Na Tegemeo Kastus
Wananchi mnapaswa kujivunia uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi unaofanywa na serikali. Zahanati ya Jobaj ni moja ya zahanati tatu wilayani Karatu zilizopata million hamsini kwa ajili ya ukarabati wa zahanati.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipokagua jengo la nyumba ya mganga lilojengwa kwa nguvu ya wananchi. Amewapongeza wananchi hao kwa moyo wa kizalendo wa kuboresha miundo mbinu ya afya. Amesema serikali imetoa fedha kwa ajili ya kukarabati zahanati ya Jobaj zahanati ya Mang’ola juu, na zahanati ya kijiji cha huduma ambazo kwa pamoja zimepata kiasi cha million 150. Amesema zahanati hizo zikishamaliza kukarabatiwa majengo, huduma za afya zitakuwa za kisasa.
Katika ziara hiyo mkuu wa wilaya alikagua hali ya upatikanaji wa dawa na kufanya mkutano wa hadhara. Amesema serikali ya awamu ya tano inyoongozwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeboresha huduma za afya kwa kiwango kikubwa. Amesema kuna makundi maalum ambayo yanapata huduma za afya bure kama watoto chini ya miaka 5 kinamama wajawazito na wazee ambayo kwa vituo vya afya vya binafsi wanalazimika kutoa fedha.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda akikagua zahanati ya Jobaj.
Amesema zahanati ya Jobaj ina uwezo wa kuhudumia wakinamama wajawazito kati ya 12 mpaka kinama 13. Amesema wananchi wakijiunga na mfuko wa bima ya afya utasaidia kuongeza upatikanaji wa dawa katika zahanati hiyo. Hivyo ametoa rai kwa wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa ili iweze kujengea uwezo zahanati hiyo kupata dawa nyingi ambazo zitasaidia kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa.
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda amewaomba wananchi kupeleka watoto waliochaguliwa kidato cha kwanza kwenda shule. Amesema hakuna urithi mkubwa utakaomuachia mtoto kama elimu. Ameongeza kusema mtoto akisoma inamsaidia kujenga misingi bora ya kujitegemea, ambayo ni tofauti na mtoto aliyenyimwa kwenda shule. Mtoto aende shule hata kama hana sare ili mzazi utafute sare wakati mtoto akiendelea kusoma.
Katika mkutano huo wa hadhara Mh. Kayanda ametoa maelekezo mahususi kwa wazazi wa kijiji cha Jobaj kuhakikisha wanachangia chakula kama walivyokubaliana katika mkutano wa kijiji. Ameelekeza mwisho wa kuchangia chakula uwe mwezi wa pili mwishoni, na ameelekeza eneo la shamba la shule ya msingi Jobaj, ambalo serikali ya kijiji ikishirikiana na wazazi iliazimia kulilima mwezi wa tisa mwaka huu wahakikishe wanaanza kulima kwa kuzalisha mahindi ili kusaidia upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wa shule ya msingi Jobaj.
Amesema malengo yaliowekwa na serikali ya kijiji ya kutenga sehemu ya shamba la shule, ni makakati mzuri wazazi wanatakiwa kusimamia ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula cha wanafunzi unafanikiwa.
Wananchi wakichangia katika mkutano huo ndugu Emmanuel Mgana amesema swala la afya halina mbadala. Amesema ni vyema kukata bima ya afya iliyoboreshwa iwe sheria badala ya kuwa swala la hiari kwa sababu itasaidia zahanati ya jobaj kupata dawa za kutosha.
Mh. Abbbas Kayanda akiwa katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Jobaj.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa