NA TEGEMEO KASTUS
Aliyekuwa kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Endamariek anachunguzwa na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa wilaya ya Karatu juu ya matumizi mabaya ya ofisi. Tukio hilo limejitokeza baada ya wananchi kulalamika kukosekana kwa uwazi wa uendeshaji wa miradi inayosimamiwa na Halmashauri ya kijiji cha Endamarariek.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Endamarariek. Amesema kumekosekana uwazi wa mapato na matumizi katika shamba la kijiji cha Endamarariek na hivyo kumuelekeza kamanda wa takukuru wilaya ya Karatu kuchunguza juu ya mradi wa shamba la kijiji cha Endamarariek.
Sambamba na mradi huo Mh. Kayanda ametoa maelekezo kwa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kuchunguza mradi wa shambala miti katika kijiji hicho. Lakini pia Kuchunguza mradi wa trekta ili kujua mapato na matumizi pamoja na mradi wa maji katika kijiji hicho.
Mh. Kayanda amesema taarifa ya mapato na matumizi kusomwa kwa wanachi ni haki yao ili kujua taarifa ya mwenendo wa mapato na matumizi katika Halmashauri ya kijiji. Amesema ndio maana serikali imeweka utaratibu kwa Halmashauri ya kijiji kusoma mapato na matumizi kila baada ya miezi mitatu. Ametoa rai kwa wananchi kuitikia wito pindi wanapoitwa kwenye vikao vya Halmashauri ya kijiji ili kusomewa mapato na matumizi.
Mtendaji wa kata ya Endamarariek ndugu Azizi Mfundo amemshukuru Mkuu wa wilaya ya Karatu kwa kusaidia kutatua mgogoro wa ghala la kijiji ambao ulidumu kwa muda mrefu. Ghala hilo limerudi kwenye umiliki wa kijiji lakini pia kwa kutatua mgogoro wa mipaka ya barabara ambao ulisababisha ukarabati wa barabara kusimama kwa muda. Ndugu Mfundo amemshukuru Mkuu wa wilaya kwa kuwasaidia kupata mtendaji wa kijiji mpya, kijiji cha Endamarariek ni moja ya vijiji vilivyokuwa vikikaimiwa na watendaji wa kijiji kwa muda mrefu.
Wakati huo huo mkuu wa wilaya ametembelea na kuifungua zahanati ya Mahhahhaa na ambayo ilikuwa imekaa muda mrefu kwa kukosa watumishi. Mh.Kayanda amewaomba wananchi wa Mahhahha kuwapokea watumishi hao waliopelekwa katika kituo hicho. Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha huduma za afya zinapatikana karibu na maeneo wanayoishi wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Karatu, Mh. Abbas Kayanda akizungumza na wananchi wa Mahhahha
Zahanati ya Mahhahha imejengwa baada ya Mh. John Lucian kutafuta Mfadhili kutoka Beligium ndugu Erick Maes aliyetoa million 96 Pamoja na nguvu za wananchi. Baada ya kukamilika zahanati hiyo imepewa jina la Gerti Maes Memorial clinic kama sehemu ya kumbukumbu ya Mke wa mfadhili huyo aliyefariki kwa matatizo ya kansa. Zahanati hiyo inavifaa vya kisasa pamoja na madawa kwa ajili ya kuanza kutoa tiba. Inatarajiwa kuhudumia wananchi 2120 wa Mahhahha na vijiji vingine vya jirani.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa