Na Tegemeo Kastus
Vituo vingi vya afya vimekuwa na tabia ya kutotoa huduma siku ya Jumamosi na Jumapili jambo linalosababisha adha kubwa kwa wananchi. Sasa uwekwe utaratibu mzuri ili mgonjwa anapokuja kupata huduma aweze kusikilizwa kwa wakati kwa sababu ugonjwa hauna muda maalumu. Kila kituo cha kutolea huduma kiwe na bango la namba za viongozi ili ikitokea changamoto mgonjwa kukosa huduma aweze kutoa taarifa.
Hiyo itasaidia wananchi kufikisha kero zao za kukosa huduma kwa wakati ili ziweze kutatuliwa bila kupata adhaa. Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipotembelea zahanati ya Qurus na zahanati ya Gongali katika ziara yake ya kuangalia upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya wilaya ya Karatu. Mh. Kayanda amebaini utoro kwa baadhi wa watumishi wa afya, kuondoka vituo vya afya hasa siku za mwisho wa juma bila ya kuwa na sababu maalumu jambo ambalo linalochangia kudhorotesha hali ya utoaji wa huduma.
Mh. Abbas Kayanda akikagua hali ya utoaji wa huduma katika zahanati ya kijiji cha Gongali kata ya Qurus
Mh. Kayanda amebaini udhaifu wa kutokuweka mazingira ya kutolea huduma za afya katika hali ya usafi jambo ambalo linatoa taswira mbaya ya utoaji wa huduma za afya. Ameelekeza waganga wasimamizi kuhakikisha wanaweka katika hali ya usafi vituo vya kutolea huduma na kuhakikisha hali ya usafi inaimarika kwenye vituo vya kutolea huduma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vifaa tiba vinavyohitajika katika utoaji wa huduma vinapatikana. Ameongeza kusema rejista ya utoaji wa dawa lazima ijazwe ili kujua dawa zilizoingia na dawa zilozotoka. Mh. Kayanda amesema katika vituo vyote alivyotembelea amebaini upotevu wa madawa ambao umechangiwa kwa kiasi kikubwa na udhaifu wa kujaza rejista ya dawa hivyo kutoa mwanya wa dawa za serikali kupotea. Katika ziara hiyo Mh. Kayanda ametoa maelekezo mahususi kwa mganga msimamizi wa zahanati ya Qurus kuhakikisha dawa zote zinaingia kwenye rejista baada ya kukuta zahanati ya Qurus rejista yake ya dawa haijajazwa tangu mwaka jana 2020 na MSD wameleta dawa mwaka huu ambazo nazo hazijaingia kwenye kwenye rejista na wala hazijapangwa kwenye chumba cha dawa.
Mh. Kayanda akimjulia hali mama aliyekuja kupata huduma ya afya katika zahanati ya Gongali
Mh. Kayanda amebaini uzembe wa mganga wa zahanati ya Qurus kutokuwa na chanjo ya polio jambo lilosababisha zahanati hiyo kushindwa kutoa chanjo ya polio kwa watoto wadogo. Amemueelekeza mganga msimamizi wa zahanati hiyo kuhakikisha jumamosi amepata chanjo ya polio katika kituo chake cha kutoa huduma na kuitoa kwa watoto. Ikiwa ni sambamba na kugawa vyandarua kwa kinamama wenye watoto wa changa na kuhakikisha hakuna mwananchi anayeenda kununua dawa kwenye maduka binafsi kwa sababu dawa zinaletwa na serikali.
Katika hatua nyingine Mh.Kayanda amemuelekeza Mganga Mkuu wa wilaya kuandika barua bohari ya madawa MSD ili kuhakikisha wakati wa usambazaji wa dawa kwenye vituo na zahanati kamati za dawa za vijiji zinashirikishwa kikamilifu katia makabidhiano. Amesema hiyo itasaidia kamati za dawa kujua ni dawa kiasi gani zimeletwa katia kituo cha afya ili viongozi wa kamati watoe taarifa kwa wananchi. Badala ya mtindo wa sasa ambao hauendani na sera ya afya ambao watu wa bohari ya dawa wanakabidhi dawa kinyemela kwa wahudumu wa afya peke yake.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa