Na Tegemeo Kastus
Dunia imekuwa kijiji na hatuna budi kuwajengea uwezo wa kitaalamu wanafunzi wa sekondari ili waweze kuendana na Mabadiliko ya sayansi na technolojia. Maudhui ya Masomo ya vitabu vya mitaala na kiada yameanza kuhifadhiwa kwenye mfumo wa (Tehama) computer unaomrahisishia mwanafunzi kupakua na kupata dondoo za masomo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda akifungua semina ya uwezeshaji ya walimu watakaofundisha somo la Tehama (computer) katika shule tisa za sekondari wilayani Karatu. Amewapongeza shirika la WEI Bantwana na SHIDEPHA kwa kusaidia kuleta somo la Tehama wilaya ya Karatu. Amesema serikali imepokea mradi huo kwa moyo mkunjufu sana, kwa sababu wamekuja kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu.
Walimu wakiwa katika semina ya uwezeshaji katika Ukumbi wa Halmashauri ya Karatu.
Walimu hao wanawezeshwa kufundisha somo la Tehama kama mitala ya elimu sekondari inayoelekezwa na wizara ya elimu. Shule ambazo zimewezeshwa walimu kupata uwezo wa kufundisha somo la Tehama ni sekondari ya Awet, Banjika, Endala, Florian, Ganako, Getamock, Mang’ola, Dkt,Wilbroad na Welwel.
Mh. Kayanda amesema kuhudhuria mafunzo ni jambo moja lakini kutekeleza maelekezo unayotakiwa kuyafuata ndio jambo la msingi. Mh. Kayanda amesema walimu wa shule hizo za sekondari tisa watambue uzito wa majukumu waliyopewa ya kwenda kufundisha wanafunzi lakini pia kuwajengea uwezo walimu wenzao katika vituo vyao vya kazi. Amesema kuwapa maarifa ya Tehama walimu wengine kunasaidia somo hilo kuendelea kufundishwa na walimu mwingine pindi mwalimu mhusika wa somo anapokuwa hayupo.
Mh. Kayanda amesema mwalimu lazima aoneshe weledi wa kufundisha somo ili matokeo yaonekana kwa wanafaunzi na muitikio uwe mkubwa wa kusoma na kupenda somo la Tehama. Amesema walimu wanapaswa kumjengea mazingira mazuri mwanafunzi kulipenda somo. Wanafunzi huwa wanaelewa masomo ya vitendo kwa sababu ni rahisi kushika na kufanyia kazi. Amesema matarajio ni kuona wanafunzi wanaopenda kusoma Tehama wanaongezeka na ufaulu wao unakuwa mzuri.
Mh. Abbas Kayanda (kushoto) akifungua semina ya walimu wa (computer) Tehama
Mh. Kayanda amesema mambo mengi sasa yanahusisha Tehama, Mathalani mfumo wa udahili wanafunzi elimu ya juu. Mwanafunzi anaomba kwenye mtandao badala ya kwenda chuo husika kuchukua fomu. Wanafunzi wanapaswa kuona somo la Tehama ni sawa na somo la kiswahili na masomo mengine. Amesema maeneo mengine wanafunzi wanasoma somo la Tehama na kulifanyia mtihani kidato cha pili na kidato cha nne.
Naye Dkt.Herbert Mwashiuya Monitoring and Evaluation Advisor amesema katika kusaidia kuwajengea uwezo wanafunzi shirika la Wei Bantwana wameanzisha klabu za masomo ya Tehama. Amesema kupitia klabu za masomo mwanafunzi ataongeza udadisi zaidi na kulipenda somo la Tehama. Amesema semina imelenga namna ya kuwajengea uwezo walimu katika kuanzisha klabu za masomo ya Tehama ili mwanafunzi aweze kurejea kujikumbusha mambo aliyofundishwa darasani kwa kupitia klabu.
Dkt. Mwashiuya amesema wakati wanaanza kutekeleza mradi wa kufundisha somo la Tehama walikuta shule za Banjika na Welwel ndio zilizokuwa zimeanza kuutekeleza mradi huo wa kufundisha somo la Tehama (Computer).
Mh. Abbas Kayanda akiwa katika picha na walimu wa (Computer) Tehama.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa