NA TEGEMEO KASTUS
Mradi wa maji wa Getamock ulioshindwa kufanya kazi kwa muda miaka zaidi ya nane, sasa umeanza kufanya kazi. Mradi huo uko chini ya uangalizi wa ruwasa na una vituo vya kutolea maji ishirini na sita ambavyo vimeanza kutoa maji katika kata ya Endamarariek.
Hayo yamebainika katika ziara ya mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipotembelea kata ya Endamariek kukagua shughuli za maendeleo. Mh. Kayanda amesema ni wakati sasa wa jumuiya za watumia maji kusimamia miradi huo vizuri ili uweze kuleta manufaa kwa wananchi. Ameongeza kusema fedha za makusanyo ya huduma ya maji ziwekwe katika akaunti ya jumuiya ya watumia maji Getamock ili kuepusha watu kutumia fedha mbichi. Fedha hizo ndizo zitasaidia kurekebisha miundo mbinu ya maji na kusaidia mradi kujiendesha.
Mh. Abbas Kayanda akiwa katika dp ya maji katika kijiji cha Getamock
Mh. Kayanda ametoa mda wa siku tisa ili fedha zote zilizokusanywa ziwe katika akaunti iliyofunguliwa na jumuiya ya watumia maji Getamock. Wakati huo huo Mh. Kayanda amemuagiza mkaguzi wa ndani kufanya ukaguzi wa fedha hizo ili kujiridhisha kama hakuna ubadhilifu uliojitokeza.
Mh. Kayanda ameomba wananchi kuheshimu wataalam wa fedha watakaokuwa wanasaidia kusimamia mapato na matumizi ya fedha katika jumuiya ya watumia maji. Lengo ni kusaidia shughuli za fedha kuendeshwa kitaalamu kulingana na sera na miongozo ya serikali. Amesema usimamizi wa maji utakuwa mzuri, na utajenga utamaduni wa kutoa taarifa za mapato na matumizi. Miradi ya jamii lazima iendeshwe kwa uwazi na huo ndio utendaji kazi mzuri. Mh. Kayanda amepongeza wakala wa maji vijijini kwa jitihada walizofanya za kufufua mradi wa maji. Amesema matokeo sasa yanaonekana hii inatokana na juhudi za serikali za kuiweka miradi ya maji chini ya wakala wa maji vijijini.
Mhandisi Baraka Kilangai akimueleza Mh. Abbas Kayanda namna mfumo wa maji utakuwa unavyofanya kazi.
Mh. Kayanda amekemea tabia ya watu wasio waaminifu kuhujumu miundo mbinu ya maji, ameelekeza uongozi wa kijiji kusimamia na kulinda kikamilifu miundo mbinu ya maji. Lazima tujenge nidhamu ya kulinda rasilimali za maji, kwa mtu mmoja mmoja kuwajibika kusimamia usalama wa miundo mbinu ya maji ili kukomesha tabia za kukata kata mabomba ya maji.
Naye wakala wa maji vijijini Ruwasa Mhandisi Baraka kilangai katika taarifa yake amesema wakala wa maji vijijini wamerekebisha km 8.9 kati ya km 14 zinazotakiwa kurekebishwa. Amesema katika kipindi cha matazamio walichojiwekea maji yanatoka vizuri japokuwa kuna wakati maji yanatoka kwa kusuasua. Mhandisi Kilangai amesema mkakati wao ni kuhakikisha wanamalizia sehemu ambazo hawajazifanyia marekebisho ili watu wapate maji bila kuwa na changamoto yoyote.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa