Na Tegemeo Kastus
Katibu tawala wa wilaya ya Karatu Ndugu Abbas Kayanda amesema Kijiji cha Endesh na kitongoji cha Kambi ya Simba Tarafa ya Eyasi vitapata maji safi na salama. Mradi huo unatekelezwa na wadau wa maendeleo shirika la world vision Tanzania.
Ndg. Kayanda amesema hayo wakati wa ziara yake ya siku moja kwenye miradi inayotekelezwa na shirika la world vision Tanzania tarafa ya Eyasi. Ziara hiyo ililenga kuona ufanisi wa miradi hiyo katika maeneo mbalimbali. Ndg. Kayanda amesema shirika hilo limepanga kusaidia kuimarisha miundo mbinu ya afya katika kituo cha afya Mbuga Nyekundu. Miradi hiyo kwa pamoja itagharimu kiasi cha billion 1.8, Ndg Kayanda amesema katika mazungumzo yake na viongozi wa shirika la world vision(cluster AP Eyasi) limeridhia kutoa 20% gharama za miradi yake kwa ajili ya kuelimisha wananchi kuhusu ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19).
Ndg. Kayanda ametembelea mtambo wa maji Malekchand uliojengwa na shirika hilo kwa gharama ya million 90 na unauwezo wa kutoa maji kiasi cha milimita 7000 kwa saa. Ametembelea pia mashine ya kukoboa Mpunga Jobaj iliyowekwa na shirika la world vision kwa kushirikiana na LECKOFANET.
Ndg. Kayanda ametembelea shule ya msingi Eyasi na kuona darasa la awali ambalo limewekwa na Maabara yenye vitabu vya kiada na ziada. Lakini pia Shirika la world vision lilishafanya ujenzi wa vyoo katika shule hiyo. Ametembelea shule ya msingi Mikocheni ambayo nayo ina madarasa mawili ambayo nayo yamewekewa madawati pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo. Ametembelea ujenzi wa hosteli ya wasichana shule ya msingi Gidamilanda pamoja na darasa ambalo limejengwa na shirika hilo na kuwekwa Madawati. Amesema sasa shule zilizosaidiwa miundo mbinu na shirika la world vision zinapaswa kuonesha utofauti. Ametoa maelekezo kwa Afisa Tarafa wa Eyasi kukaa na wazazi pamoja na kamati ya shule ya Msingi Eyasi ili watoto waanze kula chakula wakiwa shuleni na watumie muda mwingi kwenye masomo badala ya kwenda na kurudi shuleni. Amesema hiyo itasaidia mahudhurio ya wanafunzi shuleni kuwa mazuri, amesema Mzazi kuchangia chakula ni hiari lakini ni hiari ambayo ukimchangia mtoto chakula inamsaada mkubwa kwake.
katibu tawala Ndg. Abbas Kayanda (katikati aliyevaa kofia) akikagua miundo mbinu ya maji inayoendelea kujengwa shule ya msingi Mikocheni.
Ndg. Kayanda ametoa maelekezo kwa uongozi wa kijiji cha Gidamilanda kuhakikisha wanamaliza kuweka sakafu ya uwanii ili kutengeneza mazingira mazuri kwa wanafunzi wa kike watakaoanza kukaa katika hosteli hiyo. Amesema watoto wanaosoma shule hiyo ni wajamii za kifugaji na wanatembea umbali wa km 22 kwenda na kurudi shuleni. Ndg. Kayanda ametoa maelekezo kwa uongozi wa kijiji kukaa na kujadili ni namna gani wataanza kuwahudumia wanafunzi watakao kuwa wanakaa Hostel ya Gidamilanda ili jengo hilo lianze kutumika pindi shule zitakapofunguliwa. Ndg. Kayanda ameshukuru shirika la world vision kwa kusaidia kujenga miradi ya maendeleo kwa wananchi kwa kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano katika sekta ya elimu,afya na maji.
Kwa upande wake muwakilishi wa Shirika la World Vision, Ndg, Richard Kitomori amesema mwaka wa fedha unaokuja watakuwa na mradi katika kijiji cha Gidamilanda, Endesh lakini pia mradi wa afya utakaolenga kuimarisha miundo mbinu katika kituo cha afya Dumechang na Mbuga Nyekundu. Amesema malengo makubwa ya shirika ni kuhakikisha wananchi wa Lake Eyasi wanapata miundo mbinu ya maji safi na salama. Amesema mradi unalenga kuwafikia watoto wanaoishi mazingira hatarishi kupata huduma elimu na maji ili iweze kuwasaidia, Ndug. Kitomori ameishukuru sana serikali kwa ushirikiano wanaopata katika kutoa ushauri na kutoa michoro katika kutekeleza miundo mbinu ambayo wameitengeneza.
Ndg. Abbas Kayanda (kulia) akikagua maktaba ya vitabu katika shule ya msingi Eyasi.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Gidamilanda Ndg. Selestian Hayshi ameshukuru sana shirika la world vision kwa kutengeneza bweni kwa ajili ya wanafunzi wa Gidamilanda. Amesema shule ya msingi Gidamilanda wanafunzi wamekuwa wakishindwa kuhudhuria masomo, amesema kwa mwaka huu wanafunzi 39 waliandikishwa lakini mpaka sasa wamebaki wanafunzi 16. Ndg. Hayshi amesema wamepokea maelekezo katibu tawala na watayafanyia kazi haraka.
Ndg. Abbas kayanda (kushoto) akiwa na ndg Richard Maasay wakikagua magodoro katika bweni la wasichana shule ya msingi Gidamilanda yaliyotolewa na world vision Tanzania
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa