwekea mtu sumu yenye madhara.
Unapaswa kumuondoa mgonjwa nguo zinazobana, bangili ushanga kutegemea na sehemu aliyojeruhiwa. Kama mgonjwa amejeruhiwa mguu mtoe viatu katika mguu uliong’atwa na nyoka. Unashauriwa kumlaza au umkalishe chini ikiwa kama eneo liloathirika ni chini ya moyo. Unapaswa pia kuepuka kumtembeza kwani shughuli yoyote ya kutumia nguvu inaweza kuharakisha mzunguko wa sumu mwilini.
Afisa wanyama pori ndugu Lengai anasema Eneo ilioathiriwa/ alilong'atwa/kidonda ama kutemewa sumu unaweza kuosha kwa kutumia maji safi na sabuni. Epuka matibabu ya asili / kienyeji kwani inaweza kumsababishia mgonjwa hatari, njia za asili kama ya kuweka jiwe haina uhalisia wowote wa kuponyesha mgonjwa. Afisa wanyamapori ndugu Lengai anasema mpaka sasa hakuna njia ya asili ya kienyeji iliyothibitishwa na wataalam kuwa inatibu sumu ya nyoka. Inapendekezwa kitaalamu kumsafirisha mgonjwa haraka kwenye kituo cha afya ili aweze kupata huduma za matibabu.
Huduma za matibabu hutegemea kama kuongeza maji mwilini ambayo husaidia kuongeza presha ya damu na kupunguza sumu sambamba na dawa za kuua bacteria, dawa za maumivu ikiwa ni pamoja na kuchomwa sindano ya kuzuia tetenasi. Mgonjwa atapewa dawa ya kuondoa sumu mwilini kama ikithibitika nyoka alikuwa na sumu ambayo inaitwa kitaalamu Polyvalent antisera. Mgonjwa na hutakiwa kuondolewa sumu ndani ya dakika 20 la sivyo mgonjwa atafariki. Mtu aliyegongwa na nyoka asiye na sumu hapaswi kupewa dawa ya aina hii.
Afisa wanyamapori ndugu Lengai anasema ni vyema kukata nyasi ziwe fupi ndogo na uondoe masalia yote ya nyasi zilizokatwa au majani makavu yaliyoanguka na kujikusanya, kadhalika ni vyema uondoe sehemu za mti zilizoanguka juu ya paa au zinazoning’inia juu ya nyumba yako.Fukia mashimo madogo na makubwa yasiyo na kazi katika maeneo ya nyumbani na mashambani na ondoa vichaka eneo unaloishi.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa