Afisa elimu sekondari ameendelea na ziara yake kutembelea shule za sekondari katika wilaya ya karatu. Shule za sekondari Awet, Upper kitete na Slahamo sekondari zimefikiwa na kukaguliwa utendaji wa kazi wa walimu wa shule hizo.
Katika ziara hiyo afisa elimu sekondari Bi, Kalista Maina amebaini mahudhurio hafifu kwa walimu kwenye kuingia na kufundisha darasani. Licha ya sababu mbalimbali zinazotolewa na walimu hao kama kuwa na vikao au shughuli za dharura kutokea, afisa elimu amesema ni vyema wakawa wanaandika tarifa hizo za upotevu wa vipindi kwenye (class journal) daftari la mahudhurio ya vipindi darasani.
Bi, Maina amebaini udhaifu wa walimu kushindwa kushirikiana kwa pamoja katika ufundishaji, ili kusaidiana na kupeana mbinu pamoja ubunifu wa kufundisha watoto. Amesema kuwa na mitihani mingi ya ndani na nje inasaidia kwa sababu maswali yanatabia ya kujirudia. Amehoji kama kuna mwalimu anafaulisha masomo yote hana “F” iweje mwingine asijifunze mbinu za mwalimu aliyefanya vizuri.
Bi. Maina amesema ziara yake itamsaidia pia kutoa maoni wakati wa kujaza fomu za opras kwa walimu lakini pia wakati wa kupanda daraja. Amesema kama mwalimu unaomba kupanda daraja na matokeo yako ya mtihani sio mazuri amesema hawezi kutoa maoni ya kuomba upandishwe daraja. Lazima ubunifu na ufanisi katika kazi uonekane ili uwe katika sehemu nzuri ya kupanda daraja.
Bi. Maina ametoa maelekezo kwa walimu wa shule ya sekondari Slohamo wanaofundisha kidato cha nne kuandika barua za kujieleza kwanini wamefanya vibaya. Ameelekeza pia walimu waliopata “F” zote kwenye masomo yao mtihani wa Moko kidato cha nne kwenda kwa Mwajiri kujieleza. Amesema walimu wa Slohamu wanavielelezo vizuri vya namna wanavyotekeleza majukumu lakini matokeo ya Moko kidato cha nne hayaendani na taarifa walizojaza.
Ukaguzi ukiwa unafanyika shule ya Upper kitete
Naye Afisa elimu taaluma Ndugu Robert Sijaona amesema mwalimu ni mtu mwenye uwezo wa kumuelewesha mtu asiyejua kufahamu. Amesema mitihani unatungwa na walimu kwa malengo ya kumpima mwanafunzi. Ameomba walimu kujitafakari mbinu wanazotumia, amesema watoto wanauwezo. Ndugu Sijaona ameongeza kusema; mwalimu unajisikiaje, unapopata “F” wanafunzi wote, itafika kipindi hata kazi itakushinda. Lakini wanafunzi hao hao wanapata D, wanapata C masomo mengine. Mwalimu lazima utambue namna ya kwenda na mwanafunzi ili aweze kuelewa, maswali yote yanatoka kwenye silabasi. Amesema ni vyema kutumia maneno yalioanishwa kwenye silabasi wakati wa ufundishaji. Kuna maneno (misamiati) ambayo inatumiaka kuelekeza namna ya kufundisha, maneno hayo hayo yanatumika katika kuuliza mtihani.
Ndugu Sijaona amesema maneno kama, Bainisha, Fafanua, Elezea, Taja ni maneno yanayotumika kwenye silabasi. Tutumie maneno hayo kueleza namna ya kujibu maswali yanayotumia maneno tofauti tofauti katika ulizwaji wa maswali. Hii itamsaidia mwanafunzi kufahamu na kuongeza uwezo wa kuijibu maswali kwa ufasaha. Masomo ambayo wanafunzi wanapata “F” ndio yanayochangia ufaulu wa shule kuanguka.
Ukaguzi ukiwa unafanyika shule ya Slohamo
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa