Na Tegemeo Kastus
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Theresia Mahongo amepokea mchango wa fedha kutoka kwa viongozi wa kanisa la sabato Karatu. Michango hiyo imetolewa baada ya Mkuu wa wilaya kuhamasisha wadau kuchangia michango ili kununua vifaa tiba vya kukabiliana na tishio la ugonjwa (COVID-19) virusi vya corona.
Mhe. Mahongo ameshukuru wachungaji wa kanisa la sabato kwa msaada wa fedha kiasi cha Tsh 1,510,000 utakaotumika kununua vifaa mbalimbali vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona. Mhe. Mahongo amesema kanisa la KKT Karatu nalo linatarajia kutoa kiasi cha Tsh 1,000,000 kwa ajili ya kununua vifaa vya kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona. Mhe. Mahongo ameshukuru wadau wote wanaoendelea kuchangia vifaa kwa ajili ya kukabiliana na janga la ugonjwa wa virusi vya corona.
Mhe. Mahongo amesema wameshapokea vifaa vingine vichache kutoka kwa wadau wengine ambavyo ni mabuti, kuna wadau waliochangia (mask) barakoa, wadau wengine wamechangia gloves, kuna wadau waliochangia fedha kiasi cha Tsh. 600,000 mpaka wakati anakutana na viongozi hao wa kanisa la sabato.
Mhe. Mahongo amewahakikishia viongozi wa kanisa la Sabato kwamba fedha zilizotolewa zitatumika vizuri na mchanganuo wa matumizi yake utawekwa wazi. Amesema fedha hizo zitaenda kununua vifaa ambavyo waliomba siku za awali na vitafanyia kazi ambayo inatarajiwa kufanywa. Mhe Mahongo amesema ofisi ya Mkuu wa wilaya itatoa barua ya kuwatambua wadau kwa mchango wao.
Mhe. Mahongo amesema daktari aliyemhudumia mgonjwa ambaye baadae alibainika ana virusi vya corona huko Longido alikuja Karatu. Tayari mshukiwa huyo amechukukuliwa na kupelekwa Arusha kwa uangalizi (karantini) na nyumba ya wageni aliyofikia Karatu imewekwa karantini. Mhe. Mahongo amesema watu watatu wako chini ya uangalizi (wamewekwa karantini) na ufuatilia unaendelea ili kujua mganga huyo amekutana na watu wangapi (contact tracing).
Mhe. Mahongo amesema tunafanya hivyo ili kuendelea kujikinga, amesema wahudumu wa nyumba za wageni walishapewa maelekezo kuendelea kujihadhari kwa kuvaa (mask) Barakoa na gloves wakati wa kuhudumia watu ili kujikinga na maambukizi.
Mkuu wa wilaya Mhe. Theresia Mahongo akiwa katika kikao na viongozi wa kanisa la sabato Karatu kilichofanyika katika ofisi ya mkuu wa wilaya.
Mchungaji Dikson Mkama wa kanisa la Sabato Karatu amesema wametambua kazi ya kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona ni kazi ngumu. Amesema baada ya kikao cha wadau Mchungaji Mkama alipeleka wito kwa waumini kanisani na kuhamasisha waumini wachangangie na kuunga mkono jitihada za serikali za kupambana na corona. Amesema waumini wamelipokea swala hilo kwa uzito mkubwa ndio maana wamewakilisha mchango wa waumini ofisi ya Mkuu wa wilaya kama sehemu ya jitihada zao za kupambana na vita dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa