Na Tegemeo Kastus
Sekta binafsi ndio waajiri wakubwa na walipaji wakubwa wa kodi ya serikali, sekta binafsi ndio wachangiaji wakubwa wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali. Kazi ya serikali ni kuimarisha ulinzi na usalama ili kuwezesha taasisi binafsi ziwe na mazingira wezeshi kwa wawekezaji kufanya kazi vizuri. Lazima tuwe na eneo kwa ajili ya uwekezaji kwa ajili ya kuwavutia kufanya shughuli za biashara.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipokuwa akizungumza katika kikao cha baraza la biashara la wilaya ya Karatu kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri. Amesema lazima baraza la biashara liwe na one stop centre sehemu ambayo muwekezaji atapata taarifa mbalimbali za fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Halmashauri ya wilaya ya Karatu.
Wajumbe wa baraza la biashara la wilaya ya Karatu wakiwa katika kikao
Mh. Kayanda amesema kuna fursa ya kupeleka mazao ya vitunguu nchini Qatari lakini wananchi hawafahamu kama kuna fursa hiyo. Kuna wawekezaji wa kutoka nchini Kenya wanataka kujenga kiwanda cha kuchakata mbaazi, kama tunahitaji kuleta mabadiliko ya kiuchumi inabidi tuanze kutengeneza mazingira wezeshi ya uwekekzaji.
Mh. Kayanda amesema ni jukumu la Halmashauri kutangaza fursa zinazopatikana ili kujenga uelewa mkubwa kwa wananchi, ameongeza kusema kama hatutaweza kuwekeza na uwekezaji utaendelea kuwa duni. Ametoa mwelekeo kwa baraza la biashara kuja na taarifa za fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Halmashauri ya wilaya ya Karatu. Ametumia nafasi hiyo kulitakia heri baraza linalomaliza muda wake wa uongozi baada kufanya kazi kwa kipindi cha miaka minne. Amesema baraza hilo limefanya kazi nzuri na nijukumu la wajumbe wapya wa baraza la biashara kubeba na kuhuisha jitihada zilizofanywa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu Mh. John Lucian akizungumza katika kikao hicho amesema Halmashauri itaweka mfumo mzuri wa mawasiliano na ushirikiano mkubwa kwa baraza la biashara. Ikiwa ni pamoja na kujikita katika kutoa elimu kwa wananchi na umma juu ya fursa za uwekezaji zinazopatikana. Ikiwa ni sambamba na Halmashauri kutenga eneo maalumu kwa ajili ya wawekezaji kujenga viwanda.
Amesema Halmashauri inakusanya ushuru katika sekta ya mifugo sekta ya kilimo na sekta ya biashara ili kupata fedha zinazosaidia kutekeleza miradi ya maendeleo. Mh. Lucian amesema Halmashauri itaweka sera nzuri, na mazingira rafiki kwa sekta zote ili muwekezaji anufaike na uwekezaji atakaoufanya na aweze kutoa ushuru kwa Halmashauri.
Mh. Abbas Kayanda akizungumza na wajumbe wa baraza la biashara la wilaya ya Karatu.
Ndg. Charles Goranga Mwenyekiti wa baraza la biashara linalomaliza muda wake wilaya ya Karatu amesema vikao vya baraza la biashara vimekuwa vikisuasua kufanyika kutokana na ushirikiano duni uliokuwepo awali.
Amesema ni wakati sasa kwa baraza la biashara kufanya kazi kwa pamoja na wadau wengine ili kuendana na kasi ya mahitaji ya watu.
Akichangia katika kikao cha baraza la biashara Mkuu wa kituo cha polisi Karatu ndg. Henry Mwansansu amesema kuna malalamiko makubwa ya kukosekana kwa soko la mahindi. Hivyo kuongeza vitendo vya udanganyifu kwa wakulima katika biashara ya mazao ya chakula, amesema ni vyema baraza la biashara likasaidia kuwalekeza wakulima njia bora za kupata wateja wa zao la mahindi. Amesema kesi za utapeli wa uuzaji wa zao la mahindi zimeongezeka kutokana na wakulima kutokuwa na taarifa sahihi za bei ya soko na sehemu ya uhakika ya kuuza mazao yao.
Wajumbe wa baraza la biashara la wilaya ya Karatu wakiwa katika kikao
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa