NA TEGEMEO KASTUS
Timu maalumu ya uchunguzi itakayohusisha Maafisa wa Tanapa ziwa Manyara na vyombo vya ulinzi na usalama itafanyaa uchunguzi wa ng’ombe wa tatu waliouliwa kwa kupigwa risasi. Ili kufahamu undani wa ng’ombe waliouliwa ulifanyika ndani ya hifadhi au nje ya hifadhi ya ziwa Manyara.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Buger katika mkutano wa hadhara. Amesema timu ya uchunguzi itakapokuja lazima ije iripoti kwa Uongozi wa kijiji cha Buger, ili iweze kupata ushirikiano wa viongozi na wananchi wa Buger. Uchunguzi utakapodhibitisha kwamba askari wamechukua maamuzi nje ya utaratibu, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao ili iwe fundisho kwa askari wengine wenye tabia kama hizo kuacha kujichukulia maamuzi nje ya utaratibu.
Mh. Abbas Kayanda akizungumza na wananchi wa Buger katika mkutano wa hadhara
Mh. Kayanda amekemea pia tabia ya askari wa hifadhi kuvamia makazi ya watu nyakati za usiku amesema huo siyo utaratibu mzuri. Amesema kama kuna mtu amekosea, utaratibu wa kisheria lazima uendelee kufuatwa. Kuvamia mtu usiku ni hatari kwa askari mwenyewe lakini hata kwa mwananchi inafanya watu wanaishi kwa hali ya wasiwasi. Wananchi wanapaswa kuwa huru kufanya shughuli zao katika kijiji kwa amani halikadhalika askari wa hifadhi nao wako huru kufanya kazi zao.
Mh. Kayanda amewaomba wananchi kuendelea kuheshimu makubaliano yaliofikiwa mwaka jana kati ya wananchi na viongozi wa hifadhi ya ziwa Manyara kuhusiana na kutoingiza mifugo kwenye hifadhi. Amesema hifadhi ikivamiwa na kila mtu, mwisho wa siku kutakuwa hakuna hifadhi, na itakuwa ni hasara kwa nchi yetu. Moja ya mambo walikubaliana ni pamoja na kutoza faini Mifugo itakayokamatwa ndani ya hifadhi kwa mujibu wa sheria, na kuendelea kuishi kwa amani na upendo kati maskari wa hifadhi ya ziwa manyara na wananchi wanaoishi kuzunguka hifadhi ya ziwa Manyara.
Naye Kamishina Msaidizi wa Tanapa Ndg. Herman Batiho amesema sheria inamtaka mtu anayetaka kuingia kwenye hifadhi kupata kibali cha wenye mamlaka. Sheria za hifadhi haziruhusu mtu kufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya eneo la hifadhi, ikiwa ni pamoja na uwindaji, kukata miti na kulisha mifugo. Amesema mtu anayebainika kufanya mambo kama hayo sheria imeweka wazi kiasi cha faini kilichopitishwa na bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Mh. Abbas Kayanda katika matukio tofauti wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Buger
Kamishina Msaidizi ndg. Batiho akizungumzia tukio la kuuawa ng’ombe lilofanyika, amesema hakuna kiongozi wa hifadhi aliyeelekeza askari kufanya tukio kama hilo. Askari wamepewa vitendea kazi vya kufanya kazi ya kulinda hifadhi amesema baada ya tukio hilo lilojitokeza ni vizuri kupata chanzo cha tatizo hilo kwa kuunda timu ya uchunguzi na ikibainika mshukiwa achukuliwe hatua za kisheria na kiutumishi zitachukuliwa na TANAPA.
Mama mwenye mifugo iliyouliwa Bi, Roziana Emmanuel amesema ng’ombe wake walikuwa kwenye malisho shambani kwake nyumbani mida ya saa tano asubuhi, kabla ya kuuwawa na askari wa hifadhi. Bi, Roziana amemuomba mkuu wa wilaya ya Karatu kusimamia changamoto hiyo ili iweze kutatuliwa.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa